Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umezindua Baraza la Wafanyakazi linaloendeshwa kidijitali kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na kusaidia jitihada za kulinda mazingira.
Uzinduzi huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF, Joyce Mapunjo, ambaye aliipongeza Menejimenti kwa hatua hiyo muhimu katika kuongeza ufanisi wa baraza.
Sambamba na uzinduzi huo, Mapunjo alifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa PSSSF kilichoanza Februari 6 na kinatarajiwa kukamilika Februari 7, 2025.
Mwenyekiti huyo amewataka watumishi wa PSSSF kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa wanachama ili kuhakikisha malengo ya Serikali inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yanafikiwa. Alisisitiza umuhimu wa kila mfanyakazi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kusaidia Serikali kufikia malengo yake ya kuwahudumia wananchi, wakiwemo wastaafu wa PSSSF.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la PSSSF ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru, alisema kuwa kila kinachofanywa na PSSSF kina lenga kutafsiri ndoto kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga Taifa imara kiuchumi.
Akizungumzia Baraza hilo kuendeshwa kidijitali, Badru alisema, "Lengo kubwa ni kuendana na jinsi tunavyowahudumia wanachama wetu, kwani hivi sasa tunawahudumia kidijitali na sisi tunapaswa kwenda vivyo hivyo. Pia najua Baraza ni chombo muhimu katika kutoa maamuzi, Baraza la PSSSF linashirikishwa katika mambo yote muhimu ya uendeshaji na linaleta tija katika utendaji wa Mfuko."
Peles Jonathan-Hageza, Mjumbe wa Baraza la PSSSF kutoka TUICO Makao Makuu, aliipongeza PSSSF kwa jinsi inavyoshirikiana na Baraza hilo katika masuala mbalimbali muhimu ya kiuendeshaji.
Baraza la Wafanyakazi la PSSSF la sasa ni baraza la pili tangu kuanzishwa kwa PSSSF mwaka 2018.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED