Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi amewakumbusha watumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ushirikiano, upendo, furaha na amani ili kuyafikia malengo ya ofisi hiyo.
Dk. Yonazi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi Ofisi yake wakati wa mkutano wake na watumishi hao uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo Njedengwa Jijini Dodoma tarehe 04 Februari, 2025.
Dk. Yonazi amesema ipo haja ya kila mtumishi kujifanyia tathmini katika utendaji wakewa kazi huku akizingatia miongozo na kanuni za utumishi wa umma na kusema kuwa, kila mtumishi anawajibika katika kuhakikisha ofisi inapata matokeo iliyoyakusudia na kwa ufanisi.
“Ni wakati sahihi kila mmoja kuilinda furaha aliyonayo awapo mahali pa kazi, isingefaa utoke nyumbani huna furaha na ufike eneo la kazi ukose furaha, ni vyema kuja eneo la kazi na kuipate furaha mara mbili kwa kuzingatia mazingira yaliyorafiki katika kutekeleza majukumu,” alisema Dk. Yonazi
Aliongezea kuwa kila mtumishi wa umma awe na desturi ya kuheshimu nafasi ya mwingine bila kujali tofauti zinazoweza kuwepo miongoni mwa watumishi hao.
“ Ni vyema kila mtu akajali mwingine na ikumbukwe hakuna mtu mwenye uwezo mdogo wa kufanya kazi, jambo la msingi ni kuhakikisha ule uwezo uliopewa na Mwenyezi Mungu na Mafunzo mbalimbali unatumia vizuri na kuhakikisha uleta matunda mazuri na kuleta maendeleo kwa Nchi yetu” alisema Dk. Yonazi.
Sambamba na hilo aliwaeleza watumishi hao kuwa kila mmoja ni kiongozi katika eneo lake la kazi hivyo abebe dhamana hiyo kwa weledi na ufanisi mkubwa.
“.....kila mtumishi aliyepo hapa ndiye Katibu Mkuu kwenye eneo lake, kwa kubeba imani ya kwamba ni Katibu Mkuu anapaswa kuwa na nidhamu na bidii katika kazi ikiwa ni pamoja na kuwa mwaminifu,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dk. James Kilabuko katika neno lake la utangulizi amewaasa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuzingatia sheria za utumishi wa Umma huku akiwasihi kuimarisha umoja na mshikamano ili kuiletea Serikali maendeleo yake.
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Waziri Mkuu, Numpe Mwambenja ameomba watumishi kuendelea kujitathimini mienendo yao katika utumishi wa Umma kwa kufanya kazi vizuri na nidhamu na kuheshimu viongozi huku wakiheshimiana wao kwa wao.
Numpe alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna unavyojali maslahi ya watumishi na ustawi wao kwa ujumla na kuwasihii watumishi kuendelea kutimiza wajibu kwa kuzingatia kauli ya “hakuna haki bila wajibu”.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED