MKAZI wa Mtaa wa Sawe, Kata ya Maisaka katika Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani Manyara, Yona Angres, amepoteza maisha, baada ya kudaiwa kunywa pombe nyingi za kienyeji kupita kiasi.
Jana, Kamanda wa Polisi wa mkoani Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Ahmed Makarani, alisema Angres alifariki dunia kwa kuzidiwa na kiwango cha kilevi kinachotokana na pombe kali za kienyeji, ambazo hazina uthibitisho wa kisayansi. Aisema polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya kifo hicho.
Alipotafutwa kuzungumzia matumizi ya vilevi kwenye eneo lake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sawe, John Paul, alisema Angres alifariki dunia baada ya kunywa pombe nyingi za kienyeji zinazotengenezwa holela katika mji huo.
"Baadhi ya watu waliokuwa naye kwenye eneo hilo, walisema huyo jamaa (Angres) alikunywa pombe nyingi za kienyeji na kufariki dunia baada ya muda mfupi," alisema Paul.
Mmoja wa mashuhuda, Isack Dere, alisema Angres alianza kunywa pombe hizo tangu asubuhi na ilipofika jioni, ndipo alipozidiwa na kupoteza maisha.
Kutokana na tukio hilo, aliitaka jamii ya eneo hilo kunywa pombe zilizothibitishwa na mamlaka na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kupata alama ya ubora na kupata uthibitisho wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuliko kunywa pombe zilizotengenezwa holela.
"Hapa Babati kuna kiwanda kizuri cha vinywaji changamfu ambacho kina uthibitisho wa ubora wa viwango. Sasa kwa nini mtu unakunywa mataputapu hadi ufariki dunia kabla ya muda wako?" alihoji Dere.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Asia Juma, alisema Angres ni kijana aliyekuwa anafanya vibarua mbalimbali ikiwemo kusomba maji na kulipwa fedha.
"Nadhani siku hiyo hakula chakula kisha akashiba ndiyo sababu akafariki dunia kwa kunywa pombe nyingi za kienyeji kupita kiasi," alisema Asia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED