Wachezaji tumieni mapumziko vizuri, acheni kuzidisha starehe

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:32 AM Jun 03 2024
Ligi Kuu Tanzania Bara.
Picha: TFF
Ligi Kuu Tanzania Bara.

MSIMU wa mashindano ya ndani na nje ya nchi umemalizika rasmi jana, baada ya kufanyika kwa fainali ya mashindano ya Kombe la FA.

Hii ni baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara Jumanne iliyopita, ambapo baada ya hapo wachezaji wa timu nyingine, isipokuwa Yanga na Azam FC, ambao jana walicheza fainali, walirejea  majumbani kwao kwa ajili ya kupumzika na kujiandaa kwa msimu mpya wa mashindano.

Wachezaji hao wanatoka katika mikoa mbalimbali hapa nchini huku wale wanaotoka nje ya nchi, pia kila mmoja anarejea kwao kuungana na familia zao baada ya kumaliza majukumu.

Ni kipindi ambacho wachezaji wanakwenda kupumzisha miili na akili baada ya mikiki ya msimu mzima, ya uwanjani, pamoja na kusafiri huku na huko kwa kutumia ndege au magari. Kusema kweli inachosha sana kwa sababu hata msafiri tu wa kawaida ambaye hachezi mpira, akishafika anakuwa na uchovu  unaochukua siku nzima kurejea katika hali ya kawaida.

Sasa pata picha kwa mchezaji ambaye amesafiri kwa umbali mrefu, anatakiwa kesho yake acheze soka, halafu asafiri tena akacheze katika mkoa mwingine siku chache tu baadaye.

Niwape pongezi wachezaji wote walioshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kazi kubwa ambayo wameifanya, licha ya hiyo ni kazi yao, lakini wanaifanya katika mazingira magumu, ikizingatia miundombinu ya nchi yetu kuanzia usafiri na hata baadhi ya viwanja kutokuwa rafiki kama wenzetu huko Ulaya.

Ushauri wangu ni baada ya kazi kubwa walioifanya, ikiwamo kutoa burudani kwa mashabiki, wanapaswa wapumzike kweli katika kipindi hiki.

Nikisema wapumzike kweli inamaanisha nyota hao wanatakiwa kutumia muda zaidi wakiwa na familia zao ambazo waliziacha peke yao kwa muda mrefu.

Haikatazwi kujiliwaza na kufanya starehe, au burudani, kwani hata wachezaji huko nje tunawaona 'wakila bata' baada ya msimu kumalizika, lakini wasijisahau sana wakafanya hivyo kupitiliza.

Kuna wachezaji kipindi hiki sasa ndiyo wanapata nafasi ya kushinda baa, kuzurura huko na huko na kufanya mambo mengi ambayo badala ya kupumzisha, wanauchosha mwili.

Wenzao wa Ulaya wanafanya hivyo kwa kiasi tu, lakini baada ya hapo wanafanya mazoezi madogo madogo, na kupumzika, ili kuurudisha mwili kwenye nguvu tayari kwa ajili ya kurejea kuanza msimu mpya.

Starehe za kupitiliza hufanya wachezaji wanaporejea kuwa na vitambi au uzito mkubwa, hivyo kuwafanya makocha wawe na kazi kubwa ya 'kuwakamua' kwa mazoezi makali.

Vile vile starehe za kizembe, hufanya mwili kuwa dhaifu, na kuathiri hata kiwango cha mchezaji husika mwanzoni mwa msimu. 

Licha ya kupumzika, kuburudika au kwenda kwenye matembezi kama mbuga za wanyama, na sehemu mbalimbali za vivutio kwa ajili ya kupumzisha akili, wachezaji wanatakiwa kujua kuwa soka ni ajira yao, hivyo angalau wiki moja kabla ya kuanza 'pre season', wanatakiwa kujiweka fiti, ili wanaporejea wawe katika 'shepu' nzuri ya kimichezo, ambayo haitowafanya kuanza vibaya mechi za mwanzo.

Tumeona huko nyuma baadhi ya wachezaji wakianza vibaya mechi za mwanzo, hadi baada ya michezo kadhaa ndipo wakarejea katika viwango vyao kutokana na kushindwa kujitunza wakati huu wa mapumziko.

Huu si utamaduni mzuri, wachezaji wanatakiwa kufuata maadili ya soka kwa ajili ya kufanya wajibu katika klabu zao ambazo zinawalipa fedha nyingi, lakini pia mustakabali wa maisha yao ya soka, kwa sababu huenda wakafanya kazi hiyo katika muda mfupi.