Wajumbe Simba tangulizeni maslahi ya klabu, siyo yenu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:14 AM Jun 10 2024
Mkutano  Mkuu wa Klabu ya Simba.
Picha: Mtandao
Mkutano Mkuu wa Klabu ya Simba.

WAKATI Simba ikifanya vibaya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, upande wa mwekezaji na wanachama walikuwa kimya.

Wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wakinung'unika, wakiwa na maswali mengi ya kujiuliza, kwa nini kikosi chao kinacheza vibaya, kina mapungufu, na hakishindi kwa 'swaga', bali papatupapatu, walikosa watu wa kuwaambia kitu.

Wakawa wanaulizana wenyewe kwa wenyewe bila kupata jibu, matokeo yake wakagawanyika na kugombana wao kwa wao.

Ni mtu mmoja tu angalau alikuwa anaweza kutoka na kuwafariji Wanasimba, naye ni Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally.

Ahmed ndiye aliyeonekana kuwa karibu na wanachama na mashabiki, akawa kiunganishi pekee kati ya timu, uongozi na wenye timu yao kwa maana ya mashabiki.

Mambo yaliendelea kuwa mabaya, lakini hakuna mjumbe yeyote aliyejitokeza kuelezea sababu ya timu hiyo kufanya vibaya.

Wote wako kimya na walionekana kama vile hawajui wajibu wao kwamba wanapaswa warudi kwa waliowaweka madarakani kuwaambia kila kitu kinachotokea.

Hawakujali manung'uniko, machungu na maumivu ya wanachama na mashabiki. Hata ligi ilipomalizika, bado  walikuwa kimya. Wakati wenzao Yanga wakiwa wameitisha Mkutano Mkuu, wao waliendelea 'kuuchuna'.

Ndipo Mwekezaji na Rais wa Heshima wa Klabu hiyo akaibuka na kuwataka wajumbe wote walio upande wake wajiuzulu. 

Inasemekana wengine wamegoma. Baadhi ya wanachama wanaona isiwe tabu, wakawataka na wa upande wao kuachia ngazi kabla hawajachukua hatua za kikatiba.

Sasa ndipo tukaona wajumbe ambao siku zote walikuwa 'wameuchuna' wakijitokeza. 

Ni kama walikuwa wamejificha kwenye mashimo. Cha ajabu badala ya kwenda kumaliza kiu ya wanachama na mashabiki kwa nini msimu huu timu imefanya vibaya, imekuwaje wamesajiliwa wachezaji ambao wanaonekana wana viwango vidogo, na kwa nini muda wote timu inafanya vibaya wao wako kimya, wao ametoka moja kwa moja na kuitisha kikao na viongozi wa matawi kuelekezea uwekezaji wa Mo, kasoro zake, na mambo mengine ambayo ukiyasikiliza utagundua kuwa wanachofanya ni kuhamisha ajenda, yaani waonekana kuwa wao wapo safi, tatizo lipo kwa Mo.

Mo huyu huyu ambaye ameipa Simba ubingwa misimu minne mfululizo, leo amegeuka na kuwa mbaya. 

Mo ambaye anadaiwa kuwa hatoi pesa, lakini wajumbe hawataki kujiuzulu. 

Unachojiuliza kama pesa hakuna, kwa nini wanang'ang'ania na imekuwa kwao ngumu kuwajibika?, ina maana wao ndiyo wanataka kutoa pesa za usajili?, wao ndiyo watakuwa na pesa za kuwalipa wachezaji mishahara?.

Ikumbukwe Simba kabla ya Dewji, ilikuwa ikipiga mechi za 'ndondo' ili kupata pesa za kujikimu.

 Timu ilikuwa inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi maeneo ya Sinza, ikiwa haina hata mashabiki wanaokwenda kuangalia mazoezi ndiyo wanaochangia pesa waliokuwa nayo ili zinunuliwe katoni za maji.

Nilidhani kama wana hoja za msingi, kwa nini wasiitishe Mkutano wa dharura wa wanachama wote, badala ya kusaka watu wachache tu ambao ni viongozi wa baadhi ya matawi, Dar es Salaam?.

Mimi nadhani wajumbe hawana hoja, na huku ni kutapatapa baada ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanachama kuwa wajiuzulu, wameshindwa kuiongoza klabu.

Soka ni mchezo wa wazi, inaonekana kabisa Wajumbe na Bodi wamefeli, na hili limeelezwa na hata na mchezaji, Fondhoh Che Malone, na kocha wa makipa, Daniel Cadena ambao kwa nyakati tofauti wamesema tatizo la Simba lipo kwenye uongozi. Hawajasema mwekezaji. Na hii wala haihitaji elimu ya Chuo Kikuu kufahamu hilo.

Kumtupia lawama Mo ni kutapatapa kwa sababu Mo ameshaifanya Simba kuwa bora, lakini wao hawajawahi kuifanya kuwa hivyo tangu walipoteuliwa na wengine kuchaguliwa.

Hii inaonyesha kuwa wajumbe hawa wana maslahi binafsi na si kingine. Huwezi kung'ang'ania sehemu ambayo unasema fulani anafaidika na siyo wewe. 

Mimi nawashauri kama kweli wapo hapo kwa maslahi wa Simba na si yao wajiuzulu kama walivyofanya wengine, kina Rashid Shangazi, Raphael Chageni, Hamza Johari, na Zulfikar Chandoo ambao wamekuwa wazalendo na kuweka mbele maslahi ya klabu.

Vinginevyo waitishe Mkutano Mkuu wa dharura ili wakawekane sawa mbele ya wanachama wote badala ya kutafuta kichaka cha kujifichia.