Wazazi tujitambue, malezi sawa kwa jinsi zote muhimu, tusibague

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:07 AM Jun 14 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.
Picha: Mtandao
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.

WAZEE wamesema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Msemo huu unanikumbusha madai kuwa baadhi ya kaya hufanya ubaguzi baina ya watoto kiume na wa kike katika kuwalea.

Ubaguzi huo hufanyika  baada ya mtoto wa kiume kupewa nafasi kubwa ya kusoma  na mtoto wa kike kupata nafasi  ndogo. Mtoto wa kike hupewa nafasi kubwa ya kuandaliwa kuolewa.  

Dhana ambayo inadaiwa kuwa ni potofu.

Dhana hiyo imezidi kuzua mjadala pale ambao kupigwa vita na vyombo mbalimbali,  vikiwamo taasisi na asasi za kiraia zisizokuwa za kiserikali za kutaka  haki sawa kwa watoto wa jinsi zote mbili  za kike na kiume.

 Tatizo hilo la ubaguzi linaendelea hadi sasa katika kulea watoto hao jinsi mbili hadi majumbani.

 Katika malezi majumbani, baadhi ya walezi ama wazazi huwalea kibaguzi kwa kuwafunndisha tabia ambazo  inawadumisha watoto kuona jambo fulani  ni la kike na lingine ni la kiume.

 Utaratibu huo unasababisha pasiwepo na maelewano katika jamii jambo linaleta madhara.

 Kuna baadhi ya wazazi na walezi huwanunulia vifaa vya kuchezea vikiwamo midoli na matoi  katika hali ya kuwatuliza na kuendelea na kazi zao lakini wakati huo huo wapate  kujifunza kupitia hayo madoli ama vifaa vya kuchezea.

 Lakini sasa, wazazi walezi hao huamua kuwanunulia watoto wa kiume vifaa hivyo vikiwamo magari, ndege, magari moshi na meli wakati watoto wa kike wanawanunulia wanasesele, ambayo hubeba sura za watoto hivyo huyabeba na kuyalea kama watoto.

 Jambo hili huwafanya watoto kuwa na maarifa ya kulea watoto wakati watoto wa kiume hupata maarifa ya kiufundi ya kuendesha magari, ndege, meli au magari moshi hali ambayo inawafanya watofautiane kimaarifa hayo ya kiufundi jinsi hizo mbili.

 Tofauti hiyo inawafanya jinsi hizo mbili kuwa na mtazamo tofauti  matokeo yake  kunazuka migogoro kati ya mwanamke na mwanaume ya maslahi hususani kwenye ajira za kiufundi.

 Tofauti hii, inaashiria kuwa jinsi hizi mbili kuona kuwa moja haistahili kujifunza mambo hayo ya kiufundi na mwingine anastahili hatimaye kuleta mgogoro baadaye, kwamba malalamiko mengi yanatolewa kwamba jinsi ya kike inakandamizwa.

 Mtoto wa kiume ana mazoea ya kujishughulisha na kazi za kiufundi na kamwe hastahili kubeba watoto. Kwani anajiona, si mtu kwa hivyo mtoto wa kike ndiye anayestahili kubeba mtoto kwani tangu utoto kwake alijifunza kubeba mwanasesele.

 Hivyo, ikitokea fursa ya kazi ya kiufundi kama kuendesha gari, gari moshi, meli, ama ndege anapewa mtoto wa kiume ambaye  tayari  na maarifa ya kuendesha na hata kwa uzoefu alioupata hususani darasani.

 Hali hiyo huwa mbaya zaidi pale ambapo mtoto wa kike ambaye ni mwanafunzi akiwa darasani hushindwa kufuatilia masomo ya sayansi shule, kwa kuwa hana uchangamfu wa masuala ya sayansi na hivyo kuachwa nyuma kimasomo na kimaendeleo.

 Matokeo yake hivi sasa kumezuka malalamiko mbalimbali kiasi cha baadhi ya wanawake kudai haki za usawa, baina ya wanaume na wanawake.

 Ikibidi walezi na wazazi wabadilike, kuacha tabia hiyo ya ubaguzi, ili kuwapa fursa watoto wote wapate malezi bora sawa, kwani kufanya itawafanya  watoto kuwa  sawa hadi utu uzima.