ZAO la Chai ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi nchini. Linaongeza ajira na pato la mtu mmoja mmoja.
Kwa miaka kadhaa wakulima wa zao hilo, wamekuwa wakipitia wakati mgumu kupata masoko ya uhakika jambo ambalo liliwakatisha tamaa baadhi yao.
Hata hivyo, kwa sasa pasina shaka juhudi za kiserikali zimejikita katika kutatua tatizo hilo. Jitihada kubwa imeelekezwa katika kutafuta masoko mapya na kurejesha yaliyopotea.
Hivi karibuni, bodi yenye mamlaka na zao hilo, imerejesha soko la chai la nchini Oman na Sudani na sasa uongozi wake umekwenda nchi za Saudi Arabia kwa lengo la kuongeza soko la bidhaa hiyo katika nchi za Kiarabu.
Kwanini Uarabuni? Hiyo inatokana na desturi za watu wengi kutoka nchi hizo, kupenda kinywaji hicho.
Ni jitihada zinazoacha tabasamu kwa wakulima pale wanaposikia mipango na jitihada wanapiganiwa zao lao kumea.
Jingine kubwa, ni kile kitendo cha kuwaleta nchini wataalamu wa chai kutoka Japan, waliotembelea mashamba yaliyoko katika mikoa ya Njombe na Iringa na baadhi ya viwanda vinavyochakata chai kwa lengo la kujifunza fursa zilizopo na kubadilishana uzoefu katika zao hilo.
Hata hivyo, walionesha kuipenda chai ya Tanzania wakiisifu ni nzuri kutengeneza kinywaji cha kijani, ambayo nchini kwao imeshika soko.
Jitihada hizo, ni mpango madhubuti wa serikali katika kuinua sekta ya chai na wakulima wake na hata kumaliza vilio vyao vya kila siku vya kukosa soko.
Kutokana na ujio wa Wajapani, kunafafanuliwa kwamba matarajio yao baada ya ugeni huo ni mapinduzi ya viwanda na kuongeza ubora wa chai, ili iwe rahisi kulikamata soko la ndani na nje ya nchi.
Sambamba na juhudi hizo, pia serikali inaendelea na mpango wake wa kushawishi wawekezaji kuwekeza katika sekta kwa kujenga viwanda na kulima mashamba makubwa.
Katika ufafanuzi wake, chombo chenye mamlaka na zao hilo, kinasema hali ya soko inazidi kuwa nzuri na hata maeneo waliyokwenda wameonesha kuikubali chai ya Tanzania.
Selemani Chillo, ofisa wa kiserikali mwenye dhamana hiyo anatamka: “Tunaendelea na juhudi za kushawishi na kuitangaza chai yetu nje ya mipaka ya Tanzania, kushawishi wawekezaji tunaamini tukifanikiwa katika hilo thamani ya zao hilo itakuwa juu na watu wataipenda chai ya Tanzania.”
Kwa kifupi, ipo mipango mingi inayoratibiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, ikiwamo kufanya uwekezaji utakaoendana na teknolojia ya kisasa, mkakati wa kuweka viwanda vidogo viodogo katika mashamba ya wakulima, utanuzi wa masoko, pamoja na kuvuta wawekezaji kutoka nchi za nje.
Ofisa Kilimo Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo, Bahati Majaliwa, anasema mpango wa serikali ni kujenga viwanda vidogo vidogo vitakavyo wasaidia wakulima kusindika chai ili waweze kupata faida zaidi kutokana na mauzo.
"Wajapan wameipenda sana chai yenye majani membamba, na inazalishwa kwa wingi, katika maeneo mengi ya uzalishaji hapa nchini ikiwamo yale ya mkonge lakini nchini kwetu ni zaidi ya asilimia 80 ya chai hiyo inazalishwa.
"Wakulima waendelee kutunza mashamba yao vizuri ili kupata tija kutokana na majani watakayozalisha" anasema Majaliwa aliyekuwa miongoni wa walioongozana na ugeni huo kutoka Wizara ya Kilimo
Majaliwa anasema mkakati wa Wizara ya Kilimo kwa sasa ni kuhakikisha wakulima wanasindika chai yao na kwamba mpango uliopo ni kuwekeza katika viwanda vya wakulima wadogo.
"Bado Wizara ina nia ya kuhakikisha uwekezaji viwanda unafanyika ili wakulima waweze kusindika chai.
"Wakulima wa chai watambue serikali inaendelea na jitihada kuhakikisha zao la chai linaendelea hapa nchini kwa kuweka viwanda vya wakulima wadogo" anasisitiza.
Anasema ujenzi wa viwanda kwa wakulima wadogo utasaidia kuwainua kiuchumi na kuzalisha chai yenye tija itakayoleta ushindani katika soko la kitaifa na kimataifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED