Mwenyekiti wa CCM Tanga achangia madawati Shule ya Sekondari Mgwashi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:39 AM Feb 04 2025
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu, Rajabu Abdulrahaman.

Katika kusherehekea miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu, Rajabu Abdulrahaman, ametembelea katika Shule ya Sekondari Mgwashi iliyopo Korogwe Vijijini Kata ya Mngwashi na kutoa mchango wa shilingi milioni saba (7,000,000) kwa ajili ya kununua madawati 100.

Naye Mbunge wa jimbo hilo, Timotheo Mzava, alichangia shilingi milioni saba (7,000,000) ili kukamilisha ununuzi wa madawati mengine 100. 

Mwenyekiti Abdulrahaman alisisitiza kuwa CCM inatekeleza kwa vitendo kutatua changamoto za wananchi, huku akiwataka viongozi wa vyama vingine kuacha malalamiko na badala yake wachukue hatua stahiki.

Kuhusu kero ya ucheleweshaji wa ujenzi wa zahanati, Mwenyekiti Rajabu ametoa maagizo kwa uongozi wa halmashauri kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 1 Aprili 2025, zahanati hiyo iwe imeanza kutoa huduma kwa wananchi.

1

Alieleza kuwa licha ya wananchi kushiriki katika kuchangia ujenzi huo, serikali tayari imetoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo. Hata hivyo, alieleza kusikitishwa na hali ya mradi kutokukamilika kwa muda mrefu na akaonya kuwa wale waliotumia vibaya fedha hizo watachukuliwa hatua kali.

"Hapa kuna tatizo... Serikali imetoa shilingi milioni 50, lakini bado jengo halijakamilika, licha ya wananchi pia kuchangia. Wanaohusika na upotevu wa fedha hizi watawajibishwa," alisema Mwenyekiti Rajabu Abdulrahaman Abdallah.

2