Wawili wauawa kwa kushukiwa majambazi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 08:06 AM Jan 11 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilbrod Mutafungwa.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilbrod Mutafungwa.

JESHI la Polisi mkoani Mwanza limethibitisha kuua watu wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi, katika jaribio la kuiba nyumbani kwa mfanyabiashara, wakiwa wamevalia mavazi ya kike kuficha jinsia na mwonekano wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilbrod Mutafungwa, alithibitisha jana kuwa watu hao ambao ni wanaume, waliuawa kwa risasi na polisi waliokuwa katika doria juzi saa 2:45 usiku.

DCP Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea katika Mtaa wa Kabambo, Kata ya Kiseke wilayani Ilemela na watu hao walikuwa wamevalia magauni na vilemba.

Alisema walivamia nyumbani kwa Flora Sungura Abdallah (42) na kuingia ndani wakati mfanyabiashara huyo anafunguliwa geti akitoka kwenye shughuli zake za kibiashara.

“Watu hao walikuwa na bunduki aina ya Shotgun moja iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na risasi mbili na mapanga mawili. Baada ya hali hiyo, wakazi wa eneo hilo walipiga kelele za kuomba msaada na taarifa hizo kufika kwa askari polisi waliokuwa doria eneo hilo,” alisema.

Kamanda Mutafungwa alisema baada ya askari kufika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada na kuwataka watu hao kujisalimisha, walikaidi amri na kutaka kuwadhuru wakazi wa nyumba hiyo pamoja na askari.

“Ndipo askari walifyatua risasi, hivyo kusababisha watu wawili ambao mmoja alishika bunduki na mwingine akiwa na panga kujeruhiwa kwa risasi hizo na kupoteza maisha papo hapo,” alisema.

Kamanda Mutafungwa alisema miili ya watu hao ambayo haijatambuliwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando ikisubiri utaratibu wa utambuzi na uchunguzi wa kitaalamu.

Alisema  katika tukio hilo hakuna mali iliyoibwa na kuwa jeshi hilo likakamata silaha aina ya shotgun moja, mapanga mawili na begi la mgongoni likiwa na suruali, shati, bisibisi na viatu.

Kadhalika, alisema watu wawili wa jinsia ya kiume wanaodhaniwa pia kuwa majambazi walitoroka kwa kutumia usafiri wa pikipiki ambayo namba za usajili hazijafahamika.

“Tunaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watu hao waliokimbia na watu wengine ambao walipanga na kuratibu tukio hilo la kihalifu unaendelea ili kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema DCP Mutafungwa.