Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa suala la matumizi bora ya Nishati linapaswa kuwepo kwenye mipango ya Serikali katika nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuwezesha nchi hizo kutumia umeme kwa ufanisi na hivyo kupunguza upotevu wa umeme.
Dk. Biteko amesema hayo leo tarehe 04 Desemba 2024 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati (REEC 2024) ulioandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland ukishirikisha Viongozi na Wadau mbalimbali wa Matumizi Bora ya Nishati kutoka EAC na SADC.
Amesema pamoja na nchi mbalimbali barani Afrika kuzalisha umeme na kusafirisha kwa ajili ya matumizi lakini bado kuna chagamoto za kuhakikisha kuwa umeme huo unaozalishwa na kusafirishwa unatumika kwa ufanisi.
“ Kwa mfano kuna sababu gani ya mtu hayumo ndani ya nyumba lakini vifaa vyote vya umeme kama vile luninga, kiyoyozi, televisheni, radio na taa wakati wote vinafanya kazi, vitendo kama hivi vya kutumia umeme bila ufanisi vinaongeza mzigo kwenye uzalishaji wa umeme, umeme ambao kiasi kwa kiasi fulani ungeweza kutumika kwa mahitaji mengine.” amesema Dk. Biteko
Ameeleza kuwa, takwimu za Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (IEA) zinaonesha kuwa ufanisi wa nishati duniani umeimarika kwa asilimia 1.1 tu mwaka 2023 ikiwa ni chini ya lengo kwani kwa sasa ufanisi wa nishati unatakiwa kukua kutoka asilimia 2 hadi 4 hivyo ili kufikia lengo hilo nchi za Afrika zinahitaji kushirikiana katika kutatua changamoto zinazopelekea kutokuwa na matumizi bora ya nishati.
Amesema Mkutano wa REEC 2024 uwe ni sehemu ya kuweka msisitizo kuwa matumizi bora ya nishati si suala la hiari bali ni la lazima na msingi katika upatikanaji wa nishati ya uhakika, kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na kuwa na ukuaji wa uchumi ambao ni endelevu.
“Uwepo wa Viongozi, Wataalam na wadau wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali za Afrika utafanya mkutano wa REEC 2024 kuwa wa mafanikio kwani utahusisha pia kubadilisha uzoefu na utaalam katika matumizi Bora ya Nishati na utaiwezesha Tanzania na Bara zima la Afrika kufikia suluhisho la upatikanaji wa nishati safi.” amesema Dk.Biteko
Dk.Biteko ametilia mkazo uwepo wa teknolojia za kupikia zenye ufanisi wa nishati ili kupunguza gharama za nishati majumbani, kuwa na hewa safi ndani ya nyumba, na kulinda misitu dhidi ya matumizi ya kuni kupita kiasi.
Aidha ameishukuru EU, UNDP na Ubalozi wa Ireland kwa kuunga mkono Serikali katika uandaji wa Mkutano huo wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati pamoja na Benki za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) zinazounga mkono mikakati mbalimbali ya kuendeleza Sekta ya Nishati nchini na kutoa wito kwa wadau hao wa maendeleo kuendelea kutoa mchango wao kwenye ufanisi wa matumizi ya nishati nchini bila kusahau nishati safi ya kupikia.
Katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Mkutano wa REEC 2024, Dk. Biteko amezindua Mkakati wa kwanza wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Nishati (2024-2034) ambao pamoja na masuala mengine unalenga kuhamasisha watanzania kutumia nishati kwa ufanisi ili kupunguza gharama za matumizi, kupunguza upotevu wa umeme na kutunza mazingira.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda amesema REEC 2024 unahamasisha fursa za ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuweka miongozo wa matumizi bora ya nishati katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Amesema siku mbili za mkutano huo zitaleta matokeo mbalimbali ikiwemo kuongeza uelewa kuhusu matumizi bora ya nishati, kutatua changamoto zinazojitokea katika utekelezaji wa mikakati ya matumizi bora ya nishati na kuwa na ushirikishaji wa Sekta binafsi katika matumizi bora ya nishati.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema mkutano wa REEC 2024 ni mkutano unaoendana na Sera ya Nishati ya Tanzania ya mwaka 2015 inayotambua kuwa kama taifa linahitaji nishati ya kutosha lakini inayotumiwa uangalifu, umakini na ubora ili kuhakikisha nchi haizalishi nishati isiyoihitaji na haingii gharama ambazo isingeziingia endapo ingetumia nishati kwa ufanisi.
Amesema kwa upande wa Tanzania, ili kuwa na matumzi Bora ya Nishati, Serikali ya Tanzania kwa kushirikina na Wadau wa Maendeleo inatekelza mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati utakaowezesha watanzania kutumia nishati kwa ubora na kwa uangalifu na hii ikienda sambamba na kusimamia aina ya vifaa vya umeme vinavyoingia nchini ili kuingiza vifaa vyenye ufanisi na ubora unaotakiwa.
Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Amon Manyama amesema UNDP inajivunia kufanya kazi na serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa Mradi wa Matumizi Bora ya Nishati.
Amesema Mkutano wa REEC 2024 ni muhimu katika kuhamasisha na kuchagiza matumizi sahihi ya nishati kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Kusini mwa Afrika.
Aidha, EU na WB zimeipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa miradi ya Nishati ikiwemo mradi huo wa Matumizi Bora ya Nishati na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye miradi ya maendeleo endelevu itakayoinua uchumi wa Watanzania huku ikilinda mazingira.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED