ISHARA ya mwaka kufika ukingoni ni maadhimsho ya Sikukuu ya Krismasi, ambayo kiutamaduni huunganishwa na mwaka mpya, kwani tofauti zao ni mwaka mmoja tu. Hapana shaka hilo limeshatimu kwa 2024!
Kipindi kilichoko huendana na matukio maalum, ikiwamo mapumziko ya mwisho wa mwaka na baadhi yetu nao huchukua likizo kipindi hicho.
Ingawa nchini likizo hiyo haipo rasmi kisheria, lakini kisera ofisi nyingi na hasa za kimataifa, watu huenda kupumzika na baadhi ya wafanyakazi, hupenda kwenda katika mapumziko mafupi.
Pia, nchini kuna baadhi ya jamii kama za mkoa wa Kilimanjaro, watu huenda nyumbani, huku watani wao wakiwadhihaki ‘wanaenda kuhesabiwa.’
Huko makwao wanapumzika, kujumuika kijamii na wanaburudika kadri wanavyoweza. Zao lake, kuna jambo kiafya; watu wanaongezeka uzito na imekuwa jambo la kawaida kwa watu wazima wengi.
Kisaikolojia, likizo mbalimbali za msimu zinaweza kushawishi ulaji kupita kiasi, tabia ya kukaa tu na ulaji wa vyakula vyenye kalori nyingi.
Hapo kuna vidokezo kadhaa vya kusaidia kuepuka kuongezeka uzito, wakati wa msimu huo wa likizo.
Uchunguzi unaonesha kwamba, watu wanaokula bila kuzingatia kanuni na miongozo ya lishe, wana uwezekano mkubwa wa kula kupita kiasi na kupata athari katika miili yao.
MBINU STAHIKI
Ili kuzuia hali hiyo, inaelezwa mtu ale kwa uangalifu na kupunguza vikwazo, ikiwa ni pamoja na kazi na vifaa vya elektroniki.
Jaribu kutafuna polepole na vizuri, hali inayomwezesha mlaji kutumia kalori kidogo, vilevile mtu anatakiwa kuvuta pumzi kidogo kabla ya kuanza kula.
Ni hali inayotajwa kuleta utulivu wakati wa kula, ikisaidia kuweka mawazo kamili kwenye sahani, badala ya orodha yako ya mambo mengi ya kufanya.
Tafiti kadhaa zinaonesha kuwa wanaojihusisha na mazoea ya kula, kwa uangalifu wana uwezekano mdogo wa kupata uzito mkubwa.
MLO WA PROTINI
Milo ya likizo kwa kawaida huwa na wanga nyingi lakini ina protini kidogo.
Hata hivyo, ni muhimu kujumuisha protini kwa kila mlo, kwa kuwa inakuza utimilifu na inaweza kuwa muhimu kwa kudumisha uzito.
Ulaji protini na milo mingine, unatajwa kupunguza ulaji wa kalori kwa kupunguza njaa na hamu ya kula.
Protini, pia inatajwa manufaa yake katika kudhibiti uzito, kwa sababu inaongeza tindikali ya metaboliki yako na viwango vya homoni zinazopunguza hamu ya kula.
Vyanzo vya protini ni pamoja na nyama, kuku, samaki, na baadhi ya vyakula vya mimea kama maharage.
VYAKULA VYA NYUZI
Vyakula vyenye nyuzi, vinatajwa katika utaalamu lishe ni kirutubisho muhimu kuchangia shibe ya mlaji.
Baadhi ya tafiti zinaonesha kwamba, ulaji vyakula vya nyuzi, unasadia kupunguza ulaji kalori kwa ujumla, hali inayosaidia kuzuia kuongezeka uzito wakati wa likizo.
Ni bahati mbaya vinatajwa vyakula vingi vya kawaida nyakati za likizo havina kiasi cha kutosha cha nyuzi.
Watu wanashauriwa kujitahidi kula vyakula vyenye nyuzi nyingi, kama vile mboga, matunda, kunde, nafaka zisizokobolewa, karanga na mbegu.
Watu wengi hutumia muda mrefu kupika wakiwa likizo, hali inayosababisha kuongezeka uzito, kwa sababu ni rahisi kuonja au kujaribu.
Kuonja chakula chako inaweza kuwa muhimu, hasa ikiwa unawapikia wengine, lakini kumega kidogo kidogo kunaweza kuwa zaidi ya kiasi.
Mlaji anapaswa pia kuhakikisha, hana njaa wakati wa kupika, kwani ni rahisi akawa mwonjaji ladha kupitiliza.
DHIBITI KITIMDAMLO (DESSERT)
Katika safu ya mlo, kuna kinachoitwa kitaalamu kwa jina ‘dessert’. Hiyo ni ladha fulani inayokamilisha mlo, mfano kwa mchana na mara nyingi huwa jamii ya sukari, mathalan ‘icer cream’, juisi au soda.
Wakati wa likizo kama sasa kwa wengi, hiyo inashauriwa kuepukwa au kupunguzwa kadri inavyowezekana, kwani ina mchango wa kutumia sukari ya ziada, ikiendana na kuongezeka uzito mwilini.
Pia, unatajwa mbadala wa kula taratibu, unaomfanya mtu ahisi kisaikolojia anaridhika zaidi na kuna uwezekano mdogo wa kuzidisha ulaji wake.
KUTUMIA SAHANI NDOGO
Karamu zenye chakula cha jioni, zimekuwa za kawaida wakati wa likizo sehemu nyingi, zikiwaleta pamoja ndugu, jamaa, marafiki.
Ni sherehe anayotakiwa mtu fursa kutumia sahani ndogo, inayomsaidia binadamu kiafya. Kinyume chake ni kwamba, mtu anapokula kikubwa, kwa hamasa ya sahani yake kubwa, inaweza kusababisha kula kupita kiasi.
Kwa hivyo, sahani ndogo ni njia rahisi ya kudhibiti kiasi cha chakula au mlo wako.
EPUKA VILIVYOSINDIKWA
Vyakula vilivyochakatwa wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka, kama vile viazi kwenye mikebe huwa havifai sana.
Vyakula hivyo mara nyingi huwa na sukari nyingi na mafuta yasiyofaa, yenye mchango kuathiri uzito wa asili wa binadamu.
Ili kuzuia kuongezeka uzito, mtu anashauriwa kuchagua chakula na apike, kwa hatua zote. Kwa njia hiyo, kuna mchango wa kufuatilia, hata kudhibiti uzito binafsi.
Pia, inashauriwa kwamba, kunapokuwapo nia ya dhati ya kudhibiti uzito huo, inawezekana ikasaidia kujiwekea mipaka na kushikamana na malengo yako kuhusu ulaji bora wa chakula.
Mara nyingi, watu huacha malengo yao baada ya hali hii kutokea. Hata hivyo, ni bora kuendelea na kufanya chaguo bora zaidi wakati ujao unapokula.
Ingawa kuyasimamia malengo yako ya uzani kunaweza kuchosha wakati wa msimu wa likizo, vidokezo na njia nyingi zinaweza kusaidia kuwa na afya njema, furaha, na kuzingatia uzito wakati huu wa mwisho wa mwaka.
Zaidi ya vidokezo vya jumla vya lishe, ni bora mtu akahakikisha anafanya mazoezi ya kutosha kupunguza ulaji vyakula visivyofaa.
Ikiwa ana bidii, anaweza kubaini kwamba hajazuia tu kuongeza uzito bali hata kuupunguza uzito wakati wa msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
BBC
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED