Hongera Wizara ya Afya kufanya uamuzi huu wa tumbaku, lakini...

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:39 PM May 31 2024
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel.
Picha: Maktaba
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel.

WIZARA ya Afya imesema tayari bunge limepitisha Sheria ya Udhibiti wa Tumbaku ijulikanayo kama ‘The Tobacco Products Regulation Act, 2003’, inayotoa katazo la uvutaji sigara hadharani.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel alibainisha hayo hivi karibuni jijini Dodoma wakati akijibu swali kutoka kwa mbunge aliyeuliza ni lini serikali italeta sheria ya kuzuia uvutaji wa sigara na mazao mengine hadharani.
 
 Naibu Waziri huyo akasema, sheria hiyo imezuia matangazo ya tumbaku na bidhaa nyingine na tumbaku katika maeneo ya umma, ikiwamo vyombo vya habari, mbao za matangazo na kwenye matamasha.
 
 Vilevile, Dk. Mollel anatoa wito kwa wabunge kuwa mabalozi wa udhibiti wa tumbaku katika jamii kwenye maeneo yao, ili kusaidia wananchi kuepuka magonjwa yasiyo yakuambukiza.
 
 Pamoja na uamuzi huo wa wizara, ninadhani ipo haja ya kuchukua hatua zaidi kwa ajili ya kuokoa maisha ya Watanzania ambao si watumiaji wa tumbaku au bidhaa nyingine inayotokana na tumbaku.
 
 Hatua ambazo zinafaa kuchukuliwa ni kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu madhara ya tumbaku kupitia kwa wataalam wa afya ili waweze kujibu kitaalam hoja za wavutaji.
 
 Imekuwa ni jambo la kawaida kukuta wavutaji wakivuta sigara katika mkusanyiko wa watu hasa kwenye vituo vya daladala au mtu amebeba mtoto huku akivuta dani ya usafiri wa binafsi huku akiwa na watoto.
 
 Kwa hali hiyo, ni wazi wapo wengi ambao hawajui madhara ya kuvuta tumbaku, kwani wengine huwa wanahoji kwamba kama ina madhara kwa nini inalimwa au kwa nini kuna viwanda vya kutengeneza sigara?
 
 Hivyo, ninadhani ipo haja kwa wizara yenye dhamana ya afya za Watanzania kujipanga zaidi, kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma wajue madhara ya uvutaji kisha waamue kuacha au kuendelea kuvuta.
 
 Uelimishaji unaweza kuwa kwa njia ya mihadhara, kuunda klabu za kujadili madhara ya bidhaa za tumbaku shuleni, ndani ya jamii kwa njia ya vyombo vya habari na uandaaji na usambazaji wa vipeperushi na nyaraka mbalimbali za uelimishaji.
 
 Mbali na hilo, uelimishaji unaweza kuwa wa kupitia mitandao ya kijamii, ushiriki na uelimishaji kwenye siku ya kuzuia matumizi ya tumbaku duniani, kama ambavyo itaadhimishwa siku chache zijazo.
 
 Vilevile wadau wanaweza kushiriki na kutoa elimu katika maonyesho mbalimbali, elimu kupitia picha zinazoonyesha madhara ya kiafya, michoro na vibonzo lengo likiwa ni kuokoa Watanzania.
 
 Wakati huu wa kuelekea katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku,ni vyema suala la elimu kuhusu madhara ya tumbaku likapewa mkazo ili kunusuru afya za Watanzania.
 
 Mei 31 ya kila mwaka, huwa ni maadhimisho ya siku hiyo ambayo mwaka jana ilielezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Tedros Ghebreyesus kwamba tumbaku inasababisha vifo milioni nane kila mwaka duniani.
 
 Aidha, anasema, zaidi ya ekari milioni 300 katika nchi zaidi ya 120 duniani zinatumika kwa ajili ya kilimo cha tumbaku hata kwenye nchi ambazo watu wake wana njaa kali.
 
 Kwa kuwa lengo la maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Matumizi ya Tumbaku Duniani, ni vyema jamii ikaelimisha hatari za matumizi ya tumbaku, ili kupunguza vifo vinavyotokana na matumizi ya tumbaku.