Msako wa TBS viwanda uende zaidi ya malengo

Nipashe
Published at 07:32 AM Jun 13 2024
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limetangaza kuanza msako kwa wazalishaji wa chuma ili kuwachukulia hatua wale wanaotengeneza bidhaa zisizokidhi viwango kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, alibainisha hayo mapema wiki hii wakati wa mkutano kati ya shirika hilo na wadau katika ofisi za shirika hilo, Ubungo, Dar es Salaam. Alisema miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wamiliki wa viwanda hivyo ni kuvifungia iwapo vitabainika kutengeneza bidhaa zisizokidhi viwango kama sheria inavyotaka.

Katika taarifa yake hiyo, mkurugenzi mkuu huyo alibainisha kuwa moja ya matakwa muhimu ya viwango vya bidhaa za chuma zinazozalishwa au kuingizwa nchini ni pamoja na kuandikwa taarifa zinazoonyesha jina la mzalishaji na ukubwa wa bidhaa. Alisema taarifa hizo ni muhimu kwa wanunuzi na watumiaji wa bidhaa kwa kuwa huwezesha kutoa mrejesho kwa mzalishaji husika na kufanya ufuatiliaji endapo itabainika kuwa na kasoro yoyote.

Pia alibainisha kwamba uwapo wa taarifa muhimu kwenye bidhaa huziwezesha taasisi za udhibiti kuwa na uwezo wa kuzitambua, kuzifanyia ufuatiliaji katika soko na kuchukua hatua stahiki kwa mzalishaji atakayebainika kukiuka matakwa ya sheria, kanuni na viwango.

Pamoja na matakwa hayo ya kisheria na kanuni, alibainisha kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa bidhaa kwamba baadhi zina kasoro, hivyo kulifanya shirika hilo kufanya ufuatiliaji kuanzia maeneo zinakozalishwa. Kuwapo kwa tatizo hilo, alisema wazalishaji hao wamesababisha changamoto katika udhibiti na hasara kwa watumiaji, hivyo TBS haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya  yeyote  atakayezalisha bidhaa kinyume na matakwa ya viwango.

Hatua ya TBS ambayo kwa hakika hufanywa mara kwa mara na kubaini matatizo katika bidhaa mbalimbali, imetangazwa wakati mwafaka kwa kuwa hivi sasa kuna viwanda vingi vinavyotengeneza bidhaa za chuma. Kuna wasiwasi mkubwa kama watengenezaji wa bidhaa hizo wanafuata matakwa ya kisheria kupitia TBS kuhusu viwango na ubora unaotakiwa. 

Nia ya TBS ni nzuri katika kuhakikisha Watanzania wanatumia bidhaa zenye viwango vilivyothitishwa na taasisi hiyo ya serikali ili kumlinda mtumiaji wa mwisho ambaye ni Mtanzania wa kawaida. 

Kwa mantiki hiyo, TBS inapaswa kupewa ushirikiano kutoka taasisi za kiserikali ambazo zimepewa dhamana ya kusimamia sheria kama vile Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kubaini kama wazalishaji hao wanalipa kodi zinazotakiwa katika shughuli kama hizo. 

Pamoja na kwamba chuma ni moja ya bidhaa zinazolalamikiwa na wananchi kuhusu ubora na viwango, kuna bidhaa zingine ambazo zina madhara makubwa kwa wananchi kama vile vyakula na vinywaji kama havitadhibitiwa ipasavyo. 

Matumizi ya vinywaji kama pombe kali ambazo zimebainika kuwa nyingi hazina ubora zimekuwa zikitengenezwa na watu binafsi na viwanda bubu katika maeneo mbalimbali. Matokeo ya kuwapo kwa bidhaa hizo ambazo zinatengenezwa kinyemela ni kuwasababishia madhara makubwa watumiaji hasa wale wanaoshindwa kubaini bidhaa halali na isiyo halali. 

Kwa mantiki hiyo, ukaguzi wa bidhaa uliopangwa kufanywa na TBS unapaswa kujikita katika bidhaa zote badala ya chuma pekee ili kuwalinda watumiaji ambao ni wananchi. Ni dhahiri kwamba kwa kufanya msako wa bidhaa zote, TBS kwa kushirikiana na polisi, TRA na mamlaka za serikali za mitaa, kutaibua mambo mengi na kuwachukulia wote wanaotengeneza bidhaa zisizokidhi viwango na kuweka rehani maisha ya Watanzania.