RAIS Samia Suluhu Hassan, hana mpinzani kwenye umaarufu. Ni kiongozi wa kwanza mwanamama kuongoza Tanzania na hata nchi za Afrika Mashariki.
Kinachompa umaarufu na mvuto ni msimamo wake au yale anayoyasimamia na vipaumbele vyake ni pamoja na maridhiano ya kisiasa na hasa kwenye nishati inayolinda mazingira.
Boniface Mwamposa ni mtu anayefahamika zaidi mwaka huu. Akijiita Bulldozer ni mchungaji anayependwa na kuaminiwa na mamilioni ya wafuasi wake na wengine wasio wa kanisa lake.
Mchungaji huyo anatoa mahubiri kwa njia ya televisheni , redio na majarida amezidi kuwa maarufu sana, akiongoza Kanisa liitwalo Arise and Shine ambalo chini ya uongozi wake huduma yake imekuwa kwa kiwango kikubwa, na kuvuta wengi
Mwamposa anashawishi mkubwa, anafahamika bila kujali imani ya dini. Anafuatwa na mamia ya watu kutoka mikoa mbalimbali wakitafuta uponyaji na pia wanamuamini kuwa anaweza kufanya jambo na kubadili maisha yao.
Kanisa hufurika waamini kila siku na mkesha wa kumaliza mwaka wa Vuka na Chako na mingine kama Vuka Kabla hujavuka ni mambo yanayovuta watu wengi kuwa sehemu ya kusanyiko lake.
TUNDU LISSU
Tundu Lissu ni miongoni mwa watu ambao wanazidi kuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa Watanzania. Wengi wanafuatilia mambo yake kwenye mitandao ya mawasiliano, vyombo vya habari , hotuba na harakati zake kisiasa. Hata kile anachosema watu wanakinukuu kwenye vijiwe mitaani.
Umaarufu wa Lissu na ushawishi wake ni ule ambao hautokani na mamlaka za pengine hasa kuwa na cheo bali ni kutokana kazi anazofanya za kimkakati za kuchochea mabadiliko hasa ya kisiasa na kuondoa hofu na woga miongoni mwa Watanzania.
Ali Kamwe na Ahmed Ally nao ni maarufu, wanasikika na kufuatiliwa kila siku. Ni wasemaji wa Simba na Yanga wanaozungumza kila wakati kuhusu timu hizo.
Misemo yao mfano Ali Kamwe anasema “gusa achia” akimaanisha Yanga inavyocheza.
Wakati Ahmed Ally ni mwasisi wa kauli mbiu ya Simba ya ‘ubaya ubwela,’ asili yake Kizaramo ubaya umerejea na kwamba Simba imerudi kwenye ubora wake na ina kasi mpya.
Ruth Zaipuna ni Ofisa Mtendaji Mkuu au Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, amekuwa mtendaji kwa miaka mine sasa akianza tangu Julai 2020
Yeye ndiye mwanamke wa kwanza Mtanzania kuiongoza benki hiyo akishikilia nafasi hii, ambayo anawajibika kwa wateja wa benki, wanahisa ikiwamo serikali, watu binafsi na wengine wa nje na ndani ya Tanzania.
Dorothy Semu ni mmoja wa wanasiasa machachari wanawake akiwa mwanamama anayeongoza ACT Wazalendo, aliwabwaga wanaume kadhaa walokuwa wakisaka nafasi hiyo.
Anaongeza kukuru kakara za kisiasa kwenye upinzani, akitoa changamoto, maelekezo na kutaka kuwa na Tanzania mpya inayolinda na kudumisha demokrasia.
Anasisitiza na kukosoa, kwa mfano uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 2024 urudiwe maana haukuwa huru na haki.
YALIYOTIKISA ZAIDI
Ni kauli ya Nape Nnauye aliyesema:“Matokeo ya kura si lazima yawe yale ya kwenye boksi. Inategemea nani anayehesabu na kutangaza matokeo. Na kuna mbinu nyingi, kuna halali, kuna nusu halali na kuna haramu. Na zote zinaweza kutumika, ilimaradi tu ukishamaliza, unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe pale nilipokosea,” anawaambia wafanyabiashara katika soko la Kashai mjini Bukoba mkoani Kagera.
Habari mpasuko anayotoa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakati huo kabla ya kutumbuliwa aliibua mijadala baada ya kueleweka kuwa si lazima CCM ishinde kwenye boksi la kura bali zipo mbinu nyingine haramu.
Ilikuwa Julai mwaka huu akiwa katika soko la Kashai itakumbukwa kuwa Juni 2015, mkoani Mwanza alisema CCM itashinda hata kwa bao la mkono.
Anayasema hayo miezi mine kabla ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa uliolalamikiwa na upinzania kuwa ulijaa figisu.
MATUKIO YALIYOUMIZA
Mwaka unapoondoka mauaji ya kinyama ya mtoto Asimwe Novath mwenye ualibino yalihuzunisha wengi kuanzia kwenye vyomba vya habari, mitandao ya kijamii, vyombo vya usafiri hadi kwenye vijiwe mitaani.
Uchungu ulizidi zaidi kutokana na baadhi ya wauaji kudaiwa kuwa ni baba yake mzazi na pia yupo kiongozi wa kanisa anayetuhumiwa kupanga na kugharamia mauaji hayo.
Alifariki Mei mwaka huu nyumbani kwao Kamachumu mkoani Kagera.
Septemba mwaka huu Ally Mohamed Kibao, alishushwa kutoka kwenye basi la Tashrif jijini Dar es Salaam wakati likielekea Tanga na kuchukuliwa na watu wasiofahamika walikuwa na pingu na silaha. Baadaye mwili wake ulipatikana Ununio Dar es Salaam.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED