Wabunge wataka manufaa zaidi ufanisi wa bandari

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:09 PM Dec 04 2024
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza.

WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, wamepongeza ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam, na kutaka wananchi wanufaike na uondoshaji wa haraka wa mizigo bandarini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza, amesema kiu ya wabunge na Watanzania, ni kuona gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka nje ya nchi zinapungua, kwa kuwa muda wa meli kusubiri kuingia nangani, umepungua kutoka siku 21 hadi siku tano.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam leo Desemba 04, 2024 wakati wajumbe wa kamati hiyo walipotembelea bandari ya Dar es Salaam.

Naye, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TPA), Yusuf Mwenda, amesema wanataka bandari ya Dar es Salaam iwe mshindani katika kuhudumia nchi za maziwa makuu, akisema lengo ni kufika siku moja.

“Hata walizofikia hapa bado, tunataka zipungue zaidi. Tukipunguza muda wa kuondosha mizigo, tutawavutia wengine waje wapitishe mizigo kwetu. Tunataka tusiwe na meli hata moja inayosubiri,” amesema.

Mwenda amesema hivi sasa meli zinazosubiri kuingia nangani zimepungua hadi saba kutoka 30; na kwamba lengo ni kuhakikisha kila meli inapofika inatia nanga na kushusha mzigo.

“Zikienda hivi, sisi TRA tutakusanya fedha nyingi sana. Tutakusanya kupitia forodha na tutapata kodi nyingi za ndani kutokana na mizigo inayouzwa na wafanyabiashara,” amesema.

Amesema kinachopaswa kufanywa ni kuongeza magati hadi 14, ili bandari iweze kuhudumia meli nyingi zaidi kwa mara moja.

Mkuu wa Uhusiano kwa umma, kampuni ya Adan inayohudumia gati namba nane hadi 11, Donald Talawa, amewaambia wabunge kuwa wamejipanga kuhudumia makasha 77,000 mwezi huu, kutoka 73,000 mwezi uliopita.

Amesema mfumo wa kampuni hiyo wa kuhudumia makasha unasomana na wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na TRA, ili kuhakikisha serikali inapata tozo na kodi stahiki.

Mwakilishi wa kampuni ya DP World, Elitunu Mallamia, amesema uwekezaji wa vifaa na mfumo, umeongeza ufanisi katika kupakua na kupakia shehena melini.

Amesema kwenye gati namba sifuri inayohudumia magari, meli hazisubiri kwa kuwa inafika na kutia nanga.

“Meli za magari hazisubiri kabisa. Zinapowasili zinaingia moja kwa moja kuhudumiwa. Tumeboresha kasi ya ushushaji wa magari hadi kufikia pungufu ya saa 48 kwa meli. Imetuwezesha kuhudumia magari 17,000 kutoka wastani wa magari 14,000 kwa mwezi,” amesema.