Mbona hatujishirikishi tunabaki kulalamika

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 11:51 AM Jun 04 2024
Madawati.
Picha: Mtandaoni
Madawati.

KUMEKUWA na malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi kuhusu uhaba wa miundombinu mfano madawati katika shule za umma za msingi na sekondari, unaolazimisha wanafunzi wengi kukaa chini.

Malalamiko hayo na mengine sugu yamekuwa yakitolewa dhidi ya serikali, huku wengi wao wakiishutumu kushindwa kuyatatua kwa madai ya ukosefu wa fedha. Upungufu huo ni sehemu ya vyanzo vya kushusha na kuzidi kuporomoka kiwango cha elimu kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya kitaifa.

Yote hayo yakitokana na mazingira ya kujifunza na kufundisha kuwa duni. Aidha, kuna wazazi na walezi ambao pia wamekuwa wakipinga kuchangia chakula kwa wanafunzi shuleni wakidai kazi hiyo inapaswa kufanywa na serikali.

 Ili kukabiliana na hilo la wanafunzi kupata chakula cha mchana kumezilazimu shule nyingi kupitika vikao vya kamati zinazoundwa na wazazi na walezi wa wanafunzi kukubaliana kuchangia kiasi cha fedha au chakula kwa kila mwanafunzi ili apate mlo wa mchana na kuendelea na masomo. 

Hata hivyo wapo ambao wanalalamika kuwa kiasi wanachotoa kila siku kwa kila mwanafunzi kugharamia chakula cha mchana hakilingani na chakula watoto wao wanachopata. Wanalalamika kuwa kiasi hicho wanachoingia kwa siku kinapaswa kuwapa mlo unaolingana na fedha waliyotoa wakitoa mfano wa kulishwa makande na ubwabwa kwa maharage.  

Kuna shule ambazo zimeweka utaratibu wa kuzuia mwanafunzi kuingia kwenye eneo la shule kwa kuweka mlinzi getini anapokosa fedha iliyopangwa na kamati hizo. Ikumbukwe akizuiliwa hukosa masomo, hali ambayo inachangia pia kukithiri kwa utoro kwa wanafunzi kwa kisingizio hicho.   

Ikumbukwe serikali inatatua changamoto nyingi kwa shule zake ikiwa ni pamoja na uhaba wa madarasa, shule   kulingana na idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi, sekondari na hata ya kidato cha tano na sita ambao wamekuwa wakiongezeka kila mwaka.

Vilevile, imekuwa na jukumu la kuhakikisha inaajiri walimu wa kutosha kuwapa elimu bora wanafunzi ili kupata wataalamu wa leo na kesho wakiwamo madaktari, wanahabari, walimu na wahandisi. Tunapaswa kufahamu ya kwamba, serikali ili kufanikisha mipango hiyo na mingine katika sekta  zake nyingine imekuwa ikitumia fedha nyingi.

Mfano imekuwa ikijenga miundombinu mbalimbali ikiwamo ya maji, barabara, umeme, simu na viwanja vya ndege kwa kutumia fedha ambazo imekuwa ikikusanya kodi kutoka kwa wananchi. Pia zipo za misaada ya wafadhili na mikopo kutoka kwa benki na taasisi za fedha ambazo baadaye inatakiwa kuzirejesha kwa makubaliano ya vipindi maalumu.

Sisi wazazi na walezi tunapaswa kuelewa kwamba ni jukumu letu kusaidiana na serikali kwa kutatua baadhi ya changamoto ikiwamo kukabiliana na uhaba wa madawati kwa kukubali kuchangia kiasi cha fedha kwa ajili ya kufanya matengenezo. Tukae katika kamati zetu za shule kwa ajili ya kupanga jinsi ya kushirikiana kutatua changamoto hizo na nyingine kwa ajili ya ustawi wa elimu bora kwa watoto wetu huku serikali nayo ikipambana kukabiliana na changamoto nzito zinazohitaji mabilioni ya serikali.

Kwani mzazi na mlezi anapokwepa kushiriki kutatua changamoto zinazozikabili shule wanazosoma watoto wao ni sawa na kumfanyia mwanawe vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa mfano kukaa chini kwa kukosa madawati na chakula cha mchana.

 Lah sivyo kama mzazi au mlezi anaona kulipia chakula gharama basi aombe kibali cha kumpelekea mtoto wake chakula shuleni wakati wa mchana ili aweze kupata uelewa anapokuwa anafundishwa darasani. Ikumbukwe kwamba kumkalisha mwanafunzi chini kunampunguzia uelewa anapofundishwa kutokana na mazingira anayokumbana nayo kuwa magumu. 

 Ingawa Waswahili wanasema shibe na mwana malevya endapo mwanafunzi atakula hadi kuvimbiwa kama ambavyo baadhi ya wazazi wanavyo taka, vivyo hivyo japo  njaa ni mwana malegeza, madhara yake huchangia mwanafunzi kukosa usikivu darasani, hivyo kidogo atakachopata tumboni, kitahamsha ufahamu wake kichwani.