Bima Toto Afya inavyomkamilishia Samia mkanda kuwajibika jamii kiuzazi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:27 PM Dec 19 2024
Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, akiwa katika tukio la kurejeshwa Bima ya Afya nchini, katika utaratibu mpya aliyoutangaza wiki hii.
Picha: Mtandao
Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, akiwa katika tukio la kurejeshwa Bima ya Afya nchini, katika utaratibu mpya aliyoutangaza wiki hii.

MOJA ya wasifu ambao Rais Dk. Samia Rais amekuwa akijinadi nao kiutawala, kisiasa na wanajamii, ni katika nafasi yake kijinsia kama mama na anawajibika katika wasifu huo.

Kadri akifuatiliwa matendo yake kiutawala, huangukia katika wajihi huo kuanzia nasaha zake, matendo hadi utekelezaji.

Ikiangaliwa kwa kina nyendo hizo, kuna nafasi ya uzazi, mahususi kiafya. Mwaka huu ukihitimu kuna hoja na vielelezo vingi katika ngazi ya utekelezaji kiafya, mbali na ujenzi wa majengo ya vituo vya afya na hospitali, vifaa na kuelimisha wataalamu.

Ni utendaji unaopata urafiki kutoka kwa mtangulizi wake, Dk. Jakaya Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne na mstaafu pekee aliye hai katika nchi na watano waliomtangulia Dk.Samia.

Dk. Kikwete katika afya, ana wasifu na rekodi kuwa mwasisi wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) uliobuniwa mwaka 2007 na kuanza kufanya kazi 2008.

Kwa sasa, mstaafu Dk. Kikwete ni Mjumbe wa Bodi ya Menejimenti nchini ya tawi la shirika la kiafya kimataifa, Nutrition International (NI), akiwa na mchango wa kuwezesha nyendo hizo, ikifaidisha utawala  wa Rais Dk. Samia.

Mnamo Machi mwaka huu, ikaipatia 

Wizara Afya vidonge vya matone ya Vitamini A milioni 22, kwa ajili ya kuwapatie watoto walio na umri chini ya miaka mitano, ziwafikie jumla yao milioni 11 kwa ajili ya kuwaongezea kinga ya mwili na kuimarisha afya yao ya macho.

 Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel, ambaye kitaaluma ni tabibu wa binadamu, akahimiza: “Wazazi zingatieni lishe bora kwa watoto tangu wa utangaji wa mimba na kuwa na desturi ya kula mlo bora kwa mama wajawazito.

“Hii itamsaidia mtoto hata baada ya kuzaliwa na wakati yuko shule ubongo na akili yake kufanya kazi kikamilifu, pia itamkinga na magonjwa ya mara kwa mara,” anasema Dk. Mollel. 
 
Pia, Dk. Mollel anafafanua kuwa, pia Rais Dk. Samia ameelekeza fedha shilingi. bilioni 99 za kuajiri na posho za wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ambao wamekuwa msaada mkubwa wa kufikisha elimu ya lishe na afya bora.

KUTIBU NA KUSOMESHA 

Hilo linatokea, huku Rais Dk. Samia katika uzazi wake huo, mnamo Februari, mwezi mmoja kabla ya kupokea dawa hizo za msaada, aliahidi kumsomesha mtoto Alhaji Abdallah (10) na wadogo zake watano.

Ni uamuzi wake, baada ya kutaarifiwa mtoto kuacha shule akiwa darasa la tatu, kutokana na ugumu wa maisha na kulazimika kuuza ndizi, ili kuisaidia familia yake ya watu sita. 

Hapo akaahidi kumpatia kiwanja na kumjengea nyumba mama yao, Ester Hussein, aliyekuwa mgonjwa.

Ni tukio la mkoani Kigoma, pale mtoto Alhaji aliomba kipaza sauti katika mkutano wa aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, kuwasilisha kero yake, akiomba awezeshwe kupata elimu kwa kuwa mama yake hana uwezo akiumwa maradhi ya kuvimba tumbo.

Makonda baada ya kumsikiliza, alimwahidi CCM ingemsomesha na akaanzisha mchango wa papo kwa hapo kumsaidia, ikapatikana shilingi milioni 2.22.

Siku iliyofuata, Makonda akaenda kuitembelea familia hiyo na kumpatia ujumbe wa Rais Dk. Samia kuwasaidia familia hiyo watoto wote watano na kulipia vifaa vyote vya shule na sare.

"Rais Samia ameguswa na maisha ya Alhaji, ameona upendo aliona namna alivyokuwa anapigania maisha ya mama yake na wadogo zake na kipaji chake ya biashara, kwa sababu alikuwa anatunza fedha kutoka Sh. 4,000 hadi kufikia Sh. 20,000,” akasema.

Akafafanua, Rais Dk.Samia amemtuma kumfahamisha Alhaji, kwamba watajengewa nyumba ya kifamilia na ingekamilika ndani ya mwaka huu.

Kwa mujibu wa Makonda, ni jozi inayokamilika kwa kuwekwa vifaa kama viti, meza na vitanda na mama huyo kupata mtaji wa biashara shilingi milioni tano na kugharamia matibabu, akihakikishiwa kufanyiwa uchunguzi sahihi.

ATOA OFA TIBA

Iikiwa kama nyendo zake za kawaida mnamo Aprili mwaka huu, mara nyingine akatoa ofa kudhamini tiba ya wagonjwa 100 wanaosumbuliwa na tatizo la mgongo wazi.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, mgongo wazi na kichwa kikubwa, ni tatizo linalowapata watoto, chanzo kikiwa ukosefu wa madini ya foliki asidi.

Akitoa ufafanuzi mjini Dar es Salaam, Waziri Ummy akatamka: “Rais Samia amenielekeza nilete pesa kwa ajili ya watoto 100, ambao wangefanyiwa   upasuaji wa kichwa kikubwa na mgongo wazi bure kwa gharama zake.

“Kwa hiyo, Profesa (Abel) Makubi (Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma). Wasiliana na Chama cha Wazazi na Walezi wa Watoto Wenye Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi Tanzania, kujua watoto hawa ndani ya wiki moja, mbili Wizara italeta hizo fedha.”

Ni katika picha hiyo ya kile kinachojiri mwaka huu, suala la uamuzi kuhusu bima ya afya kwa watoto, ni mwendelezo wa mengi ya uzazi na ulezi kutoka kwa Rais Dk. Samia, ikiwa ni zaidi ya majukumu yake ya kawaida.