UNYANYASAJI na ukatili kijinsia unaohusisha kutelekeza familia, vipigo, watoto kuozwa, kuingiliwa kinyume cha maumbile, mimba utotoni, kunyanyasa wanawake wenye VVU, kuua wazee kwa kusingizia wachawi ni tatizo mijini na vijijini.
Taarifa ya Jeshi la Polisi kuhusu ukatili wa kijinsia inaonyesha kuwa wanapokea malalamiko mengi kwenye madawati ya kijinsia na kwenye ripoti zinazofikishwa vituo mbalimbali.
Maelezo hayo yanayotolewa Julai mwaka huu yanaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Desemba 2023 matukio ya unyanyasaji kijinsia na ukatili yalikuwa 22,147 kwa watu wazima.
Wanawake walionyanyaswa walikuwa 13,322 wakati wanaume walikuwa 8,825 . Ripoti ya polisi inasema kuna ongezeko wakati mwaka 2022 kipindi kama hicho yalikuwa 18,403 ziada inaoneka 2023 kwa kuwa na matukio 3,744.
Ripoti inasema kuna ongezeko kubwa la unyanyasaji kijinsia kwa watoto mengi yakifanyika ndani ya familia na kwenye jamii pia. Yanahusisha kuuawa, unajisi- ulawiti, kubaka, mimba za utotoni na vipigo kupindukia.
Wakati huu dunia inaposisitiza haki kwa wanawake, wasichana na watoto inakumbusha kupinga ukatili kwa kuzingatia Siku 16 za Kupinga Ukatili Kijinsia, ukirejea kwanini ukatili unakithiri kuwepo mimba za utotoni licha ya jitihada za kutoa elimu kuhusu ulinzi wa watoto, kuwafundisha kujitetea na kujilinda sheria zinaendelea kuwa kikwazo.
Kwa hiyo mzizi ni sheria, kama ya ndoa ambayo inaruhusu binti wa chini ya miaka 14 kuozwa kwa kibali cha mahakama, mzazi au mlezi.
Licha ya Mahakama ya Rufani kuamuru vifungu 13 na 17 vya sheria hiyo virekebishwe bado serikali inakaa kimya wasichana wakiendelea kuathirika.
Sheria nyingine chanzo ni ya ajira na mahusiano kazini ya 2004 zote zinawanyanyasa watoto hasa mabinti na kusababisha kupata mimba, kudhalilishwa, kutosoma na hata kuuawa.
Sheria ya kazi ya 2004 inaruhusu watoto wenye miaka 14 kupata ajira na kufanyakazi nyepesi. Hizo kazi ni zipi ni nani anayesimamia? Ikumbukwe kazi ni kazi ukimruhusu mtoto akawe ‘hausi geli’ at ‘shamba boy ‘mjini hata kama ana miaka 14 lazima apitie magumu.
Sheria mathalani inasema watoto hawaruhusiwi kufanyakazi zaidi ya saa sita. Ni nani anayejua hayo akiwa nyumbani kwa mwajiri pengine yuko Arusha, Dodoma na familia yake iko Mtwara?
Sheria inaeleza ajira haramu ni ile inayomkwamisha mtoto kwenda shule, ni ile inayomwathiri mtoto kimwili na kisaikolojia. Inakuwaje watoto waruhusiwe kufanyakazi ambazo zinakiuka vigezo hivyo na walitakiwa kuwa shule?
Wakati mwingine sheria hizi zinachochea unyanyasaji watoto na kusababisha mimba, ndoa, ubakaji, ulawiti na utumikishwaji haramu kwenye mashamba ya tumbaku, mifugo na kilimo kwa ujumla.
Ipo sheria ya matunzo ya mtotto aliyezaliwa lakini baba na mama hawakufunga ndoa. Inamtazama zaidi mtoto lakini inaelekeza kiasi kidogo cha fedha kitolewe kulipia gharama za matunzo. Awali ilikuwa Shilingi 100 kwa siku, lakini baada ya marekebisho inaagiza mzazi mama kupewa Shilingi 3,500 kwa mwezi.
Kadhalika sheria hiyo haimjali wala kumzungumzia mama mtoto ambaye ametelekezwa.
Hiki ni kikwazo kwa sababu fedha hizo ni kidogo mno, 3,500 kwa siku ikichanganuliwa inanunua kipimo kimoja cha mkaa 2,000 na fungu la mboga Sh. 800 na mafuta kipimo kimoja mijini.
Ikumbukwe mama anahitajika kumhudumia mtoto asubuhi, mchana na jioni. Kadhalika analipa kodi ya nyumba ambayo ndogo ni Shilingi 20,000 kwa mwezi. Hivi kwa gharama hizo maisha ya mtoto yanakuwaje? Ni magumu bado hasa mijini.
Sheria ya Mtoto ya 2009 haijamgusa mama mzazi kwa kuzingatia sheria ya ndoa pale ambapo wazazi wametengana na kutalikiana, mtoto atakuwa na haki zake za msingi. Sura ya 26:1(a),(b),(c) inaongelea haki ya mtoto wazazi wanapotengana.
Hivyo upungufu mkubwa, mama anayetelekezwa, pamoja na mtoto wake hawajaunganishwa moja kwa moja kisheria.
Inaelekea sheria haimtambui mama mzazi ikumbukwe ametelekezwa kuwe na sheria za kumuwajibisha na kumwadhibu baba anayehusika na uvunjaji wa sheria ya kukataa familia yake.
Kwa kutumia mwanya au udhaifu huo wanaume hawajali kutelekeza wanawake ndiyo maana ukatili unazidi.
Watu wengi wanaipuuza sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 maarufu kama SOSPA hutumiwa kuficha makosa na hata kujitajirisha.
Wapo baadhi wajanja wakisikia kuna mtuhumiwa kampa mtoto mimba wanaitumia kumweleza kuwa atafungwa miaka 30 au kama kanajisi mtoto mdogo ni jela maisha, hivyo wanatumia mbinu kuvuruga kesi na ushahidi ili wapatee fedha wayamalize na kuishirikisha familia ambayo inalipwa kiasi kidogo ili kukaa kimya.
Baadhi ya wachache wanaoweza kutumia mwanya wa ‘umbumbumbu’ wa sheria kuwa ni pamoja na viongozi wa vijiji au mitaa, mawakili, walimu shuleni na wana familia wenye tamaa ya fedha au mali.
Kwa kutumia udhaifu wa kupata pesa wahusika huongea na wazazi wa waathirika kisha kuchukua hela na kuwapa ujanja wa kukimbia na kukwepa kesi ikiwamo kukataa kutoa ushahidi.
Kutoa hela si jambo gumu ni rahisi kwenye jamii za wafugaji ambao wanaendekeza mila potofu hivyo wao kutoa ng’ombe 20 au hata Shilingi 1,000,000 ili kukwepa kesi hizo haisumbui.
Kwa ujumla kuumiza watoto kunachangiwa pia na kula rushwa na kusababisha mabinti kupewa ujauzito na kesi zao kuishia kinyemela baada ya watu kula mlungula.
UTASHI WA KISIASA
Ukosefu wa utashi wa kisiasa pengine ndicho chanzo kingine kuendeleza mfumo dume na unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa watoto.
Mfano serikali hata sasa haijarekebisha Sheria ya Ndoa ya 1971 licha ya Mahakama ya Rufani kuagiza baadhi ya vifungu kandamizi vifutwe.
Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini ni mwiba wenye ncha kali kwa ajira za watoto.
Wananchi wanatamani wanaonyanyasa watoto wakikamatwa na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao. Lakin mara nyingi haki inachelewa, haionekane ikitendeka, hukumu zinachukua muda mrefu.
Rushwa nayo ni tatizo. Baadhi ya wahusika wasio waadilifu mitaani, vijijini, mahakamani, ndani ya jeshi la polisi hushirikiana kukwamisha kesi za kuzuia unyanyasaji watoto, mimba au ndoa za utotoni.
Ndiko kushirikiana na wazazi, walezi na watoto kumaliza kesi hizo baada ya kupewa kitu kidogo na kwa wengine huendelea kutolewa mara kwa mara, hivyo kupata pa kulia.
Wakati mwingine madawati ya jinsia yanakosa ofisi, mafunzo, vitendea kazi kama magari, kompyuta, ‘printa’ na kuendeshwa bila bajeti ni moja ya mambo yanayoongeza ukubwa wa tatizo hilo.
UFUMBUZI
Kuanzisha ofisi moja inayoshughulikia matatizo ya waathirika wa unyanyasaji iitwayo “One Stop Centre ianzishwe kwenye zahanati za vijijini, vituo vya afya vya kata na ofisi za serikali za mitaani kwenye majijini na miji.
Kadhalika kwenye hospitali za wilaya huduma hizo ziwepo, ‘one stop centre’ ziwe na daktari, polisi kushughulikia jinai, ustawi wa jamii na wanasaikolojia kutoa misaada ya kisheria na wanasheria kwa ajili ya kesi.
Lazima jamii iamke kuanzia viongozi wa dini, walimu, wazazi na wana familia kupinga ukatili wa kijinsi ili kila mmoja afahamu kubaka, ulawiti, ngono kinyume cha maumbile, kutelekeza, vipigo kuuana ni nini na ni hatia.
Kuwe na kufundisha maadili shuleni, kutoa elimu ya haki za binadamu na pia sheria nyingine kama ile ya kupima nasaba (DNA) na ile usafirishaji haramu wa binadamu zijulikane.
Wananchi wanatakiwa kufahamishwa kuwa kuna maabara zenye kipimo cha kupima DNA hivyo kuua, kukimbia mimba, kutekeleza familia siyo suluhu kuna hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa na mtuhumiwa akaadhibiwa kisheria.
Ofisi ya ustawi wa jamii ya kijiji na polisi zipewe bajeti ili zipokee taarifa , kuzichunguza na kuzifuatilia na kuziwasilisha polisi wilayani na kwa Mkuu wa Wilaya mara moja kwa hatua.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED