JUMANNE ijayo, wadau na mashabiki wa muziki Afrika Mashariki, wataadhimisha miaka 37 ya kifo cha aliyekuwa mwanamuziki maarufu na mahiri wa bendi ya Juwata Jazz Band wakati huo, wana Msondo Ngoma.
Mwanamuziki huyu mwenye ulemavu wa macho, kwa muda mfupi tu alioingia na kufanya kazi ya muziki nchini akutoka Kenya, akipigia bendi mbili tu, za Les Cubano ya Morogoro, na Msondo Ngoma, aliondokea kuwa kipenzi cha wanamuziki wa dansi nchini, kutokana na umahiri wa kuimba, kutunga, ikiwemo sauti yake nyororo, laini, mwenyewe akiwa na uwezo wa kuitumia vyovyote atakavyo, wakati mwingine akitetemesha kama maji yanayotoririka kutoka kwenye milima.
Ni mwanamuziki ambaye kuanzia 1984, hadi kifo chake, alikuwa amejikusanyia mashabiki wengi na kuwa gumzo kiasi cha kuzima umaarufu wa wanamuziki wengi nchini Tanzania.
KIFO CHAKE
ILIKUWA ni saa tatu usiku ya Desemba 17, 1987, kwenye kipindi cha majira, ndipo mtangazaji alipowatangazia Watanzania kifo cha ghafla cha mwanamuziki maarufu sana wakati huo, Nico Zengekala.
Mtangazaji akasema, mwanamuziki huyo alifariki ghafla saa 11:00 alfajiri, nyumbani kwake Mtaa wa Sikukuu, Dar es Salaam.
Kilichotokea ni taharuki. Hakuna aliyeamini kuwa Nico, mwimbaji mwenye sauti tamu, nyororo ambaye ni mlemavu wa macho, amefariki. Mwanamuziki ambaye tayari alikuwa ameshajinyakulia mashabiki wengi nchini Tanzania, miaka michache tu tangu aingie nchini kutokana na umahiri wake wa kuimba, akitokea kwao Kenya.
Habari zaidi zinasema kuwa hadi saa sita usiku, kuamkia kifo chake alikuwa anapiga soga na marafiki zake mitaa ya nyumbani kwake, Kariakoo mtaa wa Sikukuu, Dar es Salaam ambako alipewa nyumba ya kuishi na bendi aliyokuwa anapigia ya Juwata Jazz, wana Msondo Ngoma.
Zilikuwa ni moja kati ya nyumba zinazomilikiwa na Juwata.
Kutokana na ustaa wake, na kifo chake cha ghafla, ilisababisha taharuki kubwa, vilio, simanzi, na kila aina ya huzuni ilitawala, Tanzania, Kenya na Uganda, huku baadhi ya Wabongo wakiwa hawaamini kama kilikuwa ni kifo cha kawaida.
Ni kifo kilichozua maneno mengi kuliko kawaida. Wengine wakasema ni mambo ya kishirikina. Wapo waliodai alilishwa sumu. Na wengine walisema umaarufu wake alioupata kwa muda mfupi tu, ulikuwa ni mwiba kwa wanamuziki si wa Msondo tu, bali hata wa Tanzania nzima, alioneka kuwafunika, hivyo baadhi yao hawakupendezewa. Lakini yote hayo yanamalizwa na ripoti ya madaktari kuwa alifariki kwa ugonjwa wa kifafa. Ndiyo uliomuondoa akiwa na umri kati ya miaka 20 hadi 24.
NYIMBO ZAKE
Alipoingia nchini na bendi ya Les Cubano, alitamba na vibao kama 'Jackie', 'Mwalimu Nyerere', 'Suzzy', 'Bwana Salim', 'Shemango', 'Mama Hisani' na nyingine nyingi.
Mwaka 1985 alichukuliwa na Msondo ngoma ambako nako alitamba na vibao kama 'Solemba' alichokitunga mwenyewe na vingine akiviimba kwa ustadi mkubwa kama 'Hasira Hasara', 'Kaka Mahmood', 'Asha Mwanasefu', 'Prisila', 'Kambarage Nyerere' na nyingine.
Wengi hawajui kuwa Nico Zengekala aliimba kwa umahiri mkubwa na kutunga nyimbo ambazo hadi anafariki alikuwa hajazirekodi. Nazo ni 'Dalila', huku akitunga 'Cha Mlevi hulikuwa na Mgema', pamoja na 'Razole' ambazo kama angebahatika kurekodi ingekuwa habari nyingine.
Hivi vyote awali ilikuwa virekodiwe na Nico, lakini alifariki kabla ya kwenda studio.
Kama nilivyosema, alikuwa na sauti tamu, nyororo, kali, ambayo alikuwa na uwezo wa kuitetemesha na, wakati mwingine akiishusha sauti kama mtu anayeweseka hivi.
KUINGIA KWAKE NCHINI
Alizaliwa katika kijiji cha Wundayi eneo la Mwatate karibu na mji wa Voi, kiasi cha kilometa 100 hivi kutoka Mombasa nchini Kenya.
Alichukuliwa na kuletwa nchini na mabaki wa wanamuziki wa Super Volcano ya Mbaraka Mwinshehe aliyefariki Kenya mwaka 1979, ambao baadhi walijiunga na Simba Wanyika, Les Wanyika, Wanyika Stars, Super Wanyika na Jobiso, ambao walimuona akiimba kwenye bendi moja ya Wataita wenzake Nairobi.
Wanamuziki hao ambao ni Watanzania waliokuwa nchini humo wakiendelea na shughuli za muziki, waliombwa kurejea nchini na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati huo Nicodemus Banduka, hivyo wakaamua kumchukua Nico, ambapo yeye mwenyewe pia alitaka kuondoka Kenya.
Kwa mujibu wa mwanamuziki Said Makelele ni kwamba ilibidi kwenda kumuomba baba yake, ambaye aliwakubalia kwa madai kijana wake ameshindikana, kwani amemkataza sana mambo ya muziki, lakini amekuwa akitoroka nyumbani kwa kupasua dari juu, kwenda kuimba sehemu mbalimbali licha ya kumfungia na kufuli ndani. Baba yake aliwaambia kuwa akidhani amemfungia, lakini watu wanakuja kumwambia amemuona akiimba kwenye mabaa na kumbi mbalimbali, huku wakimsifia kwa uimbaji wake.
Makelele anasema ilibidi wadanganye ni Mtanzania ili aruhusiwe kuvuka mpaka wa Tanzania na Kenya, kwani wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17, hivyo asingeweza kuruhusiwa kuvuka Wakadai ni Mtanzania wa Dodoma na wao ni wanamuziki wanaorejea nyumbani Tanzania kwa wito wa Mkuu wa mkoa wa Morogoro, ndipo waliporuhusiwa.
Inawezekana wakati anafariki huenda alikuwa hajafikisha hata miaka 24, na inawezekana Msondo walimpandisha umri ili aweze kuajiriwa na Jumuiya ya Wafanyakazi wa Tanzania JUWATA, kwani wasingeweza kumuajiri mtoto.
Ni kwa sababu kama aliingia nchini ana miaka 17 na hakudumu na bendi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili akajiunga na Msondo.
Ni mwanamuziki aliyedumu kwa muda mfupi nchini, lakini sauti na uimbaji wake hadi leo hi umeendelea kuwa lulu na wimbo wake wa 'Solemba' na msamiati ukiendelea kuishi.
Hakuwa staa kwao Kenya, lakini nyota ilimuwakia nchini na hata mwili wake uliposafirishwa, ulikuwa ni msafara na heshima kubwa wa magari lukuki ya serikali ya Tanzania, Jumuiya ya Wafanyakazi wa Tanzania, Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata), wapenzi na mashabiki kama vile anayekwenda kuzikwa ni kiongozi mkubwa wa kitaifa.
Hii iliwashangaza na kuwaliza wengi kwao, zaidi wazazi na ndugu zake, kwani aliondoka akiwa wa kawaida tu, lakini maiti yake imerudishwa nyumbani kishujaa. Hawakuamini.
Alizikwa kijijini kwao Wundayi, Mwatate, Voi, Taveta nchini Kenya Desemba 24, 1987.
Huyo ndiyo Zengekala, mwimbaji 'kipofu', kutoka Kenya, aliyeacha simulizi isiyofutika Tanzania.
Tuma meseji 0716 350534
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED