Uhakiki umiliki wa timu Ligi Kuu nchini uzingatie weledi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:23 AM Jun 22 2024
Ligi Kuu Tanzania Bara
Picha: Mtandao
Ligi Kuu Tanzania Bara

NI kweli kabisa zipo taarifa katika Ligi Kuu Tanzania Bara zipo taasisi zinazomiliki zaidi ya klabu moja kwa namna moja ama nyingine.

Ingawa siyo dhahiri, lakini dalili, tetesi, malalamiko, manung'uniko na hata ukiunganisha 'doti' utagundua kuna kitu kama hicho, hasa kwa misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Awali ilikuwapo tena dhahiri, lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lilisimama kidete na kumaliza kitu hicho.

Hata hivyo, yale ambayo yaliyokataliwa na TFF wakati huo kwa kupewa mwongozo na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), yamerejea tena.

Zamani kulikuwa na timu za majeshi zaidi ya moja katika ligi hiyo ya juu nchini, lakini ukaja mwongozo ambao ulitaka kila taasisi iwe na moja tu.

Kulikuwa na Polisi Morogoro na Polisi Dodoma zinazomilikiwa na Jeshi la Polisi Tanzania chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani,  ambazo zote kuna wakati zilikuwa zinashiriki Ligi Kuu.

 Kulikuwa na JKT Ruvu, Mgambo Shooting na Ruvu Shooting ambazo zote zilikuwa zinamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Athari ya timu hizi ni endapo kama klabu moja inahitaji pointi tatu ili iwe bingwa, au isishuke daraja, halafu moja kati ya mechi yake inacheza dhidi ya 'wanandugu', haiwezi kuzikosa.

Haiwezekani Ruvu Shooting ikose pointi tatu kutoka kwa JKT Ruvu kama inazihitaji ili isishuke wakati zote zinamilikiwa na taasisi moja, na mwajiri wao ni huyo huyo kasoro mikoa tu ndiyo tofauti.

Uongozi wa Rais, Leodegar Tenga, uliondoa kadhia hiyo, na ndiyo maana unaona leo kuna timu moja tu ya Jeshi la Polisi inaitwa, Polisi Tanzania, na Jeshi la Kujenga Taifa ikabaki na JKT Tanzania tu. Jeshi la Magereza wao waliliona hilo tangu zamani, wakawa na timu yao moja iliyobeba sura ya kitaifa, Prisons.

Naona kama sasa tunarudi nyuma. Kuna ujanja unafanyika, baadhi ya watu wanamiliki zaidi ya timu moja 'kiujanja ujanja' ambapo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almasi Kasongo, amesema ni ngumu kuwabaini, lakini watalishughulikia.

"Hili la ndani ya ligi kuna mtu anamiliki zaidi ya klabu moja, tabu tunayoipata ukienda kwenye hati ya umiliki huioni, na huwezi kumpata na sisi tunafanya kazi kwa nyaraka siyo hisia, kisheria wanakushinda, lakini hili limezua mjadala mkubwa, sasa kuthibitisha ndiyo changamoto, lakini siyo wenzetu wa Idara ya Sheria wameiacha iendelee, hapana, bado wanatafuta namna ya kupambana nalo, ikiwamo kufuatiliwa mwenendo wao wa kifedha ya klabu husika na wataalam wa kazi hizo, pamoja na chochote ambacho wataona kinaweza kuwawezesha kutambua mtu mmoja anajihusisha na klabu mbili katika ligi moja," alisema Kasongo.

Nadhani pia wangeenda mbali zaidi hata baadhi ya makampuni ambayo yamewekeza katika klabu moja, halafu yanakwenda kudhamini timu zingine, hii si sawa hata kidogo.

Ulaya wamekataza vitu kama hivi, kampuni kama ina maslahi na klabu moja, hawezi kumiliki, au kudhamini nyingine kwenye ligi  hiyo hiyo kuwepa upangaji wa matokeo. Kama hata wenzetu wanaogopa suala hilo na wanajua kuna uawezekano wa kuwepo, sisi ni nani tusiwe na tahadhari?

Naipongeza Bodi ya Ligi kwa kuamua kuvalia njuga masuala hayo, ambayo yanaweza kuifanya ligi yetu isiaminike mbele ya mashabiki na jamii ya wapenda soka kwa ujumla.

Napongeza pia ahadi ya Bodi ya Ligi kuahidi kuweka kanuni ya kuzuia timu kuhamahama mikoa kwa msimu mmoja wakati ligi inaendelea.

Hili tumeliona kwa Singida Fountain Gate, iliyohama kutoka mkoani Singida na kuhamia jijini Mwanza, huku Ihefu ikitoka  Mbarali, Mbeya kutumia Uwanja wa CCM Liti ulioko Singida.

Tunahitaji Ligi Bora isiyo na mikanganyiko na maswali tele kwa wadau ambayo yataifanya isiaminike.