WADAU wa afya nchini wametaja makundi yatakayoathirika na uamuzi wa kusitishwa ufadhili wa miradi ya afya, ukiwamo wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR), ni wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.
Wengine ni waraibu wa dawa za kulevya pamoja na kudorora kwa uchumi wa sekta binafsi, kutokana na kundi kubwa kuajiriwa na taasisi na asasi zilizotegemea misaada hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Kituo cha Life and Hope Sober House (LHRO), Al-Karim Bhanji, amesema tangu Oktoba, 2024, walianza kutekeleza kuwaibua waraibu wa dawa za kulevya, kuwapeleka kliniki za methadone, kupima VVU, Kifua Kikuu (TB) na kuanza dawa, mradi ambao ungekamilika Septemba, mwaka huu.
“Sisi LHRO, kwa mradi tulioyoitekeleza upande wa Dar es Salaam, tuliyofanya na MDH na Bagamoyo THPS imetuathiri, kwa sababu tulikuwa katika mkataba mpya ambao ulianza mwezi wa 10, 2024.
“Kusitishiwa ina maana wafanyakazi wote pamoja na mimi mwenyewe mkurugenzi. Unakuta hatuwezi kwenda kuibua waraibu wapya kwenye maskani, ili tuwapeleke katika kliniki za ‘methadone’.
Alisema hatua hiyo imekuja ghafla kabla ya taasisi hizo kujiandaa na kwamba ipo haja ya uamuzi kama huo kufikiriwa mara mbili hasa mfadhili ambaye ni Marekani, pamoja na serikali za nchi husika.
“Kuna wenzetu ambao wanakunywa dawa za ARVs, hatujui hatima itakuwaje, ijapokuwa wamesema watatoa nafuu. Vilevile tunaamshwa kwamba kuwa na mpango B kuwa na vyanzo vya mapato kwa masuala haya, ili kupata ufadhili kutoka ndani, tukopeshwe, tuendelee na kazi tuliyoianza,” alisema.
Paul Makuri, mdau wa afya, alisema eneo la huduma za afya mfadhili mkubwa ni PEPFAR, kwa ajili ya VVU, TB na Malaria katika utoaji wa dawa, huduma za upimaji na ufuatiliaji wa wagonjwa pamoja na kufanyika utafiti.
“Akisimamisha msaada huduma zitasimama hasa za kitaalamu, ili watu wafikiwe, sasa zitapatikana huduma kwa gharama kubwa, ambazo wengi hawatamudu.
“Ajira pia zitaathirika kutokana na wengi wamejiriwa kutoa huduma kwenye hii miradi, kama vile wauguzi, wataalamu wa afya na wamekuwa wakilipwa mishahara kupitia hiyo miradi.
“Watu wenye VVU wako milioni 1.5 nchini, wanahudumiwa na kupatiwa dawa. Pia kuna watu wameajiriwa kutafuta ambao wanapotea katika orodha ya kutumia dawa, wanawafuatilia kujua wako wapi, wanaendeleaje. Hata waliokuwa kwenye dawa wanajulishwa, wanaowajulisha watashindwa kufanya kazi,” alieleza.
Aliongeza kwamba watoa huduma za Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa (CDC), wameathiriwa pia kutokana na kusimamishwa kwa sababu fedha zilizotegemewa kutoka Marekani.
Neema Khalid kutoka Shirika la Wanawake Wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Tanzania (DWWT), alisema kuzuia utoaji wa fedha kwa eneo la VVU na TB kunaathari kwa nchi na watu, hasa katika nchi zinazoendelea ambazo hutegemea msaada wa kimataifa kwa huduma za afya.
“Baadhi ya athari kuu ni kupungua kwa huduma za afya, vituo vya afya kupungukiwa na rasilimali za msingi, kama dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs), matibabu ya kifua kikuu (TB), vipimo na vifaa vya kinga.
“Wagonjwa wanaweza kukosa huduma za mara kwa mara, na hii inaweza kusababisha kuzorota kwa hali zao za kiafya; kuongezeka kwa vifo; kukosekana kwa dawa na huduma za kuzuia maambukizi mapya kunaweza kusababisha vifo vya watu wanaoishi na HIV au TB, hasa wale walioko katika hatua za mwisho za ugonjwa.
“Kuvurugika kwa programu za kuzuia VVU na TB hutegemea ufadhili wa nje. Kuzuia fedha kutasababisha programu hizi kusimama na hii inaweza kuvunja maendeleo yaliyofikiwa katika miaka iliyopita.
“Kwa ujumla, hatua kama hii inaweza kurudisha nyuma mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupambana na HIV na TB na kusababisha madhara makubwa kwa watu.”
TAMKO RASMI
Tamko rasmi la kusitishwa kwa shughuli zote zilizo chini ya PEPFAR/CDC katika miradi ya Afya Hatua, lilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS), Dk. Redempta Mbatia.
Pamoja na huduma za maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ikijumuisha na matibabu ya VVU, ushauri, kinga na tiba ya magonjwa nyemelezi ikijumuisha TB.
Akifafanua zaidi katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu THPS, Dk. Redempta, ulisaidia kuwapo maafikiano na Hospitali za Rufani za Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, rasilimali watu 1,465 katika halmashauri 34, sampuli za usaidizi na kutoa usafiri kwa vituo vya afya 364.
Alisema kuwa mradi wa Afya Hatua (2021-2026), umekuwa ukiiunga mkono serikali katika juhudi za kufikia udhibiti wa janga la UKIMWI, kwa kusaidia huduma za kinga, matunzo na matibabu katika jamii katika mikoa ya Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga, huduma maalum za kinga dhidi ya VVU katika vituo mbalimbali.
Alisema kwamba mradi ulisaidia matibabu ya methadone kwenye kliniki za MAT Pwani na Tanga, pia ulisaidia tohara ya hiari kwa wanaume (VMMC) katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga.
Kwa mujibu wa Shirika la Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS), nchi za Botswana, Eswatini, Rwanda, Tanzania na , Eswatini, Rwanda, zimefikia lengo la '95-95-95'.
Nchi zingine 16 zinakaribia kufikia lengo hilo, zikiwamo nane zaidi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED