COREFA yajipanga kukuza vipaji vya soka Pwani

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:51 PM Jan 06 2025
Mwenyekiti wa COREFA Mkoa wa Pwani, Robert Munis.
Picha: Julieth Mkireri
Mwenyekiti wa COREFA Mkoa wa Pwani, Robert Munis.

Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) kimeweka wazi mikakati kabambe ya kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kituo cha kuandaa vijana, lengo likiwa ni kuzalisha wachezaji bora watakaoliwakilisha mkoa huo kwa mafanikio makubwa.

Mwenyekiti wa COREFA Mkoa wa Pwani, Robert Munis, amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Munis amesema kwa sasa kuna vituo vinne vya kuendeleza vipaji vya soka, lakini lengo ni kuongeza vituo hivyo hadi saba na hatimaye kufikia tisa, ili kuhakikisha kila Halmashauri katika mkoa huo ina kituo chake.

Munis amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wazazi katika kufanikisha azma hiyo. “Tunawahamasisha wazazi kuhakikisha watoto wao wanashiriki kwenye soka. Mpira ni ajira, lakini ili kufikia mafanikio haya lazima wazazi wawasaidie watoto kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kucheza na kuepuka kuwakataza kushiriki,” amesema Munis.

Mwenyekiti huyo alitaja baadhi ya viwanja vilivyopo ndani ya Mkoa wa Pwani kuwa ni Mwanambaya, Bungu, Mabatini, Tumbi, Mwanakalenge, Kiromo, Msoga, Maili Moja Mwendapole, na Kwambonde. Amesema baadhi ya viwanja hivi tayari vinatumika, huku vingine vikiwa katika hatua za ujenzi.

Makamu Mwenyekiti wa COREFA na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha, Mohamed Lacha, amewashukuru wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha upatikanaji wa ofisi ya kisasa kwa chama hicho. Lacha ameongeza kuwa juhudi kubwa zimeelekezwa kuhakikisha COREFA inaendelea kusonga mbele kwa kushirikiana kwa karibu na wadau na kuepuka migogoro ambayo mara nyingi hurudisha nyuma maendeleo ya soka.

Kwa upande wa soka la wanawake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Pwani, Asha Mbata, amesema kuwa mwaka jana wilaya zote za mkoa huo zilifanikiwa kuchezesha ligi za wanawake, isipokuwa Wilaya ya Mafia pekee. Mbata ameeleza kuwa mafanikio haya ni hatua kubwa kwa soka la wanawake na wakazi wa Mkoa wa Pwani kwa ujumla.

COREFA ina matumaini kuwa juhudi hizi zitaleta mabadiliko makubwa katika soka la mkoa huo, na hatimaye kuzalisha vipaji vya kimataifa kutoka Pwani.