Maandalizi kuelekea msimu mpya yazingatie uhalisia

Nipashe
Published at 07:23 AM Jun 15 2024
Ligi Kuu Bara.
Picha: TFF
Ligi Kuu Bara.

WAKATI mashindano ya Euro 2024 yakitarajiwa kufanyika kuanzia kesho, hapa nchini wachezaji wetu wanaoshiriki Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship, First League (zamani Ligi Daraja la Pili), na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania iliyomalizika jana wako katika mapumziko.

Kalenda hii ya mapumziko kwa wachezaji haijawekwa ili kujifurahisha, imeandaliwa maalumu kuipa nafasi miili na akili za wachezaji muda wa kujitengeneza upya na kujiandaa tayari na msimu mpya wa mashindano.

Wachezaji wanatakiwa kuheshimu muda wa mapumziko kwa sababu ambaye hatapumzika, atakuwa katika changamoto mbalimbali pale watakaporejea katika  maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa 2024/2025 ambao utafanyika kuanzia mapema Agosti, mwaka huu.

Kutumia mapumziko haya vibaya, si tu kutakutesa mchezaji husika wakati wa kuanza mazoezi ya msimu mpya, lakini nyota huyo anaweza kupoteza namba katika kikosi anachocheza kutokana na kuchelewa kuingia katika mfumo kwenye mechi za awali.

Kufanya starehe zaidi na mambo mengine yanayokatazwa kwa wachezaji, hili ni jambo ambalo linakumbushwa kwa kila mmoja kujichunga kwa sababu utimamu mzuri wa mwili ndio hupelekea kupata namba na kuisaidia timu yako kuanza vyema msimu husika.

Kuna baadhi ya wachezaji huachwa, hupoteza namba na wengine hulazimika kutolewa kwa mkopo katika timu nyingine na nafasi zao kuletwa wachezaji wapya kwa sababu tu hakuisaidia klabu yake kupata matokeo chanya wakati msimu mpya unaanza.

Inafahamika kuwa 'biashara asubuhi', kila timu huitaji kuvuna pointi tatu muhimu kuanzia mechi ya kwanza ili kujiweka mahali salama na kuelekea kutimiza malengo yake, na hili litatimia endapo wachezaji watajituza wakati wa mapumziko na kufanya maandalizi sahihi.

Haitakuwa vyema timu ikafanya maandalizi kwa 'kukurupuka' au kwa kufuata mkumbo kwa sababu wameona wapinzani wao wameamua kuweka kambi mahali fulani.

Umefika wakati wa kuzipa nafasi Idara za Ufundi kuamua aina ya mazoezi, mahali na michezo ya kirafiki ambayo itasaidia katika kukijenga na kukiimarisha kikosi husika na si kufanya kwa ajili ya kujionyesha.

Pia kumekuwa na utaratibu wa timu kuandaa mechi za kirafiki dhidi ya timu za ndani na nyingine kutoka nje ya Tanzania, lakini viongozi wamekuwa wakifanya uteuzi wa kualika klabu ambazo kiuhalisia haziwapi kipimo halisi kuelekea msimu mpya.

Tunazikumbusha timu ambazo zitaiwakilisha Tanzania Bara na Zanzibar katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, kucheza mechi za kirafiki zenye hadhi na timu watakazokutana nazo katika mashindano hayo ya kimataifa.

Kucheza mechi za kirafiki na timu ndogo, kiufundi unairudisha au unaichelewesha timu yako kuelekea katika mafanikio kwa sababu benchi la ufundi halitaona mapungufu yake sawa sawa na badala yake watafurahia idadi kubwa ya mabao ambayo yatafungwa kwenye michezo hiyo.

Hongera sana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kubadilisha mfumo wa kupata mshindi wa mashindano ya Ngao ya Jamii, ambapo msimu mpya tutashuhudia timu nne zilizofuzu michuano ya kimataifa kuanza kuonyesha makali yake katika mashindano hayo.

Baada ya kumaliza maandalizi ya msimu mpya, tunaamini makocha watakaokuwa na dhamana ya kuziongoza timu hiyo watatumia michuano hiyo kurekebisha makosa kabla ya kuanza kushiriki mashindano ya CAF ambayo mechi zake za awali zitafanyika kati ya Agosti 13 na 15, mwaka huu.