TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma imekuwa na utaratibu wa kuandaa midahalo mbalimbali inayohusisha wanafunzi wa vyuo vikuu, sekondari na shule za msingi.
Hapo mtazamo ni kupanua wigo wa uelewa kwa jamii kuhusu madhara ya kutoa rushwa au kupokea mahali pa kazi, vyuoni na kwingineko.
Mwezi uliopita, TAKUKURU mkoani Dodoma, kwa kushirikiana na wadau, ikiwamo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, pia Mamlaka ya
Kupambana na Dawa za Kulevya, wakaandaa mdahalo uliohusisha vyuo vya Elimu ya Juu na kati, ukilenga kuwapa elimu Wanafunzi, jamii na makundi tofauti walioalikwa.
Mada mojawapo ilijadili kukosekana uzalendo, kunavyomnyima raia haki ya msingi ya kufanya uamuzi sahihi kwenye, kitendo ambacho TAKUKURU ilidhamiria kuwekwa mikakati ya kuhakikisha elimu inafikia kupata uelewa unaohusu suala hilo.
Baadhi ya vyuo vilivyoleta washiriki kwenye mdahalo huo, ni wasomi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo cha Mipango na Maendeleo yaVijijini (IRDP), Chuo cha Serikali za Mitaa na Chuo cha Ufundi VETA.
Hapo wamekuwa wakibadilishana hoja kuhusu rushwa inavyoathiri miradib ya maendeleo, taasisi, pia mtu mmoja mmoja.
Katika majibizano yao kwa hoja za msingi, yalizidi kuongeza wigo wa uelewa wa madhara ya rushwa, huku jamii ikijitokeza kushuhudia mdahalo huo, lengo kuu ilikuwa ni kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuelewa juu ya madhara ya utoaji rushwa kwa jamii inayotuzunguka.
Hilo limeifanya taasisi hiyo kuanzisha klabu za kupinga rushwa ngazi ya vyuo vikuu, kati, shule za msingi na sekondari mkoani Dodoma, hata kutumika kuwa mabalozi wa kusaidia kupiga vita rushwa, pamoja na kuielimisha jamii katika maeneo wanayotoka.
Taasisi ya rushwa mkoani hapa, kwa kushirikiana na walimu wa shule hizo, kupitia maofisa wa TAKUKURU, wamekuwa wakitoa elimu kwa klabu husika, ili kuwajengea uwezo wanafunzi wanaounda klabu, kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha katika maeneo wanayotoka, pindi watakapohitimu.
Hilo limetokana na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, ikielezwa shuleni kupinga rushwa kutoa upinzani mkubwa katika midahalo inayohusu kupiga vita rushwa, chini ya usimamizi wa taasisi hiyo wanapoalikwa kushiriki.
Maofisa wa TAKUKURU, katika hatua yao wanatanua wigo wa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali mikoani kwa kushirikiana na walimu wa klabu katika shule na vyuo mbalimbali ambazo hazijaundwa.
MKUU TAKUKURU MKOANI
Victor Swella, anasema siri ya mafanikio kwenye vita hivyo dhidi ya rushwa, ni kutolewa elimu kwa wenye rika hizo, ili kuwajengea uwezo tangu awali ya kukataa vitendo vya rushwa, popote penye viashiria vya aina hiyo.
Swella anasema, uanzishwaji klabu hizo ni pamoja na kuhitaji kupanua wigo wa utoaji elimu kwa jamii, kuhusu vita vya rushwa, huku ikiwaandaa kuwa mabalozi wa kupiga vita rushwa sehemu zao baadae katika maeneo watakayokuwa pindi watahitimu masomo yao.
Swella anasema: "Tunahitaji kuona elimu ya kupiga vita rushwa inaenea katika maeneo mbalimbali ndio maana unaona tumeshirikiana na baadhi ya vyuo vikuu, vya kati pamoja na shule za msingi na sekondari.
Anaendelea: “Ili kuhakikisha elimuya kupiga vita rushwa pamoja na madhara yake inaenea kwa kiasi kikubwa."
Kwa mujibu wa Swella, TAKUKURU mkoani Dodoma, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu tafsiri pana ya vita vya rushwa, akitaja vinachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha miradi ya maendeleo ya kimkakati serikalini.
Anafafanua kuwa, katika utekelezaji jukumu la kutoa elimu, wamewafikia wananchi takribani 78,896 kwa njia ya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.
Lingine, anataja mafanikio ya utoaji elimu kwa njia ya maonesho yaliyolenga elimu ya madhara ya rushwa, ifanikiwe akiwa na ufafanuzi kwamba:
"Kuna klabu 670 za wapinga rushwa ambazo zipo vyuoni, sekondari, pamoja na shule za msingi.
“Ni klabu zinatengeneza mabalozi wazuri katika utoaji elimu kwenye maeneo wanayotoka na kwenye hili, tumezidi kupanua wigo wa utoaji elimu ya madhara ya rushwa,"anasema Swella.
MWENYEKITI MIDAHALO
Mwenyekiti wa Midahalo ya TAKUKURU, Dodoma mjini, Francis Magoha, anasema midahalo ya TAKUKURU huandaliwa kwa ushitrikiano na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, imekuwa kivutio kwa wanafunzi kujiunga na vilabu vya rushwa vyuoni na shuleni.
Magoha anasema, TAKUKURU imekuwa ikiendesha midahalo kwa nyakati tofauti, ikizihusisha shule na vyuo vya ngazi tofauti, kukiwapo mada zinazohamasisha madhara ya rushwa kwenye mikusanyiko.
Anaisifu kuwa, imesaidia kutoa elimu kwa wanafunzi, katika mtazamo mpana wa kupiga vita rushwa katika maeneo mbalimbali, ikiwamo masomoni kwa tafsiri “rushwa kwa mtu yeyote hairuhusiwi.”
Magoha anataja hali ya midahalo hiyo, imekuwa ikifanyika kila mwaka kwa kuwakutanisha wanavyuo wa elimu ya juu na kati, huwa wanajibazana kwa hoja lengo ni kuona namna wanapata uelewa kuhusu suala zima la kupiga vita rushwa
WASHIRIKI WANENA
Sauda Mahamudu, kutoka chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anasema elimu ya kupiga vita rushwa isiishie kwa wanafunzi, bali kumfikia kila mwananchi kuyajua mapambano dhidi ya rushwa si ya mtu mmoja mmoja, bali ya wote.
“Elimu hii isiishie kwa wanafunzitu bali ifike hadi pembezoni ili kuhakikisha wananchi wanaelewa madhara ya utoaji rushwa mahali pa kazi sio jambo sahihi,” anasema Mahamudu.
Mshiriki Ibrahimu Kayonko, anasema elimu inapaswa kutolewa zaidi pembezoni, ili kuwasaidia wananchi kuelewa madhara ya utoaji na kupokea rushwa katika maeneo mbalimbali.
Anasema kuanzishwa vilabu vya kupinga rushwa katika vyuo na shule za msingi na sekondari, imewasaidia wanafunzi kupata uwelewa zaidi ya madhara ya rushwa kwa mtu anayetoa na anayepokea.
DC DODOMA MJINI
Jabiri Shekimweri ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, anaipongeza TAKUKURU Dodoma kwa kuendeleza wigo wa utoaji elimu ya kupinga rushwa katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Anasema, ni hali inayozidi kuonesha nia ya kuungana na serikali katika mapambano dhidi ya rushwa.
Shekimweri anasema, ubunifu wa kuanzisha klabu za kupinga rushwa vyuoni na shuleni ni jambo zuri, kwa sababu wameanza kutengeneza mabalozi wa kupiga vita rushwa kutoka wakiwa elimu ya msingi, jambo analolisifu kuwa zuri ndani ya jamii inayowazunguka.
“Hii imesaidia kuongeza wigo wa utoaji elimu kwa jamii, lakini kushawishi watu wajiunge kwenye klabu za wapinga rushwa,”anasema Shekimweri.
Anafafanua kuwa, elimu ya madhara ya kupokea na kutoa rushwa, inapaswa kuzingatiwa, kwa sababu watu wasipokuwa na elimu ya rushwa, itawawia vigumu kujua madhara yanayotokea pale mtu anapotoa rushwa au kupokea rushwa ili afanikishe suala lake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED