Tanga yakusanya bilioni 5.3 uuzaji Hatifungani ya Miundombinu

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 05:59 PM Jan 10 2025
Meneja wa CRDB Mkoa wa Tanga, John Mtani.
Picha:Mpigapicha Wetu
Meneja wa CRDB Mkoa wa Tanga, John Mtani.

Mkoa wa Tanga umekusanya shilingi bilioni 5.3, sawa na asilimia 25 ya lengo, kupitia zoezi la uuzaji wa Hatifungani ya Miundombinu (Samia Infrastructure Bond).

Zoezi hili linaendeshwa kwa ushirikiano wa Benki ya CRDB na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Tanga.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mauzo ya hatifungani hiyo, Meneja wa CRDB Mkoa wa Tanga, John Mtani, ambaye alimwakilisha Meneja wa Biashara Kanda ya Kaskazini, David Peter, amesema hatifungani hiyo imelenga kutatua changamoto za kifedha zinazozikabili taasisi katika utekelezaji wa miradi ya barabara.

"Hatifungani hii tumeanza kuiuza tangu Novemba 29, na tutaendelea hadi Januari 17 mwaka huu. Tukiondoa siku za mapumziko, tunabaki na siku tano kukamilisha zoezi hili. Hata hivyo, hatifungani hii itaorodheshwa kwenye soko la mitaji Februari 10 na itakuwa na muda wa miaka mitano hadi Februari 10, 2030," amesema Mtani.

Aidha, Mtani ameeleza faida zinazopatikana kwa mwekezaji anayenunua hatifungani hiyo, ikiwa ni pamoja na malipo ya gawio la asilimia 12 yatakayofanyika mara nne kwa mwaka.

Amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo jirani kushiriki katika kununua hatifungani hiyo kabla ya tarehe ya mwisho, akisema ni fursa muhimu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya barabara.

Zoezi hili limeonekana kuwa hatua muhimu ya kukuza mtaji wa ndani kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta ya barabara nchini.