KWA HERI 2024; Kumbuka mwaka haubadilishi chochote

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:10 AM Dec 31 2024
 Kwa heri 2024
AI
Kwa heri 2024

KWA HERI 2024 karibu mwaka mpya. Mioyo ya watu imejaa shukurani kwa Mungu ambaye amewapa nafasi ya kuishi hadi leo.

Wapo wenye uchungu wa magonjwa, misiba na taabu lakini wote wamshukuru Muumba maana ni mapenzi yake kwao.

Kwa ujumla mwaka haubadilishi kitu kinachobadilika ni fikra au mawazo yako. Nyakati na majira zinabakia zilivyo. Usiku na mchana vitaendelea kuwepo, pia jua, mbalamwezi , joto mvua ni vya kudumu.

Ila wewe unabadilika kujipa maisha bora zaidi na kuongeza bidii ili usiishi kama ulivyokuwa mwaka jana. Kumbuka ni fikra zako ndizo ziwe mpya siyo mwaka mpya 2025. Kuwa na maono, mawazo na mitizamo chanya na mipya zaidi.

Unapoanza mwaka usitafute lawama mbona sijafanya hiki, sina nyumba, fedha wala mke au mume, mtoto tena wengine wakilalama nina watoto wa kike tu nitapataje wa kiume. Acha maana kuna wasio na watoto.

JITATHIMINI LEO 

Unapoikaribisha 2025 cha muhimu ni kujitafakari na kujitathimini mwenendo wa maisha yako. Inapendeza kama utachukua karatasi na kalamu upitie suala moja hadi jingine na kwa kila hatua ibua ubovu, udhaifu, mafanikio na panga kubadilika.

Unaweza kujihoji hasa kwenye uhusiano na watu wengine kuanzia mwenza, ndugu wa damu, watoto, majirani na wafanyakazi ofisini au wengine unaoishirikiana nao katika kazi zako.

Jiulize swali hili, mimi ni mtu wa msamaha au ni wa kisasi muda wote? Ujijibu ukiona una upungufu jirekebishe mwaka huu. Kuendeleza  tabia hiyo kunasababisha shida afya ya akili.  

Unyenyekevu, jipime wewe ni mtu mnyoofu au ni jeuri, unashiriki kwenye mambo ya jumuiya, majirani ama unafanya ubabe wakati wote?  Unawaudhi wenzake kila mara? Dhamiria kubadilika 2025.

Chunguza udhaifu wako unashiriki kwenye masuala ya kijamii mfano mtaani kwako kuna misiba, majanga kama moto unajihusisha? Kwenye jumuiya watu wa kijijini kwako unashirikiana nao kwenye shida na raha?Unatoa michango ya misiba na kushirikiana na wengine kwenye raha na shida?

Jihoji kuhusu akiba unaweka akiba? Iwe mali au fedha kama huna anza sasa na uwe na nidhamu ya fedha. Wakati mwingine unafurahia kuitwa ‘maskini ‘Si jambo jema.’  

Mfano kama familia inachangisha fedha kujenga mfuko wa kujitegemea, halafu wakakubaliana kila mmoja atoe Shilingi 100, 000 lakini wasio na kipato watoe 20,000 usikubali jitutumue  ndiko kuepuka kuitwa maskini. Tafuta pesa kwa juhudi zaidi na kwa njia halali

ANGALIA FURSA

Tafuta fursa kumbuka kuwa maisha yana fursa na kila mmoja ana nafasi anazopata akazifanyia kazi au akazichezea.Tathmini juhudi zako kwenye kutumia nafasi ulizopata za kuongeza kipato na kubadili maisha.

Chunguza umezitumiaje fursa mwaka jana? Umechezea au umenufaika?  Kwa vipi ziainishe kisha uangalie mbele mwaka huu.

Uligeuza changamoto kuwa fursa kujiletea maendeleo?  Azimia kuwa mwaka huu changamoto zitakuwa fursa kwa mfano,  ukiachwa na mwenza sitakubali kulia, nyanyuka fikiria cha kufanya badala ya kukata tamaa na kuanza matendo ya kumkomoa.

Mfano mzazi aliwakataa  watoto wake na kumtelekeza mama yao. Hakuwaendeleza kimaisha hawakusoma wala kuwa na kipato. Hiyo ni changamoto vijana wekeni juhudi fanyeni kazi zaidi ili kuitumia changamoto ya chuki ya baba yenu kuwa fursa ya kujisomesha na kujiongezea kipato na kusonga mbele.

Acheni kulaumu watu au marafiki kuwa ndicho chanzo cha matatizo  badili fikra ili uone maisha katika sura nyingine.

KUWA NA SHUKRANI

Kumbuka kumshukuru Mungu. Bila kujali imani au dini yako fahamu kuwa unaishi kwa sababu kuna Mungu aliyekupa uhai na umshukuru . Unaishi kwa nguvu zake. Pia ni lazima na muhimu hapo uwashukuru watu wanaokusaidia kuendelea na mapambano ya kila siku.

Elewa umepata mafanikio  2024 kwa sababu ya nguvu za Mungu. Fahamu baraka ulizo nazo siyo kila mmoja anazo, hata afya uliyo nayo sio kwamba kila mtu ameipata. 

Sio kila mtu anaishi, mamia hawana pumzi kumbuka afya uliyo nayo si Watanzania wote wanayo. Watu wangapi wamefariki unaowajua na hata usiowafahamu uliowasoma kwenye mitandao? Mambo mengi uliyo nayo mfano ujuzi na elimu ulio nayo kuna mamia wanaitafuta. 

Kadhalika familia uliyojaliwa mshukuru Mungu si kulalamika eti una watoto wasichana wakati unataka wa kiume, usifikiri kutafuta nyumba ndogo mshukuru Mungu, maana wapo ambao hawana watoto.

ACHA KUJIDHARAU

Watu wanajidharau mimi sina hiki wala kile. Wanatamani au kujilinganisha na wengine. Usijidharau kwa kuangalia mafanikio ya wengine. Usiwe na dharau kwa baraka ambazo Mungu amekupa badala ya kuangalia zile ambazo huna mfano gari, nyumba, ardhi na fedha. 

Kama hujafanikiwa azimia kupata mafanikio mwaka huu.  

KUMBUKA

Mwaka mpya umenza na unatakiwa kubalisha fikra ziwe tofauti, maana majira na wakati havibadiliki ila wakubadilika ni wewe.

Unapochana kalenda ya mwaka jana, anza kwa kujishukuru na kufurahia mafanikio yako . Hata kama umenunua na kuweka kitasa kipya kwenye mlango ni mafanikio yafurahie. Usijilaumu, unajiongezea msongo, hofu na matatizo ya akili.

Kula kwa afya siyo kujaza tumbo kwa kubugia chochote ali mradi umekula. Mfano kujaza tumbo kwa  ugali mkubwa na rojo la nyanya zilizoharibika au masalo siyo kujali afya.  Na kupata chakula angalau mara tatu kwa siku.

Ni vizuri kufanya mazoezi, kulala muda wa kutosha, kujikinga na maradhi siyo kujiachia mfano hunawi mikono na maji tiririka kabla ya kula, unaparamia matunda sokoni bila kuosha. Kunywa pombe muda wote.

Lala kwenye chandarua kujikinga na malaria na kwenda hospitalini kama unaumwa, usikimbilie vidonge kwenye maduka ya dawa.

Usisahau kujipenda vaa vizuri na nguo safi. Tunza mwili wako na pumzika kama unaumwa maana kazi haziishi. Zipo kila siku.  

Katika maisha jambo muhimu ni kukaa karibu na watu unaowapenda na kufurahi pamoja nao. Ipende familia yako  na mara nyingi fanya mambo mema, saidia wenye shida au wahitaji , kucheka ni vizuri pia usisahau  kujadiliana na wenzake masuala muhimu yanayohitaji ufumbuzi.

Kusali ni lazima. Jipe wakati kutafakari maisha yako na mwenendo mzima unaoupitia. Ni vizuri pia kusema hapana kama jambo hukubaliani nalo. Kadhalika ndiyo kama unaona unaridhishwa nalo.