Kanuni za 'play off', ushirikina Ligi Kuu hazifai, zibadilishwe

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:19 AM Jun 08 2024
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi hiyo, Karim Boimanda.
Picha: Maktaba
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi hiyo, Karim Boimanda.

TAYARI Bodi ya Ligi Kuu imeanza kupokea maoni kwa ajili ya maboresho ya kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi hiyo, Karim Boimanda, akasema tayari wameshaanza kupokea maoni kwa njia mbalimbali za mawasiliano, huku akiahidi kuwatembelea pia wadau wa soka, vikiwemo vyombo vya habari kwa ajili ya kupata mawazo mengi zaidi yatakayofanya kuwe na kanuni bora msimu ujao.

 Hata hivyo, alikiri kuwa eneo la imani za kishirikina ndilo lililoonekana kuvutia wadau wengi kutoa maoni yao kuliko kanuni zingine.
 "Tumeanza kupokea maoni, lakini ukweli kabisa nikiri kanuni iliyovunjwa sana msimu huu ni ile inayozungumzia imani za kishirikina, na ndiyo inayotolewa maoni mengi kwa sasa na wadau kuliko zingine kuonyesha ni namna gani hawaridhishwi na adhabu zinazotolewa, wanasema haizuii au haiwatishi watu kuendelea na tabia hiyo," alisema Boimanda.

 Binafsi, kwanza niwapongeze Bodi ya Ligi kwa kuwa na wazo la kuwatembelea wadau walipo, wakiwemo wanahabari kwa ajili ya kupata maoni mengi na kwa karibu zaidi huku akishuhudia hisia za wadau wenyewe.

 Kabla hata hawajatembelea vyombo vya habari, binafasi naanza kabisa kutoa maoni yangu kama mmoja wa wadau wa soka nchini.

 Kwanza kabisa ni kuhusu kanuni ya ushirikina, ni kosa ambalo limekuwa likijirudia kama ambavyo bodi yenyewe ilivyobainisha. Hata mimi siridhishwi na adhabu za faini zinazotolewa, ambazo klabu hazishtuki, badala yake zinarudia mechi baada ya mechi huku taarifa zikisema hata hizo faini zenyewe hukatwa kwenye viingilio vya mechi.

 Kwangu  ningependa iwekwe kanuni ya kuzikata pointi mbili timu zinazothibitika kufanya kosa hilo.
 Pointi mbili tu, zinatosha kuitoa timu kwenye reli na isirudie tena mchezo huo, na ikiwezekana iwe pointi na faini juu ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo vya aibu kwenye soka letu. 

 Ila angalizo ni kwamba timu isikatwe kama vitendo hivyo vinafanywa na mashabiki, kwa sababu timu zinaweza kuhujumiana. 

Mashabiki wa timu pinzani wanaweza kwenda katika mechi ya wenzao na kuvaa jezi za wapinzani wao na kuonyesha vitendo hivyo ili tu kuiponza timu husika.

Adhabu itolewe kwa makosa ya viongozi, wachezaji na watu ambao wanajulikana kuwa wapo ndani ya klabu husika.
 Ukakasi mwingine ni kuhusu mechi za mchujo. 

Ki ukweli mechi hizi zimekuwa nyingi sana kiasi cha kuwachanganya hata mashabiki na hazitendi haki kwa timu za madaraja ya chini.
 Mimi sikatai 'play off', lakini iwe moja tu, yaani timu mbili za chini katika Ligi Kuu, zitakazoshika nafasi ya 16 na 15 zishuke moja kwa moja, itakayoshika nafasi ya 14 iende moja kwa moja kucheza na timu itakayomaliza nafasi ya tatu Ligi ya Championship, baada ya zile mbili za juu kupanda.

 Kuwa na 'play off' nne, yaani wa Ligi Kuu wenyewe, Champioship nao wawe na mechi yao alafu washindi waje kukutana ni mlolongo mrefu. Bodi ya Ligi tunaomba ifanyie kazi ushauri huu kwa uboreshaji wa Ligi yetu.