Unavyoelekea kufikia ujio Tanzania, CHADEMA mpya

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:58 AM Dec 18 2024
Mtiania Tundu Lissu, akipongezwa na wanachama muda mfupi baada ya kueleza uamuzi wa kugombea uenyekiti.
PICHA: RESTUTA JAMES
Mtiania Tundu Lissu, akipongezwa na wanachama muda mfupi baada ya kueleza uamuzi wa kugombea uenyekiti.

HABARI kuu kisiasa hivi sasa ni uchaguzi wa viongozi wakuu wa CHADEMA, safari inayoanza na minyukano hadi kufikia mchuano mkali.

Pamoja na kwamba wagombea watatu wamejitokeza, mchuano mkali ni kati ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Tundu Lissu.

Mwanachama Odero Charles, anayejitosa kugombea pia hapewi wala hatajwi kwenye mitandao ya kijamii inayokosoa uwezo wa Lissu na Mbowe.

Wiki iliyopita, Lissu anautangazia umma nia ya kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, ili kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani, kuendesha siasa katika mazingira ya sasa anayosema ni CCM kutotaka uchaguzi wa ushindani ndani ya sanduku la kura.

Anasema kitendo cha asilimia kubwa ya wagombea wa upinzani kuenguliwa kwenye chaguzi 2019, 2020 na sasa 2024, kinawanyima wananchi haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Wakati Lissu akieleza hayo, Mbowe hajaweka wazi iwapo atagombea, licha ya kwamba amekaririwa akisema chama hicho hakijamzuia yeyote kugombea na kuhoji wanaomtaka astaafu ‘astaafu aende wapi?’

Pamoja na kimya cha Mbowe, Katiba ya CHADEMA ya 2006, inampa nafasi ya kugombea tena kiti hicho, alichokikalia kwa miaka 20 sasa.

Ni kwa sababu inaondoa ukomo wa uongozi, ambazo zinatajwa na Lissu kuwa ilikuwa ni kuweka kinga ya viongozi ili waweze kukijenga chama kwa uhakika, kwa kuwa wangeendelea kusalia madarakani kwa muda mrefu ikiwa watafanya vizuri.

UKOMO UONGOZI

Hili ndilo linalomfanya Lissu awe na agenda ya kuifumua katiba ya CHADEMA mara atakapotwaa madaraka.

“Nilipokwenda kujenga chama Singida Mashariki hakukuwa na viongozi wala wanachama, wachache tuliokuwapo tuligawana madaraka kutokana na uchache,” anasema.

Miaka 18 iliyopita, katika maeneo mengi, viongozi wa CHADEMA wamepatikana mezani bila uchaguzi, kwa wanachama wachache wa eneo husika kupeana vyeo kuanzia mwenyekiti hadi mjumbe wa mwisho, anaongeza.

“Busara ya mwaka 2006 ilitulazimu tuondoe ukomo ili chama kisikose wanachama. CHADEMA imekuwa sana, hakuna nafasi inayotolewa kwenye ‘kisahani’ kama miaka 18 iliyopita,” anafafanua Lissu.

Hata hivyo, anasema kwa mazingira ya sasa, kuweka vipindi vya kutumikia visivyo na mwisho, kunatengeneza watu kung'ang'ania madaraka na uchawa usio na sababu.

Anasema akichaguliwa kuwa mwenyekiti, atashirikiana na wenzake kuisuka katiba kwa nia ya kuweka ukomo wa madaraka pamoja na ubunge na udiwani wa viti maalum.

Anasema lengo ni kuruhusu mawazo mapya kuingia kwenye uongozi na wanawake wengi zaidi kwenye ubunge na udiwani.

Anasema nia yake ni kuwajengea wanachama wengi zaidi uzoefu wa uongozi na utumishi wa chama.

Lissu ambaye ni wakili kitaaluma, anasema nia nyingine ya kuisuka katiba ya CHADEMA kutengeneza mifumo bora ya uchaguzi ndani ya chama, ili ziwe huru na za haki.

Anaelezea pia kuwa kuna lengo la kuwa na tume huru kwenye chaguzi za chama, itakayoundwa na watu wasio na upande miongoni mwa wagombea. 

Anasema kwa miaka 20 amekuwa kwenye Kamati Kuu ya CHADEMA, na kwamba ikitokea akashindwa kwa haki katika uchaguzi huo, atabakia kuwa mwanamageuzi.

“Kipindi cha siasa ngumu kinahitaji watu wagumu. Wanaoweza kusimama hadharani wakasema maneno yanayostahili. Wenye msimamo wa kuaminika. Wenye uadilifu usiokuwa na shaka. Huu ni muda sahihi kwangu kugombea nafasi hii ya mwenyekiti,” anasema.

“Miaka 20 imenipa fursa ya kufahamu wapi panavuja, panapohitaji marekebisho na maboresho.”

Anasema hana timu na kwamba kile ambacho anaweza kumwambia mtu mmoja anakisema hadharani pia.

“Utimu si siasa zangu. Mimi nazungumza hadharani, ndicho nitakachokuambia tukiwa wawili. Naamini kuna watu ambao wanafikiria kama mimi. Kwamba kipindi hiki kinahitaji aina tofauti ya siasa.

LISSU NI NANI

Kama anavyoeleza mwenyewe kuwa ni mwanachama ambaye ametumika katika ngazi mbalimbali muhimu na zenye dhamana kubwa kwa zaidi ya miaka 20. 

“Nilianza utumishi wangu wa chama kama Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, baadaye nikawa Mwanasheria Mkuu wa Chama. Kwa kipindi kifupi, nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kati; na tangu Desemba 2019, nimekuwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara,” anasema.

Lissu amekuwa mbunge akiwawakilisha wananchi wa Singida Mashariki kwa vipindi viwili, hadi utumishi wake ndani ya bunge ulipokatishwa, akiwa kwenye matibabu.

Ni baada ya shambulio la risasi  Septemba 07, 2017 kwenye nyumba za serikali jijini  Dodoma.

Katika uchaguzi mkuu mwaka 2020, Lissu alipeperusha bendera ya CHADEMA kwenye nafasi ya urais, akichuana na John Magufuli wa CCM.

“Ninapenda kuamini kwamba, katika nafasi zote hizi, utumishi wangu kwa chama chetu na kwa nchi yetu, uliwapa ninyi wanachama na wananchi sababu kubwa ya kujivunia.

 Nje ya utumishi wa chama chetu, kama mnavyokumbuka, nimewahi kushikilia nafasi ya Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), kufuatia uchaguzi wa kihistoria wa Machi 2017, katika kilele cha utawala wa kidikteta wa Rais John Pombe Magufuli,” anasema.

Anasema tangu akiwa kijana, amekuwa mwanaharakati na mwanasheria jasiri katika masuala ya ulinzi wa mazingira na utetezi wa haki za binadamu.

Wakili, Lissu ni mmoja wa mawakili wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), aidha amewahi kuwa mtafiti katika masuala ya rasilimali za asilia katika Taasisi ya Rasilimali za Dunia (WRI), yenye makao makuu yake Washington DC nchini Marekani. 

“Ninaamini kwamba wanachama wenzangu mnaamini, kuwa nina sifa za kutosha za kugombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi katika chama chetu ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, kama zilivyoainishwa katika ibara ya 10.2 ya katiba,” anasema.

Uamuzi huo unafuta barua yake ya Agosti 06, 2024 aliyoiwasilisha kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, kutia nia ya kugombea nafasi anayoishikilia sasa, yaani Makamu Mwenyekiti.

Uamuzi wa Lissu umeibua maswali kwa baadhi ya makada wa chama hicho, ambao wanahoji sababu za kufuta barua yake ndani ya muda mfupi, wengine wakisema anagombea kwa shinikizo kutoka kwa watu wasioitakia mema CHADEMA.

Wanamtaja Lissu kuwa ataiweka CHADEMA kwenye hali ya sintofahamu kutokana na misimamo yake, hasa kutopenda mazungumzo na upande usioamini kile anachokiamini.

MWENYEKITI MBOWE

Wanaomuunga mkono Mbowe, wanamwona kama kiongozi aliyechangia kukua kwa CHADEMA kwa kuwa na mikakati na timu iliyokiwezesha kutwaa mitaa, vijiji na vitongoji vingi mwaka 2014 na wabunge na madiwani wengi kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Wanaona kwamba ni katika uongozi wa Mbowe, CHADEMA imekua na wanachama wengi, amejenga imani kubwa kwa umma kwamba ni makini kinachoweza kuongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni, halmashauri, manispaa na majiji makubwa, likiwamo Dar es Salaam.

“Mbowe ni mwanadiplomasia, anajua siasa na kubwa zaidi ni mtu aliyeibua wanasiasa wengi vijana akawajenga na kuwatangaza kwa umma kiasi cha wengine kudhihirika kuwa wanafaa na leo wanahudumu serikalini,” anasema Julius Massawe, kada wa CHADEMA mkoani Kilimanjaro.

Wengine wanasema diplomasia ya Mbowe imefanikisha kuwavuta mawaziri wakuu Edward Lowassa na Frederick Sumaye, kujiunga na CHADEMA, uamuzi wanaoona pengine hauwezi kufanywa na Lissu.