Wanasiasa acheni ‘bla blaa’, hamasisheni kuandikisha wapigakura uchaguzi ujao

Nipashe
Published at 11:08 AM Jun 14 2024
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacob Mwambegele.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacob Mwambegele.

WAKATI Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imetangaza kuanza kwa uboreshaji wa daftari la wapiga kura nchini mwezi ujao, kumekuwa na mikutano ya wanasiasa katika maeneo mbalimbali nchini, ili kutetea ulaji wao katika mitaa.

Pilikapilika za wananasiasa hao zimeshika kasi, wakati ikiwa zimesalia miezi kadhaa wananchi kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa  nchini kwa ajili ya kuwaletea maendeleo. 

Mikutano hiyo imeanza kushika kasi katika siku za hivi karibuni, kwa baadhi ya wanasiasa wakiwemo wawakilishi wa wananchi kwenye mitaa, kata na majimbo nchini kuitishia mikutano ya wao kwa wao, kwa ajili ya kuwekana sawa, ili kujihakikishia ushindi. 

Katika mikutano hiyo ya wawakilishi wa wananchi, wamekuwa wakihimizana na kupanga mikakati ya kuhakikisha wanaendelea kutetea nafasi zao na kujihakikishia ushindi kwenye nafasi za uenyekiti. 

Hapo wanaelekezana jinsi ya kuwaelimisha wananchi utekelezaji wa miradi ya maendeleo na miundombinu katika maeneo yao, kama njia ya kuwashawishi kuendelea kuwachagua katika uchaguzi huo utakaofanyika baadaye mwaka huu kwa kuvishirikisha vyama vingi vya siasa.  

Katika kuwekana sawa, wawakilishi hao wanakosoa tabia ya baadhi yao, kuunga mkono watu wanaowakashifu wenzao vijiweni ambako kuna makundi ya watu wanaolalamika huduma duni kwa kuwataja moja kwa moja viongozi kutokana na huduma duni. 

Badala yake, wanaelekeza jinsi ya kupangua hoja zenye mijadala mibaya dhidi ya viongozi, wanasiasa kwa kuvutia upande wao kwa kusifia mazuri yanayofanyika katika jamii. 

Wakati hayo yakijiri, wawakilishi hao wa wananchi wanasahau kuwa jamii inalalamikia huduma duni katika maeneo yao na kutaka kupatiwa ufumbuzi. 

Jamii hiyo imekuwa ikilalamika kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara kutokana na kuharibika vibaya na hadi nyingine kugeuka mahandaki. 

Ubovu huo wa Barabara, umesababisha maeneo mengi kukosa usafiri kutokana na magari kushindwa kupita huku nyingine zikigeuka madimbwi kutokana na kujaa maji yanayotokana na mabomba kupasuka. 

Pamoja na kero hizo sugu kuliko zote, ni kuzagaa kwa takaa kwenye makazi ya watu, kutokana na magari kushindwa kwenda kwenye maeneo hayo, hasa mijini, kusomba na kupelekwa kutupwa kwenye madampo. 

Vilevile kuna kuwapo mlundikano wa takataka kwenye makazi, kunahatarisha kutokea kwa mlipuko wa magonjwa yanayoenezwa na nzi na wadudu wengine. 

Magonjwa hayo yanaweza pia kuwakumba watoto wadogo wanaocheza kwenye maeneo ziliko takataka na kusambaa kwa kasi kwa watu wengine. 

Chakushangaza, wawakilishi hao hususani  wajumbe ambao wanaishi kwenye maeneo hayo na wananchi, lakini wanashindwa kuchukua hatua zozote za kukabiliana na changamoto hizo badala yake wanaibuka msimu unapokaribia uchaguzi. 

Hapo wanaanza kupita huku na kule wakihaha kushawishi wananchi kuchagua vyama vyao vya siasa ili kuwaongoza katika kipindi kingine. 

Sisi wanajamii sasa tunahoji wawakilishi wetu, kama hawaguswi na kero hizo, tunawashangaa kwa kuendelea kutulaghai kwa kusaka ulaji kwa kuendesha mikutano hiyo katika maeneo yao. 

Badala yake, wawakilishi wangetumia muda wao huo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika uboreshaji wa daftari hilo badala ya kujipanga kupangua hoja na malamiko dhidi yao kwa manufaa ya jamii. 

Kuhamasisha wananchi kujiandikisha kupiga kura ni jambo muhimu zao kwa sababu ndio wakati wake ili kupata idadi kubwa ya wanananchi watakaojitokeza kuchagua viongozi wao katika kipindi kijacho. 

Baada ya kufanikisha hilo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari hilo ambalo limekuwa likifanyika unapokaribia uchaguzi huo na ule mkuu, ndipo ufuate utaratibu mwingine ikiwemo wanasiasa kuelekezea utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huduma za afya na mambo mengine mengi. 

Wananchi ni mashahidi wa yale yanaendelea katika maeneo yao, hata wanafunzi wa shule za msingi wanasikika wakicheka na kuwabeza wawakilishi hao kwa kutoa ahadi kibao, ikiwa ni pamoja na kuweka taa barabara za mitaani na kuhoji wameshindwa kutengeneza barabara, huku maji yakitiririka ovyo babarabani watawezaje kufanikisha hilo.  

Kwa mtindo huo msije mkashangaa mkizomewa kwenye mikutano yenu, mnapopita barabarani na hata mnapojinadi na wagombea wenu. Jamani jirekebisheni, ndugu zetu wanasiasa.