Waziri Ulega aagiza ongezeko bajeti ya madawati

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:33 PM Jan 10 2025
Waziri Ulega aagiza ongezeko bajeti ya madawati.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Ulega aagiza ongezeko bajeti ya madawati.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kuhakikisha bajeti ya madawati inafikia shilingi bilioni moja katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili kukidhi mahitaji ya shule za msingi na sekondari wilayani humo.

Ulega, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, ametoa maelekezo hayo Januari 10 wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 3,000 yaliyonunuliwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya wilaya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ulega amesema bajeti inayotengwa kwa ajili ya madawati bado ni ndogo na haikidhi mahitaji, hasa kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya wanafunzi.

"Wilaya yetu ina vyanzo vizuri vya mapato, haipendezi kuona bado kuna wanafunzi wanaokaa chini. Bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya madawati lazima iongezeke kutoka shilingi milioni 300 za awamu iliyopita na kufikia bilioni moja au zaidi," amesema Ulega.

Waziri huyo pia amebainisha kuwa Wilaya ya Mkuranga inaongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi katika Mkoa wa Pwani. Kwa msingi huo, amesema atakutana na Waziri wa TAMISEMI ili kujadili ongezeko la walimu wilayani humo ili idadi yao iendane na wingi wa wanafunzi waliopo.

1

“Kwa sasa, idadi ya wanafunzi ni kubwa ukilinganisha na walimu waliopo. Hali hii inawafanya walimu kushindwa kuwafuatilia wanafunzi kwa ukaribu na kudhibiti mienendo yao,” ameongeza.

Aidha, Waziri Ulega amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo serikali yake imekuwa ikiidhinisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayosaidia kutatua changamoto za wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasri, amepongeza Waziri Ulega kwa jitihada zake za kuisemea Wilaya hiyo bungeni, hatua iliyosaidia kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi.

Afisa Elimu wa Msingi wa Wilaya hiyo, Jessy Mpangala, amesema uhaba wa madawati shuleni umetokana na ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa kila mwaka, hali inayohitaji juhudi za ziada kuboresha miundombinu ya elimu.

2