Viongozi wa dini wajitwisha jukumu kuzuia ndoa utotoni

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:32 AM Dec 04 2024
Sheikh Khamis Mataka.
Picha: Mtandao
Sheikh Khamis Mataka.

VIONGOZI wa dini wamesema wako tayari kutumia majukwaa yao kukemea ndoa za utotoni nchini.

Wamesema wako tayari kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu na uwezeshaji wasichana na kwamba kila msichana ana haki ya kulindwa dhidi ya ndoa hizo za utotoni.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam juzi wakati wa warsha iliyoshirikisha wadau mbalimbali wa kutetea haki za wasichana, viongozi hao wa dini walisema vitendo hivyo si vya kufumbia macho kwa kuwa vinasababisha athari mbaya kwa kundi hilo.

Sheikh Khamis Mataka aliomba serikali kuboresha sera na sheria ya ndoa, ili kuwalinda zaidi watoto wa kike ambao ndio waathirika wakubwa.

Hafla hiyo iliandaliwa na Msichana Initiative, Norwegian Church Aid (NCA) na Kamati ya Kudumu ya Madhehebu ya Haki za Kiuchumi na Uadilifu wa Uumbaji (ISCEJIC) kwa lengo kutambua umuhimu wa viongozi hao wa katika kuendeleza mapambao dhidi ya usawa wa kijinsia.

Sheikh Mataka alisema kuna haja ya serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ili kuzuia watoto wasiolewe katika umri mdogo.

"Hata maandiko ya kidini yanasisitiza kwamba ndoa inapaswa kuwa muungano wa heshima na wa hiari, si kulazimishwa kwa mtu yeyote," Sheikh Mataka alisema.

Mchungaji Monica Lugome wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), aliweka msisitizo kwa kanisa katika malezi bora ya mtoto kuhakikisha kuwa haki ya kila mtoto ya kupata elimu na maisha yenye kuridhisha inaheshimiwa.

"Kama viongozi wa dini, ni wajibu wetu kuongoza jumuiya zetu kuelekea haki na uadilifu. Ni wakati wa kukomesha mila potofu za ndoa za utotoni na kumpa kila msichana fursa ya kufikia ndoto zake," alisema.

Alisema upo umuhimu wa kuhakikisha wanaoingia katika ndoa ni watu wazima ambao tayari wamepevuka kukabiliana na ugumu wa changamoto mbalimbali na siyo watoto.

"Kulazimisha watoto kuingia katika ndoa kunawanyima haki muhimu za elimu na maisha yenye kuridhisha, kwani wanaelemewa na majukumu mazito ya kujenga familia katika umri mdogo," alisema. 

Sarah Shija ni Meneja Mipango wa NCA, alisema kukomesha ndoa za utotoni italeta mabadiliko makubwa katika uelewa kwa umma na mabadiliko ya kudumu kwa wasichana wa kitanzania.

"NCA wanaona kwamba bado kunahitajika juhudi ya kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kitabia, kuongeza ufahamu, na kuhamasisha jamii kuheshimu na kudumisha haki za watoto hasa wasichana ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali," alisema. 

Mtaalamu wa Programu ya Upatikanaji Haki kwa Wanawake wa UN Women Tanzania, Rachael Boma, alisema ni jukumu muhimu la viongozi wa kidini kuwalinda watoto na kuunda kanuni za kijamii na kitamaduni zinazoweza kusaidia kuzuia ukatili. 

"Viongozi wa kidini ni watu wanaoaminika katika jamii zao, wana nafasi ya kipekee ya kukuza ustawi wa watoto. Wanaweza kuzungumza dhidi ya mila mbaya kama vile ukeketaji, unyanyasaji, na kutelekezwa," alisema Boma.

Alisema pamoja na kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika kushughulikia suala hilo, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kutokomeza kabisa ndoa za utotoni kwa kurekebisha sheria zilizowekwa ili zitamke kwamba umri wa kuolewa ni kuanzia miaka 18.

Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Rebecca Gyumi, alisema kuna umuhimu mkubwa kuwashirikisha viongozi wa dini katika mapambano dhidi ya ndoa za utotoni.

"Kwa kuweka vita dhidi ya ndoa za utotoni kama suala la kimaadili na kidini, tunaamini itasaidia kuhamasisha mabadiliko ya kitamaduni ili kuhakikisha mtoto wa kike au msichana analindwa dhidi ya ndoa hizo za utotoni na anapatiwa haki zake za msingi," alisema.