Bendi za dansi, Kibisa zilivyotikisa enzi za Mwalimu Nyerere

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:39 PM Oct 12 2024
Bendi.
Picha:Mtandao
Bendi.

"Tumeonewa kiasi cha kutosha. Tumenyonywa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliosababisha tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka Mapinduzi. Mapinduzi ya kuondoa unyonge, ili tusionewe tena na tusipuuzwe tena".

 Yalikuwa ni baadhi ya maneno ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akitangaza Azimio la Arusha mwaka 1967, ambaye Jumatatu ijayo anatimiza robo karne, yaani miaka 25 tangu alipofariki nchini Uingereza, 1999, akiwa na miaka 77.

Azimio lilipitishwa kwenye mji wa Arusha (sasa jiji) mwishoni mwa Januari mwaka 1967 na kutangazwa rasmi, Dar es Salaam, Februari 5 mwaka huo huo.

Katika misingi yake ilikusudia kulinda Uhuru wa Taifa, lakini sio tu Tanzania, bali na mataifa ya jirani ambayo kwa wakati ule yalikuwa katika tawala za kikoloni, misingi yake ililala katika ukombozi wa Afrika na Taifa na kufanya kuwa watu wa taifa huru pasi kuingiliwa na mabepari.

Pili ilikuwa kurudisha mali zote zilizokuwa zinamilikiwa na mashirika binafsi kuwa mali za serikali, maarufu kama mali ya umma zitakazomilikiwa na wakulima na wafanyakazi.

Kwa kutambua umuhimu huo, serikali ilihimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuzuia wanyonyaji.

Hapo ndipo nchi ilipoanza kwa kutaifisha mali za mabepari ambazo walikuwa wamejilimbikizia, pia kuanza kuanzishwa makampuni na kujengwa viwanda mbalimbali.

Ndipo vilipokuja viwanda, mashirika na makampuni mengi ambayo mbali na kufanya makubwa, lakini mengi yalimiliki timu za mpira wa miguu, netiboli, ndondi, mpira wa wavu, na hata bendi za muziki wa dansi, kwaya na taarabu.

Vile vile baadhi ya wamiliki hata vikundi ya ngoma za utamaduni ambazo kwa wakati huo vyote vilibatizwa jina la 'Kibisa', kutokana na kundi moja bora kabisa la aina hiyo, lililokuwa likimilikiwa na Shirikika la Maendeleo Dar es Salaam (DDC). Kundi hilo liliitwa DDC Kibisa Ngoma Troupe. Ndipo kwa kufupisha tu mashabiki waliita Kibisa kila kikundi ya utamaduni hata kama kilimilikiwa na kampuni au shiriki lingine.

DDC pia ilimiliki bendi ya muziki ya dansi maarufu hadi leo, DDC Mlimani Park Orchestra, ikiwa na mtindo wake wa Sikinde Ngoma ya Ukae.

Tukirudi kwenye mada halisi, ni kwamba baada ya maneno ya Mwalimu, utekelezaji ukafanyika kama nilivyoanisha kuutaifisha na kuunda Mashirikika na Makampuni mengine, lakini pia watu walihimizwa kufanya kazi kwa bidii, na kuundwa na Vijiji vya Ujamaa.

Kwa kumuunga mkono, wanamuziki wa Tanzania hawakukaa kimya, kwani baada ya Azimio la Arusha walitunga na kuimba nyimbo nyingi sana kuunga mkono na kuwahimiza wananchi kufanya kazi na hata kwenda kujiunga na Vijiji Vya Ujamaa. 

Ujamaa ulitamalaki, lakini kuna baadhi walikuwa wakiupiga vita, lakini Mwalimu Nyerere alikaa imara kuueleleza. Kurugenzi Jazz Band ya Arusha, wakatoa wimbo unaitwa 'Ujamaa' wenye maneno yafuatayo.

"Matumaini yenu Waafrika ni siasa ya Ujamaa. Njama mbinu za hali ya juu kuangusha ujamaa. Ujamaa ni mzuri kwenye kuleta usawa. 

Tutaendelea hatutarudi nyuma. Tulikwishajua matatizo kutashinda. Mawazo sahau ujamaa utakufa. Fungeni vibwebwe tujenge ujamaa." Nchi ilikuwa ya kijamaa kweli kweli.

NUTA Jazz Band, wana Msondo Ngoma, haikubaki nyuma, nayo ilitoa wimbo unaitwa 'Kijiji cha Ujamaa'
"Ndugu zangu, mimi sina kazi, sasa nitapata tabu. Siku nyingi nimefanya bidii, ili niweze kupata kazi, kujitahidi ndiyo nimeiharibu kazi, ndiyo siipati. Sasa nitafanya nini mie, ooo, nakufa.

'Ndugu zangu wamenieleza niende katika kijiji cha ujamaa, nikajiunge na wenzangu, nipate mahitaji yangu, shida ziniondoke. Kwa sasa naondoka, nakwenda zangu, katika Kijiji cha Ujamaa, nimechoka sasa mwenzenu na mambo ya mjini."

Yalianza kufa kwenye miaka ya 1990 baada ya kuanza kushindwa kujiendesha, na yakawa yanaleta hasara.
Kuna sababu nyingi, ikiwemo kuwa na wafanyakazi wengi kuliko uwezo wa kuzalisha.

Mengine yalibinafsishwa na sasa yapo mikononi mwa watu binafsi. Yapo ambapo serikali imeingia ubia na watu binafsi, maarufu kama wawekezaji. Machache sana ndiyo bado yanamilikiwa kwa asilimia mia moja na serikali, mfano Shirikika la Ugavi wa Umeme, 

TANESCO.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa timu za michezo mbalimbali, na bendi kuvunjika, lakini pia hata Siasa ya Ujamaa ndipo ilipoanza kulegalenga.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akipiga ngoma, ikiwa ni ishara ya kuenzi utamaduni wa Kitanzania na Mwafrika kwa ujumla, na ilionekana kipindi chake wakati kulipokuwa na bendi nyingi za dansi zilizokuwa maarufu na zenye nguvu, Pamoja na vikundi ya utamaduni na sanaa, ikiwemo DDC Kibisa Ngoma Troupe.

Tuma meseji 0716 350534