WARAIBU 935 wa dawa za kulevya wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, wamefikiwa na elimu ya kujitambua baadhi wakiachana na dawa huku wakifahamu na kudai haki zao za msingi za kibinadamu.
Ni katika kipindi cha mwaka mmoja wa 2024, ikianza kutolewa mwanzoni mwa mwaka huu na shirika la kuhudumia waraibu la Life & Hope Rehabilitation Organisation (LHRO) katika kata tano wilayani humo.
Haki wanazostahili ni kupata bure methadone dawa za kuulazimisha mwili kuachana uraibu wa dawa za kulevya kutoka vituo na hospitali za umma.
Hayo yamo katika taarifa ya hitimisho la mradi wa utoaji elimu iliotolewa na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Al-karim Bhanji mbele ya wadau wanaohudhuria mkutano wa kuhitimisha mradi huo mjini Bagamoyo hivi karibuni.
Kingine ni kuthaminiwa katika jamii na kupewa huduma muhimu za afya, elimu upendo.
"Ndani ya mwaka huu mradi umefikia waraibu 935, wa kike 29 ambao wote tumewapa elimu ya kujua haki zao za msingi katika kata za Dunda, Magomeni, Kisutu, Nianjema na Kiromo," anasema Bhanji.
Anasema LHRO ilipanga kufikia waraibu 800 lakini ikavuka, kwa maelezo kwamba fedha za mradi kutoka kwa wafadhili zilifika kwa wakati, walipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watumishi wa serikali na pia uboreshaji wa mafunzo kwa watoa elimurika.
Anasema elimu waliotoa imesaidia waraibu 422 kubadili tabia na kuanza kutumia dawa ya methadone, wa kike wakiwa 11 na wengine 513 wakiwa bado hawajafikia uamuzi wa kuanza dozi ya methadone.
Bhanji anasema suala la kuamua kuacha dawa hizo, linategemea utayari wa mhusika na kwamba iwapo LHRO itapata fedha nyingine toka kwa wafadhili watarudi Bagamoyo kuendelea kutoa elimu ili kusaidia vijana kuacha dawa za kulevya na pia kupunguza unyanyapaa dhidi yao.
UTEKELEZAJI
Bhanji anasema ili kufikia malengo ya mradi, afua mbalimbali zilitekelezwa kupitia semina elekezi, elimu ya mtu mmoja mmoja, mikutano ya hadhara, kupitia vyombo vya habari, mahubiri ndani ya nyumba za ibada, ushirikishwaji wa waraibu na elimu kwa makundi rika.
Anasema wamefikisha elimu hiyo kwenye shule tisa zikiwamo tano za msingi, vijiwe 14 vya bodaboda, masoko manne, makanisa matatu, misikiti sita mahakama mbili, vituo viwili vya polisi na polisi kata wote wilayani Bagamoyo.
"Tulitoa elimu kwa polisi kata na dawati la jinsia wote wa wilayani Bagamoyo, tukijikita kwenye suala la unyanyapaa, kwa sababu walikuwa wakilaumiwa kukiuka haki za waraibu," anasema.
Anasema wamezifikia masikani 18 za waraibu na pia wametoa elimu kwa makundi mbalimbali ili yaunge mkono jitihada za kuokoa waraibu wa dawa za kulevya na pia kuondoa unyanyapaa dhidi ya kundi hilo.
"Wengine waliopata elimu ni watendaji wa kata, watumishi wa halmashauri ambao ni watekelezaji wa sera mbalimbali za afya na uchumi katika wilaya ya Bagamoyo," anasema.
Anafafanua kuwa shirika lilitoa fursa kwa vijana wawili kutoka kila kata yenye mradi ambao walikuwa wakipata huduma ya upataji nafuu na kuwajengea uwezo kuhusu namna ya kutekeleza mradi ili wasaidie waraibu kubadilika.
"Tunawashukuru Mfuko wa U.S. Ambassador Fund for HIV/AIDS Relief (AFHR Grant) and Pepfar kwa kufadhili mradi huu na wadau wengine ambao wamechangia kuufanikisha," anasema.
Anasema wadau hao wengine anaowataja kwa majina ya CDC, THPS wanaopambana na UKIMWI kwa ajili ya kuendeleza miradi ya MAT Clinic, kwamba wamechangia kufanikisha elimu hiyo.
"Lakini pia tuna ombi kwa serikali kwamba iendelee kuwatumia waelimishaji rika waliowezeshwa ili nao waendelee kuelimisha na kuibua na kufuatilia waraibu walio kwenye huduma za methadone na wanaotumia dawa za kufubaza VVU," anasema.
Anaongeza kusema; "Pamoja na hayo, shukrani zetu zifike kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamayo, ofisi ya mganga mkuu, ustawi wa jamii, watendaji wa vituo vya afya, ofisi ya mkuu wa polisi wilaya kwa kuwa nasi kila hatua ya utekelezaji wa mradi huu," anasema.
USHAURI WA WADAU
Mganga Mkuu wilaya hiyo, Dk. Kandi Lussingu, anawataka LHRO kuendelea kushirikiana na serikali kwa kubuni shughuli mbalimbali ambazo vijana walioacha dawa za kulevya wanaweza kuzifanya.
Dk. Kandi anasema vijana walioacha dawa hizo wakiendelea kuishi katika mazingira ya awali yaliyosababisha wakatumia dawa hizo, wanaweza kujikuta wakarudia uraibu.
"Hivyo, wito wangu kwenu LHRO, mjaribu kubuni hata miradi midogo ambayo wanaweza kuifanya na kujiingizia kipato, ninaamini serikali itawaunga mkono katika jambo hili," anasema Dk.Kandi.
Anaongeza kuwa ikiwezekana, waanzishe darasa kwa ajili ya kutoa elimu ya uzalendo kwa vijana hao kwa nchi yao na kuwafundisha nyimbo zinazohamasisha uzalendo.
"Mkifanya hivyo mtakuwa mmewasaidia, sisi kwa upande wetu tunaendelea kuwapokea na kuwapa dawa za methadone, lakini wadau kama nyie mwendelee kutusaidia kwa kubuni mbinu ambazo zitawawezesha kuwa raia wema," anasema.
Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo, Veronica Salala, anawataka polisi kata wote kuwatambua vijana walioacha uraibu katika maeneo yao na kuweka mikakati ya kuhakikisha hawarudi kwenye vitendo hivyo.
"Mnaweza kuwa mnaonana nao kila mara na kuwahamasisha muhimu wa kufanya shughuli halali za kujipatia kipato badala ya kushinda vijiweni ambako ni hatari kwa maisha yao," anashauri Veronica.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED