Usiku wa kuamkia Februari 4, 2024, muungano wa waasi wa Alliance Fleuve Congo (AFC) na M23, ambao umetwaa mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), umetangaza kusitisha mashambulizi kuelekea Kinshasa, makao makuu ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa yao, hatua hiyo inatokana na sababu za kibinadamu na utu, kufuatia vifo vya raia vinavyoendelea kutokea, huku wakilaumu serikali ya DRC kwa kutumia mashambulizi ya anga dhidi ya wananchi.
Baada ya kuutwaa mji wa Goma, wanamgambo hao wameonekana wakitembea mitaani, wakishirikiana na wakazi wa mji huo katika shughuli za kijamii. Hata hivyo, maswali yanaibuka: Je, baada ya uamuzi huo, M23 itaendelea kuudhibiti mji wa Goma? Tayari wameweka utawala wao na wameagiza shughuli za kijamii ziendelee kama kawaida. Au kuna mkakati mwingine unaopangwa na kundi hilo?
Baadhi ya raia wa DRC wanaamini kuwa serikali haipaswi kutegemea tangazo hilo la usitishwaji wa mapigano, kwani linaweza kuwa mtego wa kijeshi ili waasi hao wajipange upya na kushambulia miji mingine.
Kiongozi wa kisiasa wa muungano wa AFC/M23, Corneille Nangaa, amesisitiza kuwa wameutwaa mji wa Goma baada ya mapambano ya muda mrefu, na hawana mpango wa kuondoka. Aidha, amesema wamekuta mji huo ukiwa na hali duni ya miundombinu—bila maji, umeme, wala mawasiliano—na sasa wanapanga kurejesha huduma hizo huku wakijiandaa kuichukua nchi kutoka mikononi mwa Rais Félix Tshisekedi.
Mkazi wa Bukavu, Jean Claude, akizungumza na Sauti ya Amerika (VOA) jioni ya Februari 4, 2025, amesema usitishwaji wa mapigano ni hatua muhimu kwani itapunguza vifo na uharibifu wa miundombinu. Hata hivyo, ameonya kuwa serikali haipaswi kubweteka, kwani waasi hao wanaweza kutumia muda huo kuzunguka milima na kutwaa miji mingine.
Mkazi mwingine wa Bukavu, Mubalama Benjamine, ameongeza kuwa kuchukulia tangazo la waasi kwa uzito kunaweza kuwa mtego mkubwa kwa serikali, kwani M23 inaweza kutumia mbinu za kuizingira Bukavu.
Hata hivyo, kwa sasa, hali katika mji wa Goma inaripotiwa kuwa tulivu, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kawaida. Wanamgambo wa M23 wameonekana wakifanya usafi katika mitaa ya mji huo wakiongozwa na viongozi wao, ishara kwamba wanadhamiria kuimarisha udhibiti wao katika eneo hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED