TANZANIA IKIWA TAYARI NA ‘PPP’ YAKE...

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 09:06 AM Feb 07 2025
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Hamad Yussuf Masauni, kando ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi na Serikali, mnamo Januari 28, 2025
Picha: Mtandao
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Hamad Yussuf Masauni, kando ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi na Serikali, mnamo Januari 28, 2025

AZIMIO la Dar es Salaam la wakuu wa nchi na serikali, kwa ajili ya kutoa nishati ya umeme kwa Waafrika milioni 300 hadi mwaka 2030.

Tayari imeshakubaliwa na kutiwa saini katika kikao cha kati ya Januari 27 hadi 28, mwaka huu na wakuu wa nchi 24 zilizohudhuria Mkutano wa Nishati Safi uliopewa jina ‘Mission 300.’

Ulikuwa na lengo la kuhakikisha upatikanaji, uendelevu na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi milioni 300 wa Afrika.

Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye katika mjumuiko huo sasa ana wasifu wa kuwa ‘kinara wa nishati safi ya kupikia Afrika.’

Pia, akiwa mwenyeji wa mkutano huo, bado ameona fursa kubwa kwenye miradi ya ushirikiano baina ya sekta binafsi na serikali, kwa kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii kwa kutumia mitaji ya umma.

Moja ya kipengele katika Azimio hilo ambalo litapelekwa kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) ambalo wakuu wa nchi walitia saini na kuridhia kuishirikisha sekta binafsi kwenye miradi ya nishati, ili kutumia mtaji wa umma kutatua changamoto za jamii na kuleta maendeleo.

Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa ni “Kuangaza Afrika kuwa na umeme jumuishi wa kuaminika ambao ni nafuu kwa watu wote” kwani zaidi ya watu milioni 600 wanakosa umeme na nishati safi ya kupikia.

Ili kufikia lengo Namba Saba la Malengo Endelevu ya Nishati kwa Wote mwaka 2030, zinahitajika jitihada za pamoja kupata nishati.

“Mkataba wa pamoja wa nishati, kutambua umuhimu wa ushirikiano na kutafuta fedha kwa ajili ya ajenda ‘300’ ambapo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambazo zimejipanga kufikisha nishati kwa watu mil 250 Afrika.

“Lakini, itawezekana ikiwa kutakuwa na ushirikishwaji, kuvutia mitaji kutoka sekta binafsi na kupata fedha za kuleta mabadiliko kwenye mifumo ya nishati Afrika,” anasema.

Wakuu hao wa nchi walisema kwenye Azimio hilo wanatambua kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa katika mnyororo wa uzalishaji na kusambaza na kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ni muhimu sana hasa kwa kuzingatia nishati ni muhimu katika kuchochea maendeleo na kutokomeza umaskini.

Pia, kuna kutoa vivutio kwa sekta binafsi kwa kutengenza mazingira wezeshi ya kisera na mipango kwa kujikita kwenye chambuzi za hasara na faida katika kuandaa sekta ya umeme Afrika.

Siku ya kwanza ya mkutano huo ilitanguliwa na majadiliano ya mawaziri wa nishati na fedha wa nchi hizo za Afrika, ambao walisisitiza dhamira yao ya kukuza ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) kwa kuwa na miundo bunifu ya ufadhili katika kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati barani Afrika.

Mawaziri hao ambao kwa Tanzania waliwakilishwa na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, wakasema mustakabali wa nishati barani Afrika unategemea juhudi za kijasiri zinazochanganya uvumbuzi wa kifedha na mifumo ya kimkakati ya sera.

Tanzania ikafafanua kuwa theluthi moja ya mahitaji yake katika kufadhili mahitaji ya sekta ya nishati, yanaweza kupatikana kutokana na mitaji binafsi.

Hadi sasa nchini kuna sheria, pia sera inayosimamia ubia huo wa PPP, hapo ikitoa ishara bora kwa ajili ya utekelezaji

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Dk. Samia, akafafanua kwamba katika kufikia malengo ya kujipatia nishati, sekta zote zinapaswa kushughulikia mambo yote yaliyopo kwenye mnyororo wa nishati.

Aanasema, hiyo inafanyika kwa kuweka sera na sheria nzuri za misaada ya kifedha na kiufundi kwa ajili ya ushiriki wa seketa binafsi kuwa na mifumo bora ya kifedha.

PPPC INAVYOIBEBA PPP

Hadi sasa, Tanzania imeshajipanga kutumia fursa ya PPP kwa kuanzisha Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), chini ya mkurugenzi wake, David Kafulila, anayesema wameshasajili miradi 82 iliyoko katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa kutumia mitaji ya umma.

Kafulila anasema, ubia ni ndoa ya ushirikiano na si ubinafsishaji kama inavyoelezwa na kwamba miradi ya ubia yote ni mali ya serikali na sekta binafsi inaingiza mtaji kuendeleza.

Aidha, amezitaja sababu za ubia kuwa ni kuvuna mtaji wa sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya serikali badala ya kukopa.

Kafulila anafafanua kwamba, fedha yake serikali inatumia kuwekeza kutekeleza miradi mingine, katika maeneo ambayo sekta binafsi haijaona fursa.

Amezitaja sababu nyingine za uwekezaji kuwa ni, kuvuta mitaji kutoka sekta binafsi,kuvuta tekonolojia ambayo utafiti unaonyesha in sekta binafsi imepiga hatua eneo hilo.

Nyingine anaitaja ni kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kwa kuwa sekta binafsi inamudu kusimamia mambo yake kwa ufanisi mkubwa bila urasimu kuliko ambayo serikali ingefanya.

Kwa mujibu wa Kafulila, ni uamuzi unaashiria ufanisi, akitoea mfano kuwa zipo sekta binafsi zinazoajiri wakurugenzi kwa mshahara mkubwa, hivyo kupitia ‘PPP’, sekta binafsi inaweza kununua mtaalamu mwenye ufanisi mkubwa kwenye utekelezaji wa miradi.

Kafulila anasema, mahitaji ya binadamu yanaongezeka kila siku kuliko uwezo wa serikali yoyote duniani kuyamudu na kwamba, chanzo cha mapato cha serikali ni kodi na mikopo ,hivyo haiwezi kumudu kuyatimiza bila ‘PPP’.

"Uzoefu unaonyesha kuwa serikali haiwezi kufikia matarajio kwasababu inategemea kodi na mikopo. Deni la dunia kwa sasa ni dola trilioni 300, huku uchumi ukiwa ni dola trilioni 110 ambayo ni mara tatu ya Uchumi.

"Deni hili ni la serikali, sekta binafsi na kaya...hii inaonesha kuwa hatuwezi kukwepa kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza miradi, leo mtu wa Kigoma Vijijini (anakotoka Kafulila) atatamani maisha kama ya mtu wa Kigoma Mjini. Siku akiyapata, atataka ya juu zaidi, hivyo mahitaji ya binadamu yanaongezeka kila siku,"anasema.

"Huwezi kutimiza mahitaji kwa kukopa,lazima ualike sekta binafsi ije na mitaji yake itekeleze,kwa kutumia ‘PPP’ unatekeleza miradi bila kugusa bajeti na kupunguza shinikizo kwenye vitabu vya serikali.Ilemela mmefanya uamuzi sahihi,"anasema Kafulila.