Mechi za kwanza muundo mpya Uefa na ubora wake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:03 AM Sep 23 2024
Raya
Picha:Mtandao
Raya

RAUNDI ya kwanza ya mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya imekamilika na sasa tunajaribu kuangalia namna mambo yalivyokuwa.

Muundo ni mpya msimu huu huku timu zikiwa zimeongezeka hadi 36 badala ya 32 zilizokuwa zinagawanywa kwa makundi nane.

BBC Sport inaangalia kile kilichotokea katika mzunguko wa kwanza wa michezo na jinsi ushindani ulioboreshwa unavyoonekana. 

# Msimamo mpya wa ligi

Awamu hii mpya badala ya timu kuuunda makundi nane yenye timu nne, imekuwa tofauti na itachukua muda kuzoea.

Msimamo mmoja mkubwa wenye timu 36 ni jambo ambalo hatulioni hata kwenye soka la ligi za nchi mbalimbali.

Kumbuka, timu zitakazomaliza katika nafasi nane za juu zitafuzu moja kwa moja kwa hatua ya 16 bora, huku zile zitakazoshika nafasi ya tisa hadi 24 zitachuana katika hatua ya mtoano kwa mikondo miwili ili kupata nafasi ya kuungana nazo.

Yeyote atakayemaliza nafasi ya 25 au chini ataondolewa. Kwa hiyo ni theluthi moja tu ya timu hutoka baada ya kila mtu kucheza mechi nane.

Kwa mujibu wa Opta, pointi 16 kutoka mechi 24 zinazowezekana zinatoa nafasi ya asilimia 98 ya kumaliza nane bora.

Pointi 10 ni asilimia 99 ya uwezekano wa kumaliza nafasi ya 24 bora, kwa hiyo timu zilizoshinda wiki hii zinahitaji ushindi mara mbili tu na sare moja ili kupata nafasi ya kutinga hatua ya 16-bora.

Timu 15 zilishinda michezo yao ya ufunguzi (ikimaanisha timu 15 zilipoteza) ambayo inaacha klabu sita katikati kwa alama moja.

Kwa kifupi, ukishinda una nafasi kubwa ya kupita. Ikiwa umepoteza ... bado una nafasi nzuri. 

# Ilikuwa ya ushindani?

Ni mapema mno kusoma mpangilio wa matokeo... lakini vinara wa juu walipoteza pointi zaidi wakati huu ikilinganishwa na mzunguko wa kwanza wa michezo ya kundi mwaka jana.

Msimu uliopita timu sita kubwa kati ya nane zilishinda, huku moja ikitoka sare na kupoteza mmoja.

Mwaka huu kulikuwa na vinara tisa wa juu, huku watano wakishinda, wawili wakitoka sare na wawili wakipoteza. 

# Timu za chini zilifanya vizuri zaidi

Timu nne cha chini kati ya tisa kwenye 'chungu cha nne' zilishinda - ikiwa ni pamoja na Aston Villa. Mwaka jana hakuna timu yoyote kati ya nane za chini iliyoshinda mchezo wao wa kwanza wa kundi.

 # Michezo mikubwa ilileta matokeo?

Moja ya faida za muundo mpya ni michezo zaidi kati ya timu kubwa.

Tofauti na siku za nyuma, kila timu kubwa ya juu itakutana na timu nyingine mbili kutoka chungu cha juu pia.

Mechi pekee kubwa ilikuwa Manchester City dhidi ya Inter Milan... ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana.

Lakini hiyo haikuwa mechi pekee iliyovutia macho katika mzunguko wa kwanza, Liverpool ikikutana na AC Milan katika marudio ya fainali za 2005 na 2007. Timu hiyo ya Ligi Kuu England ilishinda 3-1.

Mechi kubwa zinazokuja hivi karibuni, si lazima ziwe kubwa zaidi, ni Arsenal dhidi ya Paris St-Germain katika kundi lijalo la michezo, pamoja na Real Madrid dhidi ya Borussia Dortmund – ambayo ni kama marudio ya fainali ya mwaka jana.

Barcelona dhidi ya Bayern Munich iko katika raundi ifuatayo ya ratiba - ingawa wawili hao walikutana katika hatua ya makundi miaka miwili iliyopita. 

# Timu za Uingereza vipi

Ulikuwa ufunguzi mzuri kwa timu tano za Uingereza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa tatu kushinda na mbili kupata sare.

Celtic iliishinda Slovan Bratislava mabao 5-1, Aston Villa ikailaza Young Boys 3-0 na Liverpool ikashinda 3-1 dhidi ya AC Milan.

Manchester City na Arsenal zote zilitoka sare tasa na timu za Italia, mabingwa wa Serie A, Inter Milan na washindi wa Ligi ya Europa Atalanta.

 # Wachezaji waliovutia macho

Harry Kane aliifungia Bayern Munich mabao manne walipoichabanga Dinamo Zagreb 9-2. Hiyo tayari imempeleka kufikia nusu ya jumla ya mabao yaliyomfanya kushinda kiatu cha dhahabu msimu uliopita.

Wachezaji wengine watatu walifunga mabao mawili, yote kwa klabu za Ujerumani - winga wa Borussia Dortmund na England chini ya umri wa miaka 21, Jamie Gittens, Michael Olise wa Bayern Munich na Florian Wirtz wa Bayer Leverkusen.

Golikipa aliyekuwa na matokeo ya kukumbukwa katika raundi ya kwanza ya mechi alikuwa David Raya wa Arsenal, ambaye alifanya kazi nzuri ya kuokoa mara mbili - ikiwa ni pamoja na mkwaju wa penalti – na kumnyima bao mshambuliaji wa Atalanta, Mateo Retegui. 

# Timu zitakazoshangaza

Timu ambazo zinaweza kuwa na furaha zaidi na kazi yao ni Celtic, ambayo ilifunga mabao matano katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza, na Sparta Prague.

Sparta, katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa kwa miaka 19, waliifunga Salzburg 3-0.

Brest ya Ufaransa, ambayo ilikuwa ikicheza mechi yake ya kwanza katika mashindano yoyote ya Ulaya, ilishinda Sturm Graz 2-1.

Girona, ambayo pia alicheza mechi ya Ulaya kwa mara ya kwanza, walikuwa sekunde chache kutoka sare huko Paris St-Germain kabla ya Paulo Gazzaniga kujifunga.