Udhibiti uhalifu mitandaoni ukemewe

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 11:12 AM Jun 18 2024
Uhalifu mitandaoni.
Picha: Mtandao
Uhalifu mitandaoni.

MAPAMBANO dhidi ya uhalifu mitandaoni ni jambo muhimu hasa wakati dunia ikiwa kwenye mabadiliko ya kutumia teknolojia ya mawasiliano.

Kuna mambo mengi yanayotokea katika kipindi hiki huku wahalifu wakitafuta mbinu mbalimbali za kuhakikisha wanakwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Dunia kwenda na mabadiliko ya teknolojia ni kurahisisha kazi na kupunguza muda unaotumika kwa binadamu kuifanya kazi hiyo.

Hata hivyo, kuna watu wanaotumia fursa hiyo kujinufaisha na kuona hawaachwi nyuma kwa jambo lolote lile.

Miaka ya nyuma kabla ya teknolojia ya mawasiliano haijabadilika, kazi nyingi zilikuwa zikifanyika kwa kwenda sehemu husika, lakini sasa hivi mtu anaweza kukaa nyumbani na akamiliza kila kitu kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Siku za nyuma sehemu zenye huduma muhimu kama ulipaji wa bili za umeme, maji na benki, mtu ilibidi aende kwenye ofisi hizo hali iliyokuwa ikisababisha msongamo mkubwa wa watu.

Sasa hivi hata ukiwa nje ya nchi unaweza kufanya miamala na kulipia bili zako kwa wakati.

Kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ilikuwa inachukua muda kumtumia ndugu yake pesa, lakini kwa sasa teknolojia imerahisisha, hakuna usumbufu tena.

Lakini, teknolojia hiyo imeingiliwa na kutumika vibaya kwa baadhi ya wahalifu kwenye sekta ya fedha kwa kuwaibia watumiaji na kuwafanya waogope kuitumia.

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), imeeleza wazi kuwa inaendeleza jitihada za kupambana na kudhibiti uhalifu mitandaoni, ikiwamo huduma za kifedha kutokana na kuongezeka mifumo mipya ya mawasiliano ya teknolojia.

Inapokuja teknolojia mpya ni muhimu ikatumika vizuri ili kunufaisha watu na kuondoa ugumu uliokuwapo mwanzo.

Kwa nchini Tanzania, wafanyabiashara, wajasiriamali wamerahisishiwa kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ambapo kwa sasa wanaweza kutuma pesa nje ya nchi na kuletewa bidhaa wanazotaka badala ya kusafiri hali inayowapunguzia gharama.

Katika matumizi ya teknolojia hii pia kunahitajika uaminifu wa hali ya juu ndio maana hata TCRA ikiwa ni mdhibiti wa matumizi mabaya ya mawasiliano imekuwa ikiingilia kati kila inapoona mambo hayaendi sawa.

Kuna wanaotumia teknolojia hiyo pia kwa malengo mabaya ya kuwachafua watu wengine kwenye mitandao.

Viongozi wa juu wanapokuwa kwenye majukwaa wamekuwa wakikemea tabia hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa kama isipodhibitiwa itarudisha nyuma maendeleo.

Duniani mabadiliko ya kiteknolojia hayawezi kuepukika, hivyo ni muhimu wadhibiti wa uhalifu mitandaoni kuwa makini kudhibiti hali hiyo ili kuepuka matumizi mabaya.

Hali hiyo imekuwa ikishamiri kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuharibu hali ya hewa na wengine wanaochafuliwa huathirika kisaikolojia.

Wengine hudiriki kutengeneza picha na kufanya ionekane kama ya mhusika waliyepania kumharibia. Kwa kweli matumizi haya ya teknolojia hayatumiki kama ilivyokusudia kwa walioanzisha kuleta mabadiliko yawe ya kihabari au kiuchumi.

Uhalifu huu unapaswa kupigwa vita na kila mtu awe mlinzi wa mwenzake kwa kutokubali kusambaza picha yoyote inayodhalilisha utu wa mtu mwingine, kuharibu sifa au kufanyika kwa wizi wa aina yoyote.

Watu wote wakisaidiana na TCRA, uhalifu wa kimtandao utapungua na wengine wenye kusudio hilo wataacha kufanya hivyo.