NI siku ya hukumu! Baada ya tambo za muda mrefu, leo sanduku la kura linaamua nani awe Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Freeman Mbowe ameomba achaguliwe tena kukiongoza chama hicho, akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanasheria Tundu Lissu na Odero Charles. Wajumbe wa Mkutano Mkuu 1,328 ndiyo wamebeba si tu nafasi za watatu kisiasa, bali pia kinachotajwa hatima ya CHADEMA.
Kati ya wajumbe hao, ni 792 ni kutoka majimbo la uchaguzi, 124 wilaya za kichama, 68 mikoa ya kichama, 30 kanda za kichama, 99 wa mabaraza na 15 wa Kamati Kuu. Wote watawachagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar.
TIMU MBOWE, LISSU
Baadhi ya sababu zinazotolewa na wanaomuunga mkono Mbowe wanasema ni mbunifu, ndiyo sababu chama hicho kinaendelea kuwa imara kwa miaka mingi.
Baadhi ya hoja ambazo zimekuwa zikitolewa na wafuasi wanaomuunga mkono Lissu ni pamoja na mvuto alionao kutokana na sera zake zinazolenga mabadiliko ya kweli ndani ya chama na taifa lake.
Lissu, pamoja na mambo mengine, ameahidi kushusha fedha za ruzuku ya chama hadi ngazi ya majimbo, ukomo wa madaraka hasa kwenye nafasi za ubunge wa viti maalumu na ujasiri wa kupambana na vitendo vya rushwa ndani na nje ya chama chake.
SERA ZA ODERO
Mbali na Mbowe na Lissu, mgombea mwingine wa nafasi hiyo ya uenyekiti ni Odero. Ahadi zake ni pamoja na kuwawezesha watanzania kupata mahitaji manne muhimu ikiwamo uwezo wa kupata chakula bora, mavazi, makazi na uwezo wa kuwasiliana.
Nyingine ni kusimamia madhumuni ya chama chake, kushika dola, kupigania watanzania kwa kupinga tozo za miamala ya simu zisizoainishwa na serikali.
BARAZA KUU
Katika nyakati za lala salama jana, akifungua mkutano wa Baraza Kuu uliofanyika Dar es Salaam, Mbowe aliendelea kusisitiza kuwa hakuna mkubwa kuliko chama hicho huku akiwatahadharisha wanachama wasitoe nafasi kwa yeyote mwenye nia ya kukipasua chama hicho.
"Tusitoe nafasi kwa yeyote mwenye dhamira ya kukipasua chama, tumesema na ninarudia chama hiki kina thamani kuliko yeyote miongoni mwetu, kwani kimebeba ndoto za watanzania.
"Kwa hiyo ndugu zangu wana-CHADEMA, tumekuja Dar es Salaam si kupaniana, tumekuja kuyajenga, kwamba chama hiki tutakipigania, tutakijenga, tutakipanga, tunapotofautiana tutazungumza, ili mwisho wa siku kikabebe ndoto ya taifa letu ya haki, demokrasia kwa kila mmoja na hatimaye maendeleo ya watu wetu wote," alisema.
WALIOKATWA WALALAMA
Baadhi ya wagombea ambao hawakuteuliwa katika nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu, wamelalamika hawajatendwa haki huku wakiomba uchaguzi usimame mpaka majina yao yarejeshwe.
Wagombea waliokatwa ni pamoja na Mwangasa, Twaha Mwaipaya, Dk. Msofe, Rose Mayemba, Adamu Chagulani na Hossiana Kusiga.
Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika alitolea ufafanuzi jambo hilo, akisema: "Ninaomba kuhakikishia kuwa usaili na uteuzi uliofanywa na Kamati Kuu, Januari 19 mwaka 2025, ulifuata utaratibu uliopo katika katiba na kanuni za chama na kutumia demokrasia kama nyenzo ya uamuzi katika siasa."
Mkutano huo wa Baraza Kuu baada ya kufanya usaili, uliwateua Mbowe, Lissu na Odero kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa huku walioteuliwa katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara ni Ezekiah Wenje, John Heche na Mathayo Gekul na kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar walioteuliwa ni Hafidh Ali Saleh, Said Issa Mohammed, Said Mzee Said na Suleiman Makame Issa.
Jana, wenyeviti 17 wa mikoa walitangaza kumuunga mkono Mbowe, huku juzi wenyeviti 21 walitangazwa na mwanachama wa CHADEMA, Godbless Lema kuwa wanamuunga mkono Lissu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED