NHC ijihadhari na madalali katika mradi wa jengo lake

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:37 AM May 30 2024

Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Picha: NHC
Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

PALE maeneo ya Kinondoni Morocco, Dar es Salaam, mkono wa kushoto ukitokea Mwenge na kulia kama ukitokea mjini, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limejenga majengo manne, likiwamo la makazi, eneo kubwa la mita 110,000 za mraba.

Shirika hilo limesema, makazi hayo yana kiwanja cha ndege juu ya jengo, katika mradi iliyouita Morocco Square, ambalo jiwe lake la msingi liliwekwa miaka tisa iliyopita na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ujenzi ukitarajiwa kugharimu Sh. bilioni 150.

 Mwishoni mwa wiki, shiriki hilo limetangaza kuita wafanyabiashara na watu wote wanaotaka kuwekeza kwenye jengo hilo, wazawa na wageni, wito  uliotolewa na Kaimu Meneja Mauzo na Masoko wa NHC, Emmanuel Lyimo, akishuhudia mwekezaji wa kwanza katika mradi huo. 

"Mpaka sasa tunajivunia tumempata mwekezaji wa hoteli kwenye jengo hili, vile vile tumeuza karibuni asilimia 75 ya nyumba za makazi, upande wa maduka tumekwishapangisha asilimia 100.

“Ofisi pia tumeuza na kupangisha, zimebaki nafasi chache tu, tunatoa wito kwa Watanzania na wawekezaji wote kutumia fursa hii hii, kuchangamkia sehemu zilizobakia," alisema Lyimo.

Pia, akasema NHC imefungua milango ya miradi ya wawekezaji  ya ubia. Kwa hili kwanza, nilipongeze shirika hilo kwa kuendelea kujipambanua kuwa ni moja kati ya mashirika machache yaliyosalia nchini kwenye uwezo mkubwa wa kupambana na mazingira na wakati.

 Wakati mashirika mengi ya umma yakiwa yamekufa, hilo bado ‘linadunda’,  ambapo nakumbuka wakati huo lilikuwa likijenga nyumba za kota, zilizoitwa 'nyumba za national', ambazo mpaka sasa zinaonekana kwa uchache maeneo ya Tandika, Temeke, Keko, Magomeni, Kinondoni na Mwananyamala, mpaka sasa imeendelea mpaka kujenga maghorofa.

Kitu ambacho kimenisukuma kuandika hili, ni tabia ya kuwapo baadhi ya watu wenye tabia ya udalali kwenye kuwekeza katika nyumba hizo. 

Inatajwa kuwa, kuna watu wanapangisha kwenye nyumba au vyumba kwa mikataba na shirika hilo, lakini baadaye nao wanatafuta watu wengine na kuwapangishwa kwa bei ya juu. 

Hili huwezi kulielezea kwa lugha nyingine zaidi au udalali, ambapo mtu ananunua kitu kwa bei husika au elekezi, lakini na yeye anatafuta mteja na anauza kwa bei ya juu zaidi ya hiyo.

 Vitendo hivi vimetajwa kuwapo hata katika masoko makubwa, ambapo watu wanakodi vizimba, halafu nao wanatafuta wateja kwa kuwakodisha kwa bei kubwa zaidi ya ile.

 Hawa watu wanafanya biashara ndani ya biashara, kwa sababu NHC inaweza kuandikishiana na mtu kwa kiasi fulani cha pesa, na yeye anampangisha mwingine kwa bei ya juu, hivyo anapopata kiasi cha pesa kwa mteja wake, anachofanya ni kuilipa NHC kiasi chao, kinachobaki ni cha kwake. 

Hii haileti taswira nzuri, kwani inaonekana kama vile gharama za uwekezaji au upangishaji kwa shirika hilo ni kubwa mno na hauzingatii maisha halisi ya Mtanzania, kumbe kuna watu wanapiga 'cha juu.'

Wito wangu wa NHC, kupitia kwa Kaimu Meneja Mauzo na Masoko huyo na mabosi wengine kuangalia namna ya kudhibiti hali hiyo.

Nadhani wao ni wataalamu zaidi, wanaweza kuangalia namna ya kuhakikisha wanaopanga kwenye mradi huo kwenye maeneo ya biashara, ofisi au makazi, kuhakikisha ndiyo hao hao wanaozitumia na hakuna mpangaji mwingine juu ya mpangaji.

 Inawezekana ni kufanya ukaguzi kwa wapangaji wao, au chochote kile ambacho wanaweza kubaini kuna tabia kama hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa huwaogopesha Watanzania wengi kukataa kuwekeza kwenye miradi ya majengo ya NHC wakihofia ughali wa kodi wakati kiuhalisia sivyo ilivyo.