Vifurushi vipya NHIF vyapokewa kwa hisia tofauti

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:53 AM Feb 04 2025
Mkurugenzi Mkuu Dk. Irene Isaka.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu Dk. Irene Isaka.

VIFURUSHI vipya vya matibabu vilivyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) vimepokewa kwa hisia tofauti mitaani, baadhi ya wananchi wakidai ni ghali kwao.

Wamiliki wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya wamesema hawana shida na vifurushi hivyo vipya, wakishauri mfuko utoe elimu kwa wanachama wake kuhusu vifurushi hivyo. 

Mwenyekiti wa Umoja wa Vituo Binafsi vya Utoaji Huduma za Afya Tanzania (APHFTA), Dk. Egina Francis, alisema hawana tatizo na vifurushi hivyo vipya, akishauri NHIF kutoa elimu kwa wateja wake ili kupunguza lawama ambazo zinaweza kujitokeza wanapokwenda hospitalini kutibiwa.

Alisema wanachotaka ni kuhakikisha vivurushi hivyo vipya vinawekwa katika mfumo ili mgonjwa anapokwenda hospitalini asihangaike.

Kukiwa na mapokeo hayo ya wadau hao, baadhi ya wananchi waliozungumza kwa nyakati tofauti jana na mwandishi wa habari hi, walidai kuwa kwa namna gharama za matibabu zinavyopanda nchini, kuna hatari kubwa baadhi ya watu wakaamua kutafuta mbadala wa matibabu, ikiwamo kukimbilia kwa sangoma.

"Hii hali ya kila siku vifurushi hivi kupanda kila siku inatisha... kuna wakati walitangaza ile inaitwa Bima ya Afya kwa Wote, tunafikiri kwamba huenda hii ikasaidia kuleta ahueni kidogo, lakini tunaona kama hali inazidi kuwa mbaya. Sasa NHIF wanatutangazia vivurushi vipya, tena gharama yake inazidi kupanda juu.

"Yaani ukiangalia hivi vya sasa ndio kama wanatuchanganya kabisa hadi unatamani kwamba angalau mara mia wangeacha kama vile vilivyokuwapo awali kuliko huku wanakoelekea... wanachotutafutia kwa sasa ni magonjwa ya akili," alidai Anna Joel, mamalishe katika eneo la kibiashara Mwenge, wilayani Kinondoni.

Christopher Thomas, mfanyabiashara wa nguo katika eneo hilo, alisema: "Vifurushi vipya vya NHIF vinamtupa mbali na matibabu mtu mwenye hali ya chini kwa sababu katika mazingira ya kawaida kati ya watanzania milioni 60, ni wachache wenye uwezo wa kupata milioni moja kila mwaka kwa ajili ya tiba.

"Yaani eti mwaka huu nitafute Sh. milioni moja au zaidi hata kama ni Sh. 500,000 halafu mwaka ukiisha nitafute tena nyingine nilipe tena, wakati hata kodi ya nyumba yenyewe ninahangaika nayo kwa tabu kuilipa. Ninaona wanataka tuwe tunajinywea miti shamba tu nyumbani ambayo hatujui hata kama inatibu au inatuua, hebu watuonee huruma.

"Tatizo ni kwamba wanaweka hivi viwango kwa kuwaangalia watu wenye vipato vyao, wakurugenzi, wabunge, watu wenye nafasi zao kubwa maofisini, wanasahau kwamba kuna sisi wa huku tunaodunduliza... wanasahau kwamba kuna mtu anauza karanga kutwa nzima hata kuipata hiyo Sh. 5,000 ni shida halafu eti huyo ndiye apate Sh. 200,000, 500,000 au Sh. milioni 1.5 au na zaidi kwa ajili ya matibabu yake yeye na watoto wake, hii inatisha sana," alilalama.

Judith Kimario, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika moja ya vyuo vikuu vilivyoko Dar es Salaam, alisema ameshangaa kuona katika vifurushi hivyo vipya, hata wazee kuanzia miaka 60 nao wanatakiwa kulipia.

"Nilijua kwamba sheria inasema wazee kuanzia umri huo wanatakiwa watibiwe bure, kwenye vivurushi hivi wanatakiwa walipie, sasa kundi hili wengi wao si ni wastaafu, hizo fedha zote wanazitoa wapi? 

"Mbona hii ni hatari, tunaomba vipitiwe upya na ikiwezekana watafute njia nyingine ya kurahisisha huduma za tiba kwa mtanzania, si kwa namna hii ya sasa," alidai Judith.

Mwanaharakati Alfred Mwaijonga alisema kuendelea kupanda kwa gharama za maisha pamoja na kutokuwa na uhakika wa matibabu kwa kukosa bima ya afya ni miongoni mwa vitu vinavyoowaongezea watu maradhi.

"Mnasema watu wanapata vichaa, haya yanasababishwa na mengi, mtu akigeuka huku vifurushi havishikiki, bado hajalipa pango la nyumba, mara sijui bili gani hujalipa, kwa nini usipate kichaa? 

"Mimi ningeshauri kwamba serikali iangalie upya namna ya kupanga vifurushi hivi kulingana na vipato vya watu wake ili kila mtanzania awe na uhakika wa matibabu.

"Mimi ninaamini wangetumia hata ule mfumo wa kuchangisha kwa lazima kila mtanzania mwenye simu wamkate hata Sh. 500 kwa mwezi ile fedha ingetosha sana kuwatibu watu wote tena bila tabu," alishauri Mwaijonga.

Vifurushi hivyo vipya ambavyo vimetangazwa na NHIF, viko katika makundi ya aina mbili; Serengeti Afya na Ngorongoro Afya. Kifurushi cha gharama ya chini ni Sh. 240,000 na cha juu ni Sh. 6,388,400.

Kwa mujibu NHIF, watoto wa kuanzia miaka 0-17, mmoja analipa Sh. 240,000 kwa kifurushi cha Ngorongoro na Sh. 660,000 kwa kifurushi cha Serengeti.