Shule zinapofungwa mzazi ,mlezi usisahau

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:51 PM Dec 04 2024
Shule zinapofungwa mzazi ,mlezi usisahau
Picha:Mpigapicha Wetu
Shule zinapofungwa mzazi ,mlezi usisahau

SHULE za msingi na sekondari zinakaribia kufungwa kuanzia wiki hii suala la kusoma, kufurahia masomo katika mazingira mazuri pamoja na kufaulu bado ni kipaumbele.

Usalama wa watoto na ulinzi wao ni jambo linalohitajika  na ndilo la msingi wa kila kitu  wazazi,walezi na jamii kumbukeni kulipa umuhimu wa kipekee.

Ulinzi na usalama unamgusa kila mmoja ili kuwaangalia watoto au wanafunzi kuanzia shuleni wanaposoma , mitaani wanapokaa na mambo muhimu wanayohitaji ili kuwasaidia wasome salama wakati huu wakiwa likizo. 

Ni kwa sababu watoto wengi wanaoathirika na ukatili wa kijinsia hasa mabinti kupewa mimba, kutumiwa kingono na walimu au walezi na wazazi, kadhalika wasichana na wavulana wanaingiliwa  kinyume cha maumbile, yote hayo yakichangiwa na kukosekana ulinzi na jamii kuwapuuza.

Ukiangalia zaidi eneo la kuendeleo na maandalizi ya elimu ya sekondari hasa wanaomaliza msingi kila mmoja anawaalika kujisajili na ‘pre-form one’ ili iwe rahisi wanapofika sekondari.

Wanachojifunza ni masomo ya kidato cha kwanza hasa Kiingereza kwa kiasi huko nako kuna udanganyifu.

Watoto wanaweza  kulazimishwa kufanya mambo ya kihalifu mitaani kwa kisingizio kuwa wamekwenda shuleni lakini wakatumbukia kwenye mikono ya wanyanyasaji.

Familia zikumbuke kuwa kusoma  hiyo ‘pre form one’pasipo na chakula kunamaanisha njaa isiyovumilika, matokeo yake ni mabinti binti kufanya lolote bila kujali itakuwaje ili wapate chakula, wasife njaa. 

Yote hayo na mengine mengi huchangia mimba, unyanyasaji na watoto kutumiwa vibaya wakati huu wa likizo lakini pia wakiendelea kujifunza.

Ni vyema wazazi, walezi na wadau wa elimu watatue matatizo hayo yanayohusisha chakula na ulinzi ili kupunguza matatizo hasa kuwaumiza watoto ambao mara nyingi hawana hatia.

Usalama na ulinzi wa watoto unakwenda mbali zaidi kwa kuwasimamia na kuwaepusha na athari za utandawazi ni kwa sababu umewaharibu wawe wa msingi na  sekondari   kwa vile wakati huu wa likizo wanaweza kutumia muda mwingi kuangalia mitandaoni kujifunza‘maovu.’

Wapo wenye  simu janja  na kompyuta wanaozitumia kuangalia maovu mitandaoni kama picha za ngono kwenye YouTube zenye maudhui yasiyo na maadili.

Wanajifunza masuala mengine makubwa kuliko mri wao, wapo wanaojifunza na kufanya uhalifu, kutumia dawa za kulevya, kuua na hata kudanganya.

Utandawazi unawatumbukiza katika kupenda muziki wa disko usiku na kuchochea watoroke nyumbani.

Wapo wengine kwa kuzoea maovu ya mitandaoni wanakimbilia kwenye sinema zinazoonyeshwa kwenye vibanda umiza mitaani.

Watoto hawa wanapokosa uangalizi wanaweza kuishi kwenye nyumba za sinema mchana au vibanda umiza, mabinti wanaweza kuzamia huko wakawa  waathirika wa unyanyasaji kwenye likizo.

Ikumbukwe kuwa kama familia na jamii hazitawajali watoto wakati huu wa likizo wengi wanaweza kushawishiwa na kutumbukia kwenye vitendo vya kuwakwamisha kimasomo.

Watoto wanaingia mitegoni wanapokwenda kwenye mabanda yanakoonyeshwa video asubuhi na mchana na kukutana na  watu wanaowalipia kiingilio, kuwapa chips na soda kitakachofuata ni ulaghai na hadaa zinazoweza kuwaondoa shuleni kwa sababu za unyanyasaji kijinsia.

Pamoja udanganyifu huo wakati mabinti wanaweza kuingizwa mtegoni na walimu ambao ama kwa kisingizio cha kuwafundisha ‘twisheni au pre form one’ wanawabaka au kuwashawishi kuingia kwenye ngono.

Ni vyema kuwaangalia watoto wasiwe waathirika wa kutafuta fedha za kujikimu kwa kulazimishwa kufanyakazi za kuosha vyombo, kutafuta kuni , kufua nyumbani kwa walimu na  watu wengine iwe mijini au vijijini. 

Wazazi na wanafamilia walindeni watoto wasichwe au kusafirishwa kwenda kwa jamaa zenu mikoani kwa mjomba, baba mkubwa au bibi na babu kwa sababu huko nako si salama.

Kaeni na watoto wenu likizo maana hasara za kuwapeleka mbali na familia ni kubwa zaidi kuliko mnavyowaza.