Namna ushabiki mpira kupitiliza unavyoangukia madhara ya moyo

By Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 12:51 PM Feb 20 2025
Tabibu Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNP), Dk. Saidi Kuganda,
Picha: Mtandao
Tabibu Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNP), Dk. Saidi Kuganda,

KATIKA jamii kuna aina tofauti za michezo, ukiwamo mpira wa miguu, kikapu na pete kwa kinamama.

Hasa katika soka, kunaonekana mashabiki wake kuwa na mapenzi yaliyopitiliza mchezoni, baadhi yao wakipata shida za kiafya na kuwapo matukio duniani wanapoteza maisha, sababu kuu ni timu yake kufungwa.

Kimsingi, hata katika mpira wa kikapu nako si salama katika nchi kama Marekani ambako ushabiki wake uko juu sana.

Nchini Tanzania, hadi kufika mwanzoni mwaka miaka ya 1990, mpira wa pete na kikapu nayo ilikuwa juu kuteka hisia za umma, kukashuhudiwa ushabiki mkubwa.

Kuanzia na mpira wa pete, ikiwa na timu maarufu kama za Bora, Jeshi Stars na Bima, wakiendana na majina ya wachezaji maarufu kama Judith Chifupa na Fatuma Chivumba walitikisa hisia za mashabiki uwanjani.

Hali kadhalika kikapu kuwapo Benki Kuu (BoT), Vijana na Pazi iliyotetewa na kocha mchezaji, Salehe Zonga, kulitekwa na ushabiki, mathalan katika mechi ya vijana dhidi ya Pazi, au moja ya timu timu, inapotokea kuchuana na BoT, ambayo mmoja wa nyota wake, Stephen Mbundi, leo hii ni Katibu mkuu katika wizara.

Hayo yote ushabiki na mihemuko yake ikiirejeshwa katika tafsiri ya kiafya, inatajwa kuwa mabadiliko ya utendaji kazi wa moyo wao, athari zikiangukia katika mishipa ya damu.

Hapo, Tabibu Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNP), Dk. Saidi Kuganda, anafafanua undani wa kitabibu kufikia athari hizo kimwili.

Anasema, kitu kinachotokea kwao ni kemikali zilizoko mwilini kupanda kwa kasi na kusababisha mtu kupata maumivu ya moyo, wakati mwingine anapoteza maisha.

Dk. Kuganda anasema kuwa mtu anapoambiwa jambo la furaha au huzuni, kuna upokeaji wake wa taarifa hiyo, wakiwapo wanaopokea kwa msemo aina yake kulingana na nafsi yake; wapo wanaopokea kwa furaha na wengine huzuni.

Anautaja ndio mzizi wa kutokea changamoto zinazoweza kusababisha kifo na wakati mwingine, mtu anaumwa, hivyo kila kitu kinatakiwa kwa kiasi.

Bingwa huyo wa tiba anasema, wapo watu wanaoshabikia mpira pindi timu inapofungwa, wao wanaanza kukinzana na wengine katika hilo.

Mtaalamu huyo anashauri wanaokuwa na matatizo ya afya ya akili, waonane na mtaalamu afya au mwanasaikolojia katika hali itakayowasaidia kujiweka sawa kwenye mfumo mzima wa afya ya akili, tayari kuangalia mechi ya mpira.

Hata hivyo, kwa wenye maradhi ya moyo anawataka kwenda kwenye vituo vya afya kabla ya kuangalia mpira au wasiangalie kabisa, ili kutetea usalama wao kiafya, kwani inaweza kuwasababisha madhara.

Dk. Kuganda anasema katika utengenezaji mfumo vyema, kanuni nzuri ya afya ni lazima mambo yote yawe kwa kiasi, mtu unapokuwa na furaha kiasi utendaji mzuri wa kazi zake kiafya unakuwako na y kuimarika.

Hivyo, mtu aliyepatwa na mshtuko, baada ya timu yake kufungwa, Dk. Kuganda anashauri kutojifungia ndani na kujipa mawazo muda wote.

Anataja, pia wahusika wajichanganye na marafiki wataokaoweza kumpa mawazo bora yanyaoweka akili yake sawa.

Maoni hayo ya kitaalamu ni kwamba penye ziada ya mawazo katika jamii, wataalamu afya wanashauri mhusika kuchukua hatua ya kujihusisha kinachoweza kumletea furaha.

Inashuhudiwa katika uzoefu wa kitaalamu kwamba, baadhi ya mashabiki hawajagundua kanuni na taratibu za kuangalia mpira huo, kwani wanasahau mtu anapoangalia mpira kuna ‘kushinda na kushindwa.’

Hapo ndipo inafafanuliwa kitabibu kwamba shabiki kipenzi anapofahamu hayo, inampa uhuru kukumbuka kuwa ‘mchezo ni furaha,’ nadharia inayoweza kumsaidia na kuwa tayari kwa lolote, ikiwamo upande anaoshabikia kufungwa, akijipa ahadi kama “sawa wamefunga tusubiri msimu ujao,” na “asiyekubali kushindwa si mshindani.”