Dharau kwenye zebra zinatuchosha

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 10:17 AM Jun 11 2024
Alama ya barabarani (zebra).
Picha: Mtandao
Alama ya barabarani (zebra).

KUNA mazoea ambayo sasa yamekithiri kwa madereva wengi kutokuheshimu alama za pundamilia ambazo ni vivuko vya wanaotembea na kusababisha ajali.

Kutoheshimu vivuko kwenye barabara kubwa na ndogo kumesababisha vifo na majeraha pia uharibifu wa mali. Wanaoathirika zaidi ni watoto, wanaoishi na ulemavu, wazee, wanaotumia vileo na hata wagonjwa.

Madereva wengi kuanzia wa bodaboda hadi malori kwenye miji mikubwa na midogo wanapokuwa barabarani hawaheshimu mistari ya pundamilia au zebra na kusababisha ajali, tena nyingine wakati mwingine zikizotokea jirani na kivuko.

Wanaoumia wanaingia kwenye hatari kwani wanaamini kuwa sehemu hiyo ni salama kutumiwa lakini sivyo, iwapo gari ndogo au basi la abiria linasimama, bodaboda huchomoka na kusababisha ajali. Tunajiuliza hivi bodaboda hawana ufahamu kuhusu kuheshimu vivuko hivyo?

 Licha ya elimu ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara, kuhusu zebra kuna usumbufu kila wakati.

Kisheria zebra zinapaswa kuheshimiwa na watumiaji wote kuanzia madereva pamoja na wanaotembea kwa kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa ili kuimarisha usalama  pande zote.

Kwa upande mwingine, wanaotembea wanashauriwa kusimama na kuhakikisha kuwa magari yote yamesimama kabla ya kuingia kwenye kivuko cha pundamilia.

Sheria ya usalama barabarani inasema ni lazima dereva kuzingatia kuwa anapaswa kusimama mahali popote ambapo alama hiyo itakuwa imewekwa. 

Pia kila anayetumia kivuko cha wanaotembea anatakiwa kuwa na tahadhari kubwa na pia akiangalia ‘spidi’ ahakikishe anatumia kivuko kuvuka barabara na si kwa mambo mengine.

Ni lazima madereva wajifunze kuwa itakapotokea anayetembea anatumia au anataka kukitumia, dereva wa gari atasimama kabla ya kivuko hicho ambacho hakiongozwi na taa za barabarani, ishara au askari.

Dereva akiwa amejiridhisha kuwa hakuna mtembea kwa miguu anayevuka au anayekusudia kuvuka barabara hiyo, inamsaidia kuepuka makosa kwani hakuna yeyote aliyekusudia kuvuka kwa wakati huo, hivyo anaweza kutembea kivukoni.

 Halazimiki kusimama kila wakati ila, kama amejihakikishia kuwa hakuna anayevuka, dereva anatakiwa kupunguza mwendo na kuangalia na baada ya hapo ataendelea na safari.

Kwa hiyo dereva atasimama kwenye eneo kabla ya zebra pale wakati wote ambao atawaona waenda kwa miguu, wakiwa wanatembea pembezoni mwa kivuko na wakati mwingine wakiwa wanavuka kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili wa barabara.

Kufanya hivyo ni lazima kwani baadhi ya madereva hawajali, hawazingatii sheria na kanuni za kiusalama kwao au kwa watu wengine na kusababisha kuongezeka ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani ya mwaka 2002 sura ya 168 kifungu cha. 73(2) watumiaji wote wa barabara wanatakiwa kuheshimu na kufuata ishara zilizowekwa barabarani, ili kuepusha ajali zinazotokea kwa uzembe.

Kuna mambo muhimu ya kuzingatia unapokuwa katika eneo la zebra, kabla ya kuendelea na safari au kuvuka kutoka upande mmoja kwenda wa upande wa pili wa barabara ikiwa ni pamoja na kupunguza mwendo unapoikaribia zebra usiingie na kuizuia ili wanaovuka waione.

Lengo ni ili angalau uwe katika mwendo wa uwezekano wa kusimama, ikiwa kuna mtu atakuwa anavuka barabara au kutaka kuvuka barabara.

Sheria inawaelekeza madereva kuwa iwapo kuna mtu anasubiri kuvuka kwenye zebra, wasimame kumpisha avuke, wasimame kwanza ili avuke au aanze kuvuka, pia kama watamkuta katikati au anamalizia kuvuka waacha amalize kuvuka.

Vile vile wasimpigie honi aliyesimama kupisha watu kuvuka kwenye kivuko, kadhalika wanaonywa wasimpite au kuovateki aliyesimama kupisha wanaovuka kwani kumpita kunaweza kusababisha ajali.

Aidha, amwashirie dereva mwenzie kusimama, iwapo anahisi amempuuza na anataka ‘kuovateki’ akiwa amepisha waotembea.

Madereva wa bajaji, malori, mabasi ya mikoani na daladala wafuate sheria na kanuni zilizowekwa,  kupunguza na kutokomeza ajali ambazo hutokea kwenye kivuko  au zebra, ambazo husababishwa na kutojali kunakofanywa na  baadhi ya madereva wanaopuuza sheria.