Wanaolia Januari ni chungu, kumbukeni nidhamu ya pesa

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 11:37 AM Dec 17 2024

Wazazi, walezi kumbukeni vifaa saidizi vya watoto wanafunzi wenye mahitaji maalum  ili wafurahie masomo Januari inapoanza.
PICHA: MTANDAO
Wazazi, walezi kumbukeni vifaa saidizi vya watoto wanafunzi wenye mahitaji maalum ili wafurahie masomo Januari inapoanza.

KIPINDI chenye gumzo la kila aina, kuanzia malalamiko nyumbani, kukimbia familia hadi kushtakiana kwa kudaiana fedha na mali kinaanza sasa.

Msimu huo unakaribia, ni baada ya mwezi Desemba kuendelea kuyoyoma ukifikia ukingoni mwa 2024 na kuikaribisha Januari 2025.

Ni msimu mwingine ambao wengi huuita pasua kichwa. Wazazi na walezi wanabungua bongo wakitaharuki kila wanapoona siku zinavyokimbia kuikaribisha Januari 2025.

Mwezi wa kwanza una mambo mengi mfano kama ni mpangaji iwe nyumba au eneo la biashara unawaza kudaiwa na kulipa kodi, ada au karo za shule kwa watoto ni jambo lisiloondoka kichwani, siku kuu za Noeli, mwisho na mwaka mpya, nazo wengi wanaziwaza.

Ndiyo maana Januari inaitwa majina mengi na kubwa zaidi ni mwezi mgumu unaojaa matumizi kuliko mapato.

Wapo watoto wanaoanza shule wa elimu ya awali, kuna wa darasa la kwanza na pia kidato cha kwanza.

Pamoja na hayo wapo wengine wanaorudi shuleni safari hii wakipanda ngazi mpya, alikuwa la pili anaingia la tatu.

Kadhalika kidato cha pili anaingia cha tatu, wote, wanahitaji maandalizi ya muhula mpya wa masomo unaoanza Januari 2025.

Wazazi na walezi wanapambana kununua vifaa vya shule kuanzia daftari, vitabu, sare, ada na wanaoingia kwa mara ya kwanza shule za bweni wana mahitaji makubwa zaidi.

Kwa kifupi Januari ni mwezi ambao wengine wanauona ni mgumu kwa kuwa wanaponda mali kumaliza mwaka bila kujali kuwa wana majukumu mengine mazito kuliko sherehe na ulevi ndani ya siku tatu.

Wakati Desemba inasisimua kutokana na sikukuu tatu za Chrismasi na kumaliza mwaka na kuanza mwingine mpya, wengi wanajisahau na kutoa kipaumbele hapo .

Wanapuuza suala za ada na heka heka za Januari na na hicho ndicho kisa cha kuuchukia mwezi huo.

ANZENI KUJIPANGA

Licha ya wazazi na walezi wengi kuzungumzia kwamba Januari ni kipindi kigumu inavyoelekea hawajagutuka na kuweka mipango kwa sababu suala la elimu ya watoto si geni walilifahamu na si dharura, linalojulikana.

Wapo wanawake wanawekeza kwenye vikoba lakini pesa wanazitumia kwenye mavazi, sherehe pengine kusafiri badala ya kuiangalia Januari iliyojaa majukumu muhimu.

ACHA KUFUJA

Jambo jingine linaweza kuwa kukosa nidhamu ya matumizi kutokutunza pesa au kuweka akiba.

Wengi wana mazoea ya kufanya matumizi mengi hata yasiyo ya lazima na inatokea kununua chochote hata kama hawakihitaji kwa wakati huo, ila kitanunuliwa kwa sababu kuna pesa mifukoni.

Kukosekana nidhamu kunajionyesha kwenye mengine mfano, wazazi au walezi wanaweza kutunza pesa ya ada au kodi ya biashara, kuanzisha biashara kama genge au mamalishe, lakini wanaposikia kuna sherehe wanabadilisha malengo na kutumia.

Mfano wakisikia harusi, mahafali, kipaimara au usafiri wa kwenda nyumbani kijijini mwisho wa mwaka wanazitoa na kupuuza mipango ya awali. Yote haya yanaponza.

Ni vyema kubadilika kwasababu wengi wanatafuta fedha kwa bidii lakini bila nidhamu ya matumizi mambo yanakuwa magumu na kusababisha kuichukia Januari.

Ni mwezi unaonekana wenye balaa wa shida. Ndiyo maana kwa wengine hawafanyi sherehe hasa harusi kwa sababu ni mgumu, na ikiwa utategemea michango ya watu kwa kiwango kikubwa. Fahamu utaikosa.

Mijadala ya kuiponda Januari na ushauri kutoka watu wengine, ipo kwenye mitando ya kijamii hata mazungumzo ndani ya jamii. Utasikia Januari ni mwezi ambao kabichi inakuwa nyama na sabuni ya magadi ni ya kila mtu.

LA KUKUMBUKA 

Kwa ujumla ili usiuone mwezi mchungu weka akiba kila wakati mwaka unavyoanza ikae benki au kwenye bidhaa pia kwenye mifugo kama kuku, mbuzi ama ng’ombe ili ukiuza upate fedha, kukwepa changamoto za kukosa karo na vifaa muhimu vya wanafunzi.

Jambo muhimu ni wewe kuweka malengo usiishi kienyeji, anza kuwa mtu wa kupanga mipango kwa kila program yako usilie eti Januari ni mwezi wa kilio.

Wazazi na walezi wajifunze kuweka akiba na nidhamu ya kutunza pesa kuliko kutumia kwa mambo ambayo si ya lazima.

Nyakati hizi katika shule za msingi za umma wazazi na walezi wafahamu kuwa ndiyo kipindi cha kuanza kufundisha mtaala mpya wa elimu ya msingi pamoja na masomo ya ufundi au amali.

Wanaoanza shule mwaka huu 2025 hawatasoma hadi darasa la saba, wataishia la sita na baada ya hapo wanaendelea na sekondari, hivyo chukua tahadhari mapema.

Kuna uwezekano mkubwa wa kuiona Januari chungu zaidi iwapo watoto wako wa familia moja watamaliza elimu ya msingi pamoja na kuendelea na ya sekondari, gharama za elimu zitaongezeka mara dufu. 

Wazazi na walezi waanze kujifunza sasa kuwa hakuna sababu ya kuishi kwa mazoea kuwa mbunifu, jiongeze na usongembele. 

Kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam na ukanda wa Pwani Januari yao ngumu kwani wanakabiliana na jua na joto kali, fukuto jingi mchana na usiku. Yote hayo yanawataka kunywa maji zaidi. Wao na watoto wao walioko shuleni.

Pamoja na jua na joto, bidhaa zimepanda bei lakini kilio ni kwamba wana mifuko mitupu. Poleni lakini mwisho wa kuilalamikia Januari uanze sasa.