VIJANA wanne kutoka Kanda ya Ziwa, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka 49, likiwamo la wao kujitangaza ni viongozi wa serikali na kufanikiwa kujipatia Sh, milioni tano.
Vijana hao ni Eradius Rwechungura (43), mfanyabiashara mkazi wa Kiseke, Mwanza; Heri Kabaju (37), maarufu kama ‘Babylon’ mvuvi mkazi Rwamisheni Kagera; Abdurahim Karugula (42), maarufu kama Obra, dereva na mkazi wa Kahoro na Eradius Apornary (22), mkazi wa Kashai wote kutoka mkoani Kagera.
Wakili Mwandamizi Serikali, Nura Manja, amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, kuwa katika mashtaka 49 kati ya hayo 11, ni ya kujitambulisha kwa utambulisho wa mtu mwingine, mashtaka 13 ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine.
Mengine 23 ni ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na shtaka moja la kuongoza genge la uhalifu, huku shtaka la mwisho ni utakatishaji fedha.
Mshtakiwa Rwechungura anatuhumiwa kwa mashtaka 12; Kabaju anatuhumiwa kwa mashtaka 19; Karugula ana mashtaka matatu ya utambulisho usiokuwa wake, matano kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na mashtaka sita ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.
Mshtakiwa Apornary, anakabiliwa na mashtaka matatu ya kutumia laini ya simu, yenye jina la mtu mwingine mwinigine.
Katika shtaka la kwanza inadaiwa kati ya Oktoba Mosi na Desemba 31, 2024 eneo lisilojulikana nchini, washtakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu kwa lengo la kutapeli watu tofauti na kwa uongo kwa watu mbalimbali na kujipatia Sh. 5,000,000.
Mshtakiwa Rwechungura, anadaiwa kujitambulisha kuwa ni Ofisa kutoka Idara ya Rasilimali Watu katika Ofisi ya Katibu Tawala Wilaya ya Bukoba, kwa Eliberth Kalima na kuwa ni Ofisa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi katika Halmashauri ya Kahama mjini, kwa Filberth Mashim huku akijua si kweli.
Mshtakiwa Kaguja, anadaiwa wa kujitambulisha kuwa yeye Ofisa kutoka Mfuko wa Hifadhi wa Jamii PSSSF kwa Anunciata Mwageni, pia kuwa ni Ofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ili kupata taarifa za mwajiriwa Christopher Msemwa, na alidai kuwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, kwa Jesca Kibena.
Manja amedai kuwa Kabuja alijiwasilisha kuwa ni Ofisa Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Halmashauri ya Njombe Mjini, kwa Rustica Kayombo na Upendo Nsellu pia alijiwasilisha kama Mweka Hazina wa Idara ya Pensheni, kwa Lucas Nzota na kuwa angemsaidia kupata mafao yake huku akijua kuwa si kweli.
Mshtakiwa Rwechungura, anadaiwa kujiwasilisha kuwa yeye ni Ofisa Takwimu kutoka Halmashauri ya Tunduma Mjini, kwa Tupilike Mbwile, Ofisa Mradi kutoka Halmashauri ya Momba Mjini, kwa Elistulida Mwakyusa na Ofisa Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kwa Emmanuela Mwambichi.
Washtakiwa wanadaiwa walikuwa wakitumia laini zilizosajiliwa kwa majina ya Bazil Katono, Happyness Jems, Aziza Ramadhani, Royce Frenki, Sajda Abed, Valence Rwezaula, Ben Mhimbira, Benetson Rwenyagira na Sabitina Ally.
Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, ilidaiwa kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo katika maeneo yasiyojulikana nchini, kupitia kujiwasilisha kwao kwa uongo walijipatia fedha Sh. milioni tano kutoka kwa watu mbalimbali waliojitambulisha kwao.
Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, ambazo kwa kawaida husikilizwa Mahakama Kuu ama kwa kupewa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi katika kesi bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Februari 14, mwaka huu. Washtakiwa wote wamerudishwa rumande.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED