UNAPOTAJA mgodi, uwe mdogo au mkubwa, ni sehemu mojawapo ya maeneo yanayoshika uchumi wa wakazi, hasa Ukanda wa Kati nchini na Kanda ya Ziwa.
Hapo kunatajwa kupitia ajira rasmi na isiyo rasmi ilikihusiana na uchimbaji mkubwa na mdogo wa madini kama dhahabu.
Katika uchimbaji mdogo, imekuwa kawaida wahusika wake wanakusanyika kufanya kazi hiyo katika ngazi ya ujasiriamali kuanzia nyenzo, hadi teknolojia husika.
Ni bahati mbaya, angalizo hilo halijafanikiwa vilivyo, kundi hilo la wachimbaji wadogo limekuwa wakala wa kueneza kwa kasi ugonjwa wa Kifua kikuu (TB).
Sababu mojawapo inatajwa ni aina ya mazingira wanayofanya kazi kuwa na msongamano mkubwa wa watu, huku ugonjwa ukihusishwa na imani za kishirikina.
Ni mazingira ya mrundikano wao shimoni wakati wa kuchimba madini na kukosekana hewa safi, hali kadhalila tabia ya uvutaji sigara kwa kupokezana, pia unywaji pombe wakiwa katika makundi, huku wengi hawazifahamu dalili za TB.
Kurejea takwimu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO), kupitia tovuti yay a Aprili, 2023, zinaonyesha watu milioni 1.6 (ikiwa ni pamoja na watu 187,000 wenye maambukizi ya ukimwi) walikufa kwa ugonjwa wa kifua kikuu duniani.
Mwaka 2021, nako kunakadiriwa kuwa watu milioni 10.6 walipata ugonjwa huo duniani, wanaume milioni sita, wanawake milioni 3.4, na watoto milioni 1.2 waliambukizwa maradhi hayo katika maeneo mbalimbali duniani.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2,000 watu milioni 74 wamesalimika baada ya kupona kifua kikuu, kutokana na mashirika mbalimbali duniani kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kwa kushirikiana na serikali zao.
Ndani ya mustakabali huo, hali ya kifua kikuu nchini haipo vyema, Tanzania imo katika nchi zenye orodha isiyoridhisha duniani, kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Ahmed Makuwani, katika kikao na Waganga Wakuu wa Mikoa, pia Waratibu wa TB na Ukoma, jijini Dodoma Januari mwaka huu.
Chanzo kimojawapo cha kuenea ugonjwa huo duniani, inajumuishwa na misongamano ya watu, hasa katika nchi zilizopo Kusini mwa janga wa Sahara.
Inapoangaliwa ugonjwa, huambukiza kwa njia ya hewa na inakuwa rahisi mtu kupata maambukizi, ikitajwa kuwa sababu inayowafanya wachimbaji wanapata ugonjwa na kueneza haraka.
Jitihada za nchini zinatajwa, serikali kuendelea kubuni mbinu za kukabiliana na ugonjwa, kukitajwa kuwapo kundi kubwa la wachimbaji wadogo ambalo halijafikiwa na kupewa elimu sahihi ya a kukabiliana na maradhi TB.
Inaelezwa, kuwapo tabia ya hata wale wanaougua na kutibiwa kwa mwongozo rasmi, baadhi yao hukimbia matibabu, mara baada ya kupata nafuu, hata wanaishia kueneza ugonjwa sehemu nyingine.
KAULI ZA WACHIMBAJI
Samweli Amosi, mchimbaji madini katika Mgodi wa Mwabomba, katika Halmashauri ya Ushetu - Kahama, anakiri baadhi yao hawazifahamu dalili za ugonjwa huo.
Anasema wanapouguia na kufika hatua ya kukohoa sana, wanadhani ni kutokana na vumbi mgodini wakati wa kusaga mawe, wanakimbilia kunywa maziwa ambayo hayawasaidii.
Anasema, hali ya kiafya inapoanza kuwa mbaya zaidi, wanashauriana kurudi majumbani kwa wazazi au wake zao, kuangalia namna ya kutibiwa kwa njia ya asili, wakiamini wamelogwa.
Kuna wanaofikia katika vituo vya afya na kupima, wanapewa majibu ya kuwa wanaumwa TB, hata wanaanza kutibiwa haraka.
Mwenzake, William Samweli kutoka mgodi wa Mwakitolyo wilayani Shinyanga, anasema migodi yote midogo nchini, haina utaratibu wa kupima afya zao watumishi, ili kutambua afya ya mgeni anayeingia.
“Sisi hatuna utaratibu wa kupima afya wala kujikinga na TB. Tunakusanyika bila mpangilio, tunabadilishana vinywa na sigara kiholela.
“Tunachofahamu tu ni kujikinga tusipate VVU na Ukimwi kwa kutumia kinga zilizopo kwenye nyumba za kulala wageni zilizopo migodini tu,” anazungumza Mabula.
Patricia Swai, kutoka mgodi wa Nyangalata, anasema mjasiriamali anayenunua mawe yanayosadikika kuwa na madini, kwenda kusaga kienyeji, akiwa hana hatua ya kujihami kuvaa vifaa kinga afya yake, akiamini kisailikolojia, majibu mabaya yatamdhoofishia safari ya kutafuta riziki.
VIONGOZI WA MACHIMBO
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) Hamza Tandiko, anakiri kuwapo ugonjwa wa kifua kikuu mgodini.
Anasema, katika jitihada za kuondoa maradhi TB migodini, inapaswa serikali kwa kushirikiana na wadau kubuni hatua za kitabibu katika maeneo hayo kudhibiti madhara.
Pia, anakiri uhalisia wa hatari ya TB kwa wachimbaji wadogo na ni sababu sasa wameweka utaratibu wa kuhakikisha wanaosaga mawe yanayosadikiwa kuwa na madini wanavaa maski, miwani na viatu vigumu.
Tandiko anasema, pia maeneo ya uchenjuaji yametengwa yasiingiliane na maeneo ya wajasiriamali wadogo, huku.
Anataja mkakati mmojawapo wa kupambana na TB, ni kwa wachimbaji kuwa na makabrasha ya kusaidia mawe yenye mfumo wa maji.
Ili kutimua vumbi wakati wa usagaji mawe na baadhi ya maeneo anajisifu wamefanikiwa na kuwapongeza watoa huduma ngazi za jamii kuwatembelea na kuwakumbusha namna ya kujikinga na Ukimwi pia.
“Tunataka kuitisha mkutano wa wadau tujadili namna ya kupata vituo vya kupima afya zetu migodini, ili tupambane na TB na Ukimwi, tunaimani serikali yetu itatuunga mkono juu ya hili…
“Tunalipongeza Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi kuwatembelea na kuwaelimisha juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia,” anaongeza.
Mdashi Shabani, Meneja wa Mgodi wa Nkandi Mtaa wa Ilindi-Mwime kata ya Zongemela Manispaa ya Kahama, anasema hawana utaratibu wa kupima afya kabla na baada ya kuingia shimoni.
Sasa anawasisitiza wachimbaji kuchukua tahadhari shimoni, huku wakiwa wanatembelewa na wala,au wa afya serikalini, wanaopowaona afya zao dhidi ya maradhi kifua kikuu na Ukimwi.
Kiutaratibu, anaeleza kwamba, kila
mara wanapimwa na wanaobainika kuwa na maambukizi, wanaanzishiwa matibabu haraka, ikiwa ni utaratibu unaoofanyika kwa hiari
“Tunapobaini mmoja wetu ana ugonjwa wa TB, tunamsimamisha shughuli ya uchimbaji ili asiendelee kuchangamana na wengine na kueneza ugonjwa huo.
“Akianzishwa matibabu na akapona, anakuja na udhibitisho wa daktari, ndipo tunamruhusu kuingia ‘duarani’ na kuchimba madini,” anasema Shabani.
Meneja wa Mgodi wa Mwakitolyo,. Wilayani Shinyanga, Michael Matemla, anasema wanachowapima sana wachimbaji wao kabla ya kuingia ‘duarani’ ni ulevi na anayebainika haruhusiwi kuingia ‘duarani’, sasa anaiomba serikali kuwafikia wachimba kuwapatia elimu kufahamu dalilili za ugonjwa huo.
WARATIBU TB
Maratibu wa Tiba Kifua Kikuu (TB) na ukoma mkoa wa Shinyanga, Dk. Laurent Mhembe, anasema ugonjwa huo una wachimbaji wadogo.
Anasema kwamba kuna tabia ya wanaobainika kuwa na maambukizi, huwa hawamalizi dozi wanazopewa, baada ya kupata nafuu, wakihamia katika migodi mingine.
Dk. Mhembe anasema, mnamo mwaka 2023 waliwafikia wagonjwa 2,894 kati yake 579 walikowapatia wachimbaji wadogo wakiwapatia matibabu kutoka katika halmashauri za Msalala, Ushetu, Kishapu, Shinyanga Vijijini, pia manispaa za Shinyanga na Kahama,
Dk. Mhembe anasema, mwaka uliofuata 2024 waliwafikia wagonjwa 1,622 na kati yake 254 walikuwa wachimbaji wadogo.
Anasema changamoto kwaoni ukosefu wa usafiri kwa watoa huduma na ukisababisha wasifike maeneo mengi ya wachimbaji na wanaishia kuwatembelea walipo karibu.
Mtaalamu huyo analalamika, mwaka huu hadi kufika Februari 11, walikuwa wamewafikia wagonjwa 450 pekee
Dk. Michael Mashala, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Geita, anakiri kuwapo ugonjwa, akitaja changamoto iliyoko kwa wachimbaji wadogo, wamekuwa wakihama bila ya kumaliza dozi, huku waliojikitokeza kwa tiba katika kipindi kigumu kwao, hawako vizuri kiafya.
Anasema, mara kadhaa wamekuwa wakipewa taarifa na viongozi wa wachimbaji siku za vikao vyao na wanafika kuwaelimisha undani wa ugonjwa huo na Ukimwi.
Dk. Mashala anataja huduma wanazowapa nio kuchukua sampuli za afya zao, wanazipima na kiwarejeshea majibu kwa njia ya simu zao na wanaobainika kuugua, wanaanzishiwa matibabu.
Dk. Mashala anatoa takwimu kwamba mwaka 2023 waliwahudumia wagonjwa wa TB 3,867 na asilimia 18 walikuwa ni wachimbaji wadogo.
Pia, anataja mwaka uliopita, waliwahudumia wagonjwa 3,673 na asilimia 21 walikuwa wachimbaji wadogo wa madini, huku mwaka huu akitaja hadi wiki mbili zilizopita walikuwa na wagonjwa 403.
Anataja, changamoto yao klwa sasa, ni kupungua wahudumu ngazi ya jamii wenye uwezo wa kufikia wanajamii waliko, wachimbaji wengi wanakuwa ‘mduarani.’
RC NA MGANGA MKUU
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, anatamka: “Mkoa huu una wagonjwa wa kifua kikuu 2,903 huku watu 1,349 bado hawajafikiwa ambao ndio wanatafutwa kupitia kampeni ya ‘Tokomeza Kifua Kikuu.’
Anasema, mtu mmoja mwenye tatizo la kifua kikuu, kwa mwaka mmoja anaweza kuambukiza watu 20 na anataadharisha, hatua zisipochukuliwa, anatahadharisha tatizo linakuwa kubwa zaidi.
Macha anawasihi wagonjwa wanaobainika kutumia dawa kwa kumaliza dozi na siyo kukatisha hali, inayosababisha kifua kikuu kuendelea kuwa usugu mwilini.
Pia, anawataka watoa huduma ngazi ya afya kutoa elimu migodini waliko wachimbaji, watambue namna ya kujikinga.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Ahmed Makuwani katika kikao na Waganga Wakuu wa Mikoa, pia Waratibu wa TB na Ukoma, jijini Dodoma Januari mwaka huu, waliweka mpango wa kuwaibua na kuwafikia wagonjwa wa TB zaidi ya 14,000, wakiwamo watoto, ili kuutokomeza ifikapo mwaka 2030.
Anasema, inategemewa kutekelezwa katika vituo vya kutoa huduma za afya ngazi ya jamii na makundi hatarini kuambukizwa, hasa wachimbaji madini migodini na wavuvi, ikitekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara, pia halmashauri zake 76.
Dk. Makuwani anasema, serikali inakabiliana na changamoto ya kuwapata wagonjwa wa kifua kikuu, ikiweka nchi katika kundi la nchi 30 zinazochangia asilimia 87 ya wagonjwa wote wa TB duniani, serikali ikijipanga kujiengua.
Anasema, serikali kupitia Wizara ya Afya, imegawa mashine 185 za ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa huo, lengo ni kupunguza nusu ya vyanzo vya kifua kikuu na vifo kufutwa kwa asilimia 75 mwaka huu, ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2015.
Kwa kurejea takwimu za mwaka 2023, Tanzania hadi sasa imeshapunguza maambukizi ya kifua kikuu asilimia 40.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED