BOSI UNICEF: Tunamuona msichana nchini anavyoendelezwa

By Mary Kadoke , Nipashe
Published at 09:12 AM Feb 07 2025
1.	Wawakilishi kutoka UNICEF Makao Makuu na UNICEF Tanzania wakiwa na wasichana balehe, pia wanachama wa Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto (WCPC) katika Kituo cha Elimu ya Watu Wazima cha Old Vwawa, Mbozi mkoani Songwe
Picha: Mpigapicha Wetu
1. Wawakilishi kutoka UNICEF Makao Makuu na UNICEF Tanzania wakiwa na wasichana balehe, pia wanachama wa Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto (WCPC) katika Kituo cha Elimu ya Watu Wazima cha Old Vwawa, Mbozi mkoani Songwe

TANZANIA hadi sasa inatambuliwa kimataifa kwa sera zake za usawa wa kijinsia, ikipiga hatua kubwa katika kuwawezesha wanawake na wasichana.

Hili lilithibitishwa na Dk. Lauren Rumble, Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa Masuala ya Usawa wa Kijinsia, wakati wa ziara yake hivi karibuni mkoani Songwe, alikotathmini juhudi za Tanzania katika kuwawezesha wasichana balehe.

Ziara yake ilionesha uongozi wa Tanzania na mbinu yake shirikishi kwa kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa.

HALI YA UONGOZI

Ziara ya Dk. Lauren ilifanyika wakati muhimu, Tanzania ipo chini ya uongozi wa Rais wa kwanza mwanamke, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyefanya mageuzi makubwa. 

Hiyo inatajwa, hata ngazi ya Afrika Mashariki kwa ujumla. Kama kiongozi wa kwanza Mwanamke wa nchi katika ukanda huu, anafungua milango mipya kwa wanawake na wasichana.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika usawa wa kijinsia. Jambo la kwanza nililogundua ni kuwa, kama wengi wanavyosema.

“Tanzania ni nchi yenye maendeleo makubwa katika masuala ya usawa wa kijinsia, hasa sasa ambapo Rais Dk. Samia ndiye Rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na Afrika Mashariki,” anasema.

UWEZESHAJI WASICHANA

Pia, kumekuwapo kipaumbele cha UNICEF, katika moja ya maeneo makuu yake nchini kuwawezesha wasichana balehe.

Dk. Lauren anaisifu mbinu shirikishi ya nchi, akisisitiza kuwa juhudi za Tanzania zinajumuisha sekta za elimu, afya, ulinzi wa mtoto na lishe. Ni mkakati mkubwa na muhimu kwa kushughulikia changamoto, ambazo zimekuwa vikwazo kwa maendeleo ya wasichana.

Anaongeza: “Mbinu ya Tanzania kwa ‘usawa wa kijinsia’ imechangia mafanikio yake katika kuboresha maisha ya wasichana.

Wanufaika wa huduma za kielimu kwa wasichana mkoani Songwe, katika picha na ugeni wa UNICEF mkoani humo
“UNICEF imekuwa ikishirikiana na serikali ya Tanzania, mashirika ya kiraia (CSOs) na sekta binafsi kuunda mazingira rafiki kwa wasichana, kuhakikisha mahitaji na sauti zao zinasikilizwa.”

HOJA YA KURUDI SHULE  

UNICEF inataja umuhimu wa Elimu ya Wasichana, kwamba ni hatua muhimu kwa, kupitia mwongozo wake ‘Kurudi Shule’ inayowapa fursa kinamama vijana kurejea shuleni baada ya kujifungua.

Inatajwa hiyo kushughulikia changamoto za kielimu, zinazowakumba wasichana wanaopata ujauzito na kuacha masomo. 

Ni mwongozo uliowahi kusitishwa, kiserikali na kurejeshwa tena na Rais Samia, alipoingia katika uongozi mwaka 2021.

Kurudishwa huko, sasa kunatajwa ni hatua kubwa kuelekea usawa wa kijinsia, kwani imewapa wasichana fursa ya kuendelea na elimu yao na kurejesha heshima yao. 

Inatajwa kuwaunga mkono kinamama na vijana, serikali ikiwasaidia kukamilisha masomo yao, pia inapunguza unyanyapaa unaohusiana na mimba za utotoni. 

Ni hatua inayowawezesha wasichana kurudi shuleni baada ya kujifungua, hivyo kuvunja mzunguko wa umaskini.

AFYA, ULINZI WA MSICHANA

Tanzania, hapa inatajwa na UNICEF imepiga hatua kubwa, kushughulikia mahitaji ya afya ya wasichana balehe. Dk. Lauren akisifu upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana.

Hapo anataja vigezo kama vile, chanjo ya HPV inayowakinga wasichana dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, ambayo ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo kwa wanawake duniani. 

Pia, kunatajwa huduma za afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati mkuu wa Tanzania kuboresha afya ya vijana, ikiwamo utoaji lishe bora na huduma za kinga.

“Mbinu madhubuti ya Tanzania kuhusu afya ya vijana, imehakikisha kuwa wasichana si tu wanakingwa dhidi ya saratani, pia wanasaidiwa kuboresha ustawi wao kwa ujumla,” anasema.

Kwa kushirikiana na UNICEF, Tanzania imeboresha huduma zake za afya, kukidhi mahitaji maalum ya wasichana wanapokua na kuingia katika utu uzima.

CHANGAMOTO ZINAZOENDELEA

Licha ya mafanikio makubwa, changamoto bado zipo. Mimba za utotoni na ndoa za utotoni bado ni vikwazo vikubwa kwa usawa wa kijinsia nchini Tanzania. 

Kwa kiwango cha mimba za utotoni cha asilimia 22, wasichana bado wanakosa fursa ya elimu na maendeleo wanayohitaji ili kufanikisha maisha yao. 

Ndoa za utotoni, ambazo mara nyingi husababisha kuacha shule mapema na fursa chache za maisha, ni changamoto nyingine inayoendelea.

Dk. Lauren anasisitiza kushughulikia changamoto hizo, kunahitaji suluhisho pana, ikiwamo upatikanaji bora wa elimu na huduma za afya. 

“Wasichana balehe mara nyingi wanakosa huduma zote wanazohitaji,” anasema kushughulikia pengo hilo,  itakuwa muhimu katika kufanikisha usawa wa kijinsia ambao Tanzania inautamani.

UNICEF ikishirikiana kwa karibu na serikali za mitaa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), inaeleza kuendeleza kukuza sera zinazowalinda wasichana na kuondoa mila hatarishi. 

Ni juhudi zinazolenga kuunda mazingira wezeshi kwa wasichana kustawi na kufikia ndoto zao.

WITO WA UONGOZI

Dk. Lauren pia anatafakari maendeleo tangu Mkutano wa Beijing wa 1995, uliowekwa kwa mtoto wa kike katika kitovu cha maendeleo ya kimataifa.

Hapo akabainisha kuwa, kuchaguliwa kwa Rais Dk. Samia, ni hatua muhimu katika safari ya kuongeza idadi ya wanawake viongozi Afrika Mashariki.

“Tunahitaji wanawake wengi zaidi katika nafasi za uongozi. Rais mmoja mwanamke haitoshi. Tunahitaji viongozi zaidi kama Mama Samia.”

Aidha, akatoa wito wa uwekezaji zaidi katika kuwawezesha wasichana, hasa kupitia maendeleo ya kiuchumi, elimu ya fedha, na ujenzi wa amani. 

Kiongozi huyo wa UNICEF anafafanua matumaini yake kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050 itajumuisha mipango ya kuhakikisha kuwa wasichana wanapata nyenzo na fursa za kuchangia katika ukuaji na ustawi wa taifa.

URITHI WA MONGELLA

Anataja maendeleo ya Tanzania katika usawa wa kijinsia, pia yanatokana na urithi wa viongozi anaotaja kwa mfano, 

Gertrude Mongella, Katibu wa Mkutano wa Beijing wa mwaka1995, uliojadili mustakabali wa maendeleo ya mwanamke duniani, sasa anatajwa alichangia kwa kiasi kikubwa kutetea elimu na uwezeshaji wa wasichana.

UNICEF wanataja juhudi zake zisizochoka, zilisaidia kuingiza ajenda ya mtoto wa kike katika sera za maendeleo ya kitaifa, ikiwamo Tanzania.

Dira ya Mongella haikuwa tu kuhusu elimu bali juu ya kuunda dunia ambapo wasichana wanaweza kufanya maamuzi kuhusu maisha yao ya baadaye. 

Kazi yake inaendelea kuhamasisha sera nchini Tanzania, zikihakikisha kuwa wasichana wanapata msaada na fursa wanazohitaji ili kufanikisha maisha yao.

TANZANIA INABAKI MFANO

Maendeleo ya Tanzania katika usawa wa kijinsia, sasa UNICEF inaitaja kuwa mfano kwa mataifa mengine. 

Kupitia uongozi wa maono, mabadiliko ya sera na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, Tanzania inajenga mustakabali mzuri kwa wasichana na wanawake wake.

Hata hivyo, changamoto bado zipo, na safari ya kufanikisha usawa kamili wa kijinsia itahitaji juhudi zinazoendelea.

Kwa uongozi wa Rais Dk. Samia na msaada wa washirika wa ndani na wa kimataifa, Tanzania inaendelea kuunda jamii ambapo kila msichana ana nafasi ya kufikia ndoto zake.

·      Makala hii ni yatokanayo na ziara yake nchini, Dk. Lauren Rumble, Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa Masuala ya Usawa wa Kijinsia.