Wakati watumiaji wa bia wakianza kufurahia msimu wa sherehe za mwaka huu, wengi wao huenda hawafahamu ya kwamba chapa zao pendwa huenda zisidumu kwenye rafu mbalimbali nchini kwa muda mrefu.
Mapema mwezi huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Obinna Anyalebechi, alionya juu ya uwezekano wa mabadiliko makubwa katika sekta ya bia nchini Tanzania, ambayo yanaweza kusababisha kufungwa kwa biashara hasa kwa wazalishaji wadogo.
Obinna alizungumzia mabadiliko ya hivi karibuni kwenye muundo wa ushuru wa bia nchini Tanzania, ambayo yameibua wasiwasi miongoni mwa watengenezaji wadogo wa bia. Wanahoji kuwa mfumo wa sasa unawapa faida isiyo ya uwiano wazalishaji wakubwa na kudhoofisha ushindani ndani ya sekta hiyo.
Utangulizi wa punguzo la ushuru wa TZS 620 kwa lita moja katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa bia inayotengenezwa kwa shayiri ya ndani umeleta mgawanyiko mkubwa kati ya makampuni makubwa na yale madogo. Watengenezaji wakubwa wa bia, wakiwa na rasilimali za kujenga na kuendesha viwanda vya kuchambua shayiri, wamefaidika sana na punguzo hili.
Kwa upande mwingine, watengenezaji wa bia wadogo, ambao uwezo wao wa uzalishaji ni mdogo, wanakumbana na changamoto kubwa. Gharama za kuanzisha kiwanda cha kuchambua shayiri inakadiriwa kuwa kati ya Dola za Kimarekani milioni 40 hadi 50, uwekezaji ambao, kulingana na Obinna, ni ngumu kwa wengi wao kufanikisha. Tanzania haina chanzo mbadala cha shayiri ya ndani, hali ambayo hapo awali iliwalazimu watumiaji wa shayiri kuagiza kutoka nje na hivyo kulipa ushuru wa juu wa TZS 918 kwa kila lita ya bia inayotengenezwa kwa shayiri ya nje.
Kwa matokeo yake, watengenezaji wa bia wadogo sasa wanajikuta wakilipa ushuru wa juu wa TZS 918 kwa kila lita ya bia inayotengenezwa kwa shayiri ya nje, ambayo ni 32% zaidi ya kiwango cha ushuru kwa bia inayozalishwa kwa shayiri ya ndani. Kulingana na taarifa za Mkurugenzi Mtendaji kwa Kamati ya Bajeti, ushuru wa bia nchini umeunda kile alichokiita "uwanja usio wa usawa kwa wazalishaji wa bia."
Ili kurekebisha hali hiyo na kuunda mazingira ya ushindani kwa pande zote, Mkurugenzi Mtendaji alijiunga na watengenezaji wengine wadogo wa bia kuhimiza muundo wa ushuru wa usawa zaidi, kwa kupendekeza kuanzishwa kwa kiwango cha kati cha ushuru wa TZS 680 kwa kila lita ya bia inayotengenezwa kwa angalau 75% ya malighafi ya ndani.
Watengenezaji wa bia wadogo kwa pamoja wanasema kwamba marekebisho haya yangehamasisha watengenezaji wote kwa sawa huku wakipunguza utegemezi wao kwa shayiri za nje. Kiwango kipya cha ushuru, ambacho hakibagui, pia kitakuza matumizi ya nafaka zinazopatikana kwa wingi katika ukanda huu kama mahindi, mtama, na mhogo. “Kitanufaisha wakulima wengi wa mazao tofauti ya ndani ikilinganishwa na kiwango cha ushuru cha TZS 620 ambacho kimekuwa kikinufaisha kundi dogo tu la wakulima wa shayiri,” alisema.
Obinna aliongeza kuwa mabadiliko yaliyopendekezwa yataimarisha kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa kilimo cha ndani na kuunda mazingira ya kiuchumi yenye uwiano bora. Pia, mwelekeo wa kutumia malighafi za ndani utapunguza matumizi makubwa ya fedha za kigeni.
"Kwa kupunguza uagizaji wa shayiri kutoka nje, fedha hizo zingeenda moja kwa moja mikononi mwa wakulima wa Tanzania, na hivyo kuimarisha maendeleo vijijini na kuimarisha uchumi wa ndani," alieleza.
Akijibu hoja za watengenezaji wadogo wa bia, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge Deo Mwanyika walikiri kwamba hoja za watengenezaji hao ni za msingi na waliahidi kuchunguza zaidi mapendekezo yao.
"Katika juhudi zetu za kuendeleza viwanda vya ndani, tunachukua masuala yaliyotolewa na SBL kwa uchambuzi zaidi, ambayo ndiyo sababu ya ziara ya pamoja ya wizara na Kamati ya Bajeti kwenye kiwanda chao leo," Kigahe alimhakikishia mkurugenzi wa SBL.
Kwa upande wake, Mwanyika alisisitiza maoni ya waziri kuhusu kufanyia kazi mapendekezo ya mtengenezaji huyo kwa kusema: "Tutapitia pendekezo hili kwa kuzingatia maslahi mapana ya kitaifa, kijamii, na kiuchumi ya nchi yetu."
Mnamo Juni 2023, Tanzania Breweries Limited (TBL), mtengenezaji mkubwa zaidi wa bia nchini na mwenye hisa zaidi ya 60% ya soko la bia, alitangaza katika hafla ya vyombo vya habari mipango ya kujenga kiwanda cha kuchakata shayiri chenye thamani ya dola milioni 40 huko Moshi, ambacho kimeanza kufanya kazi tangu mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Jose Moran, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa: Jumla ya gharama jumla za kuboresha kiwanda hiko zinatarajiwa kuwa TZS bilioni 96, ambapo TZS bilioni 42 zimetumika katika awamu ya kwanza. Kwa ujumla, kupitia uwekezaji huu, kiwanda kitapanua mchango wa utengenezaji na kilimo cha ndani katika uchumi wa Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED