Ligi Kuu Bara 2023/2024 ilikuwa na mastraika butu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:09 AM Jun 01 2024
Stephane Aziz Ki.
Picha: Mtandaoni
Stephane Aziz Ki.

WAUNGWANA lazima tulonge, Ligi Kuu 2023/2024 ilikuwa na mastraika butu, haijawahi kutokea huko nyuma.

Ni msimu tulioshuhudia wachezaji wa nafasi ya viungo washambuliaji wakichuana wenyewe kwa wenyewe kuwania ufungaji bora.

Kwa straika wa timu yoyote ile ni lazima awe anajifikiria mara mbili mbili kama anaitendea haki nafasi yake.

Viungo washambuliaji, Stephane Aziz Ki wa Yanga, na mwenzake Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC ndiyo walioonekana kufukuzana kufunga mabao, na walikuwa wanafunga kweli kweli, ambapo wale wasiojua nafasi katika mpira wa miguu, wangedhani ni mastraika.

Aziz Ki ndiye kinara aliyemaliza na mabao 21, Fei Toto akawa na pili akipachika magoli 19.

Wakati wakipigania kiatu cha dhahabu na kuifanya vita kuwa kali, hakukuonekana juhudi zozote za washambuliaji kufurukuta, zaidi ya mmoja tu kwa mbali, ambaye ni Waziri Junior wa KMC.

Huyu amemaliza ligi akiwa amefunga mabao 12, na kushika nafasi ya tatu na kuonyesha angalau alikuwa anajisukuma, ingawa hakuwa mshindani halisi.

Matokeo yake pambano liliisha kama wengi walivyotegemea, mshindi wa kwanza na wa pili katika ufungaji bora Ligi Kuu msimu huu, wote ni viungo washambuliaji.

Achana na hilo, walioshika nafasi ya nne pia ni viungo washambuliaji, Saido Ntibazonkiza wa Simba na Maxi Nzengeli wa Yanga ambao kila mmoja amepachika mabao 11.

Twende kwa walioshika nafasi ya tano, ni winga na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Junior, kiungo Marouf Tchakei wa Ihefu, pamoja na kiungo mkabaji wa Yanga, Mudathir Yahya, ambao wote wamefunga mabao tisa kila mmoja.

Hadi nafasi yupo kiungo ambaye ni Gibril Sillah wa Azam FC, akifunga na straika Samson Mpangula wa Prisons, wote wakifunga mabao manane.

Hapa utaona kutoka nafasi ya kwanza hadi ya sita ambapo kuna wafungaji 10 bora, mastraika ni wawili tu, Waziri na Mbangula, ila kwa bahati nzuri wote ni Watanzania.

Ukiangalia takwimu hizo zinakuonyesha  hata timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam FC, hazikuwa na mastrika bora msimu huu. Walizidiwa hata na KMC na Prisons.

Msimu uliopita straika, Fiston Mayele wa Yanga alifungana na kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido.

Huko nyuma zaidi tuliona mastraika kama kina Meddie Kagere, John Bocco, Amissi Tambwe wakitamba kwenye ufungaji bora, lakini kwa sasa inaonekana kinyume chake.

Sisemi viungo washambuliaji wasifunge mabao, au ni dhambi, lakini nimeandika hili kuwashtua mastraika wanaocheza Ligi Kuu waamke, pia viongozi wa klabu wangalie sasa ni jinsi gani na kusaka washambuliaji wenye ubora wa hali ya juu kama kina Kagere, Tambwe, Mayele na wengine wanaofanana na hao.

Katika soka, kazi ya kwanza ya kiungo mshambuliaji ni kutoa pasi za mwisho kwa mastraika, 'asisti' ya pili ni kufunga, na kazi namba moja ya straika ni kufunga mabao tu.

Matokeo yake tunaona sasa viungo washambuliaji wanafanya kazi namba mbili, ambayo ilitakiwa kufanywa na mastraika.

Sina uhakika, lakini inawezekana kabisa viungo washambuliaji hao waliwatengenezea sana mastraika wakashindwa kufunga, na ingewezekana wangekuwa na mabao mengi kuliko hayo ambayo wenzao wanayo.

Kwa hili kuna cha kujifunza kuelekea msimu ujao, kwani mastraika wote wa Kibongo na kigeni wamefeli.

Kuna haja ya viongozi wa klabu wanaosajili kuangalia mastraika wapya vijana kutoka klabu mbalimbali na kuacha kuwatumia wale wale wa miaka 'nenda rudi' wanaomaliza wakiwa na mabao matano au sita ambayo yanaweza kufungwa na mabeki tu.

Wanaosajili mastraika kutoka nje ya nchi watafute wale ambao wako kwenye viwango vya juu kwa wakati huo, na si kusajili kutokana na historia yao ya nyuma. au wale ambao wamemaliza mikataba kwenye klabu zao na hawawahitaji tena.