SHUJAA LAWI SIJAONA: Mpigania uhuru aliyemkaribisha Mwalimu Nyerere kwenye vyama

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:15 AM Dec 10 2024
Shujaa Lawi Sijaona.
Picha:Mtandao
Shujaa Lawi Sijaona.

YAWEZEKANA ni jina geni kwa baadhi ya watu hasa wa kizazi kipya. Lakini, ukweli unabaki miongoni mwa wapigania uhuru wa Tanganyika kuwa ndiye aliyemkaribisha Baba wa Taifa, Julius Nyerere kulala nyumbani kwake na kupanga mikakati ya kusaka uhuru.

Ndiye mzalendo  ambaye kwa heshima yake, leo anaenziwa katika Uwanja wa Soka uliopo mjini Mtwara kupewa jina lake la Nangwanda Sijaona.  

Itakumbukwa kuwa mwaka 1955, Nyerere alitembelea jimbo la Kusini na kufika Newala nyumbani kwa Sijaona, alikolala wakashirikiana kupanga mipango ya kuikomboa Tanganyika.
 
 Ni mwaka huo ambao Sijaona alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa TANU wilayani Newala, kisha mwaka mmoja baadaye, akachaguliwa Mwenyekiti wa TANU jimbo la Kusini, ndipo akalazimika kuhamia Lindi kulikokuwa makao makuu ya jimbo.
 
 Kuchaguliwa kwake kushika nafasi hizo, kulitokana na umahiri na ujasiri wa kuunga mkono kazi ya kupigania uhuru wa Tanganyika, hata akaamua kuacha kazi serikalini, kujiunga na TANU.

 Mpigania uhuru huyo alifariki Januari 28, 2005, kama angekuwa hai, angekuwa na miaka 96, ameacha  historia ya kulifanyia taifa mambo makubwa.

 Anapotajwa kisiasa, ndiye miongoni mwa waasisi wa vyama vya siasa vya ukombozi akianzisha Tanganyika African Association (TAA), baadaye TANU na hatimaye CCM.

Mzizi wa nyota ya uongozi wake, ulianza kung'aa masomoni Minaki, aliposoma sekondari,  ikielezwa kuwa alikuwa na  nidhamu na unadhifu mkubwa ,  hapo aliteuliwa kuwa msaidizi wa kiranja mkuu akisimamia chakula.

Pamoja na jukumu hilo alikuwa  mwandishi wa makala, barua nyingi, hata majarida na magazeti yanayohusu mambo ya siasa, licha ya kupigwa marufuku na serikali ya kikoloni.
 
Baadaye mwaka 1952, alipomaliza kidato cha sita, alianza  kazi ya uandishi wa habari Ofisi ya Sekretari Mkuu, Idara ya Uhusiano wa Umma, akiwa mhariri wa gazeti la kila  siku la ‘Habari za Leo.’

Ni kazi aliyofanya kwa miaka miwili hadi 1954, alipoacha na kwenda kuwa Mtendaji Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya Newala, kwa muda wa mwaka mmoja.

Sijaona aliyezaliwa Novemba 24, 1928, kijijini Mnyambe wilayani Newala mkoani Mtwara, katika familia ya wazazi wakulima alipata elimu katika shule ya Msingi Utende kuanzia mwaka 1937. 

Baada ya hapo, akahitimu darasa la nne mwaka 1942 alikofaulu na kuendelea na masomo ya darasa la tano hadi la nane, akiwa katika Chuo cha Mtakatifu Joseph, kilichoko Chidya Masasi.

Safari yake ya masomo ngazi ya juu sekondari, kidato cha tatu hadi sita alikuwa katika shule ya Mtakatifu Andrea, Minaki, Kisarawe mkoani Pwani, alikohitimu mwaka 1951. Baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Makerere,  nchini Uganda kwa masomo ya juu chuoni.

 HARAKATI  ZAIDI  

Licha ya kufanya kazi serikalini, Sijaona alijiunga na siasa za  TAA,  akipewa kadi namba 204. Kikubwa kinachotajwa kuvuta upenzi wake ni haki za kitaifa kwa wananchi wenzake, hatua aliyofanya kwa siri. 

Ikumbukwe serikali ya kikoloni wakati huo, liwazuia watumishi wake kujiingiza kwenye siasa, lakini akaifanya kwa siri, ikiwamo kumkaribisha Mwalimu Nyerere, aliyekuwa akianza harakati za ukombozi. 
 
Historia yake zaidi inaonesha, mwanasiasa huyo aliishi Lindi akifanya kazi za TANU bila malipo, vilevile akishika wadhifa wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU, baadaye katika harakati hizo alienda kikazi India.
 
 Inaelezwa, wakati wa kurejea nyumbani ndege ilitua katika uwanja wa Nairobi, Kenya, akashikiliwa kwa saa tatu na askari kanzu wa wakoloni, ingawa kosa lake halikuelezwa. 

Kilikuwa kipindi India ilipata Uhuru Agosti 1947, kisha ikaunga mkono nchi nyingi za Kiafrika kusaka uhuru, ikiwamo kutoa nafasi nyingi za kielimu kwa Waafrika wakasome, ili wawe na utashi na uwezo wa kujikomboa. Tanzania, mnufaika mmojawapo ni Waziri Mkuu mstaafu John Malecela.

Mwaka 1958 harakati za siasa za TANU kuikomboa Tanganyika zikipamba moto, ulifanyika uchaguzi wa kwanza wa serikali za mitaa na mkongwe Sijaona, akajitosa na kuchaguliwa diwani, pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Lindi.
 
 Ni ushindi uliomfanya kuweka historia  kwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza Mwafrika wa  Halmashauri za Miji Afrika Mashariki.
 
 Aidha, nyota yake ilizidi kuwaka, mwaka 1959 kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu (ulihusu Mzungu, Mhindi na Mwafrika), Sijaona aliteuliwa na TANU kuwakilisha jimbo la Kusini, alikochaguliwa bila kupingwa. 
 Haikuchukua muda mrefu, mwaka 1960 akachaguliwa mbunge wa Wilaya ya Lindi. 

Katika uchaguzi wa mwaka 1965, Sijaona alirudi kwao Newala kuwania ubunge na kushinda kwa kishindo, ilipofika 1970, awania tena nafasi hiyo, akashinda bila kupingwa katika jimbo hilo.

 UONGOZI SERIKALINI 

Mwaka 1961 baada ya Uhuru , aliteuliwa Naibu Waziri Serikali za Mitaa na Tawala za Majimbo na 1962, alikahamishwa kuwa Wizara ya Fedha, baadaye  Waziri wa Mila za Taifa na Uongozi wa Vijana. 

Ilipofika mwaka 1964 wakati wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akawa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais. 
 
 Umahiri  kikazini  ulimfanya ahamishwe katika wizara mbalimbali, zikiwamo  Ardhi, Maji na Makazi; Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais na Afya na Ustawi wa Jamii.
 
 Mwaka 1972, serikali ilipofuta Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuanzisha mfumo wa Madaraka Mikoani (iliyodumu hadi 1982), ukilenga kupeleka mamlaka za serikali ngazi za msingi kuanzia mkoa mpaka vijiji, Sijaona akawa Mkuu wa Mkoa wa Ziwa Magharibi (sasa Kagera), akiongoza kwa miezi sita.
 
 Ndani ya kipindi hicho, Sijaona akapelekwa mkoa wa Mwanza, alikodumu hadi mwaka 1976, akahamishiwa kwa nafasi hiyo kuongoza mkoa wa Kilimanjaro hadi 1980, akahamishiwa kwa kazi hiyo mkoani Mtwara. 

Ilipofika 1983, akiwa na miaka 55 aliomba kustaafu, hata akarejea maisha ya ukulima, lakini kwa uwezo wake wa uongozi, aliteuliwa mbunge hadi lilipovunjwa mwaka 1985.

 NDANI YA CHAMA

Historia inaonyesha kuwa mwaka 1956 aliiwakilisha TANU katika mkutano wa Asian Socialist Conference, uliofanyika Bombay nchini India.
 
 1959 akawa Mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU, pia  Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa TANU, kadhalika, mjumbe wa Tume ya Kuangalia Muundo wa Serikali ya Tanganyika, baada ya uhuru.

Baadaye mwaka 1961, akateuliwa kuwa mjumbe wa Mkutano wa Katiba, ilipofika 1962 wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Fedha, alikuwa Mwakilishi wa Serikali ya Tanganyika katika Kamati ya Nchi 11 ya Kiuchumi, Afrika.
 
 Inaelezwa kwamba alikuwa na jukumu la kushauriana na serikali za Afrika kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Afrika.  

Mwaka 1976, Sijaona alichaguliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Watu 20 iliyoandaa katiba ya CCM, iliyoteuliwa na Rais Nyerere, kuandaa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
 Kwa ujumla, Sijaona ana rekodi ya kufanya kazi zilizotukuka wakati taifa likisherehekea miaka 63 ya uhuru.